Alhamisi, 1 Mei 2014

TOSAMAGANGA HATARINI KUFUNGWA KWA UCHAKAVU


 Moja ya choo cha shule ya sekondari Tosamaganga ambacho kutokan na kutofanyiwa ukarabati hakifaa kutumika, kimetitia, kimebomoka na sasa kimebaki kuanguka/ Kuddondoka.
 Mmoja wa wanafunzi wa sekondari ya wavulana Tosamaganga akitoka katika jengo la choo ambacho hakifaa kwa matumizi kutokana na hatari iliyopo.

Ni moja ya majengo yaliyopo katika shule ya sekondari Tosamaganga, yakiwa yamechoka, na sasa yamesitishwa kutoa huduma ya kielimu.
Baadhi ya majengo ya sekondari Tosamaganga - yaliyositishwa kutumika baada ya kukithiri kwa uchakavu, jengo hili lilikuwa linatoa mafunzo ya kilimo na ufugaji "Cattle Unit" lakini sasa majengo yapo hoi bin taaban, inasemekana baadhi ya mawaziri na viongozi wakubwa wa serikali na vyama wamesoma hapa.

Paa la jiko la Tosamaganga ambalo lipo hatarini kuporomoka, ni jiko la ghorofa, na ubovu huo upo kwenye sakafu, ambayo ikitikishwa kwa kishindo inaporomoka "Ni hatari kubwa". 
 Moja ya jengo la shule hiyo likiwa na muonekano uliochoka, hatua hii ya uchakavu wa majengo inaweza ikawa inachangia kwa namna moja au nyingine kufifisha morali ya wanafunzi kupenda masomo.
 Eneo la jiko la shule ya sekondari Tosamaganga, ambalo limetitia na hivyo kuzua hofu ya kuporomoka kwa jengo hilo la Ghorofa na hivyo kusababisha majanga ambayo yanaweza kuzuilika.
 Jiko la shule ya Tosamaganga eneo ambalo ni hatari, na sasa limetitia, lakini muonekano wake si salama kiafya, kuna uwezekano mkubwa wa kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko "Kipindupindu" kutokana na hali hiyo ya uchafu, inayotokana na jengo hilo la ghorofa kutitia.
  Jiko la Tosamaganga, eneo ambalo linatumika kwa kupikia, ni juu ya ghorofa, ni hatari kubwa kwa usalama wa wanafunzi, walimu na hata watumishi mbalimbali wa shule hiyo, kama wapishi na wahudumu wa idara mbalimbali.






 Hii ndiyo Tosamaganga ambayo inasemekana baadhi ya viongozi mbalimbali wamesoma katika shule hiyo kongwe, ambayo ilianzishwa kabla ya Uhuru.
 Choo kimojawapo ambacho kipo katika hali mbaya, mbele yake ni bweni linaloendelea kutumika, nalo usalama wake upo mashakani.

 Mkuu wa shule ya sekondari ya Wavulana Tosamaganga Bw. Damas Mgimwa, akisoma taarifa ya shule hiyo katika mahafali ya 50 ya shule hiyo.
 Baadhi ya viongozi wa shule ya Sekondari ya wavulana Tosamaganga wakisikiliza jambo kwa umakini, kutoka kwa mkuu wa shule Bw. Damas Mgimwa, katika siku ya mahafali ya 50 ya shule hiyo Kongwe nchini.
 Mwenyekiti wa bodi ya shule ya sekondari Tosamaganga Bw. Pascal Mhongole akizungumza jambo katika mahafali hayo ya 50 ya kidato cha sita.
Afisa elimu sekondari Bw. Leonard Msigwa akitoa akijibu risala ya wanafunzi na mkuu wa shule, katika mahafari ya 50 ya kidato cha sita katika shule hiyo ya wavulana ya Tosamaganga.
Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita wa shule ya sekondari ya wavulana Tosamaganga wakisikiliza jambo wakati wa mahafali ya kuhitimu elimu yao.
Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita wa shule ya sekondari ya wavulana Tosamaganga wakisikiliza jambo wakati wa mahafali ya kuhitimu elimu yao. 
Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita wa shule ya sekondari ya wavulana Tosamaganga wakisikiliza jambo wakati wa mahafali ya kuhitimu elimu yao. 
Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita wa shule ya sekondari ya wavulana Tosamaganga wakisikiliza jambo wakati wa mahafali ya kuhitimu elimu yao. 

 <<<<<HABARI>>>>>


IMEFAHAMIKA kuwa shule ya sekondari ya Tosamaganga iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, huenda ikasitisha utoa wa elimu, baada ya kukabiliana na hali ya uchakavu wa majengo yake.

Hayo yamezungumzwa na wanafunzi wa shule hiyo, katika mahafali ya hamsini (50) tangu shule hiyo ianzishwe mnamo mwaka 1922, huku ikifanikiwa kutoa elimu kwa kundi kubwa la watanzania ambao baadhi yao ni viongozi wakubwa na watu wenye majina, ndani na nje ya nchi.

Dalili za kufungwa kwa shule hiyo, zimetajwa kuwa ni kutokana na uchakavu wa kiwango cha hali ya juu, kwa asilimia kubwa ya majengo yake ambayo kulingana na umri wa shule na sifa zake kitaifa na kimataifa shule hiyo haikupaswa kuwa katika muonekano huo wa aibu.

Florian Mwebesa ambaye ni katibu mkuu wa shule hiyo ya sekondari ya Tosamaganga upande wa serikali ya wanafunzi, amesema uchakavu wamajengo hayo unatokana na kutokukarabatiwa, huku jengo la mafunzo ya kilimo na mifugo “Cattle Unit” limefungwa baada ya majengo kuchakaa kupita kiasi.

“Majengo kama haya yamefungwa kwa miaka mingi, wakati hapo zamani yalikuwa yanatoa mafunzo ya elimu ya kijamii kama ufugaji wa Ng’ombe, Mbuzi, Nguruwe na shughuli za kilimo, jambo ambalo leo majengo haya yangekuwa kutusaidia kutupa elimu ya kujitegemea kwa kutambua namna ya ufugaji na ukulima,” Alisema Mwebesa.

Hii ni kero kubwa sana kwani shule hiyo haikutakiwa kufikia hatua hiyo, kwani imepitiwa na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali, ambao wanamaisha mazuri, lakini wameisahau kabisa shule hiyo pasipo hata kuisaidia japo ukarabati.

Mwenyekiti wa serikali ya wanafunzi Tosamaganga Dominic Kamugisha amesema baadhi ya majengo yamesitishwa kutoa huduma ya elimu, kutokana na uchakavu mkubwa yaliyonayo majengo hayo, huku Vyoo vya jengo la Mandela navyo vikiwa katika hatari kubwa.

Kamugisha amesema jengo la Mandela limesitishwa kwa zaidi ya miaka miwili, na lilikuwa linachukua wanafunzi wengi, na kufungwa kwake fulsa kubwa imefungwa kwa wanafunzi kupata elimu katika shule hiyo kongwe iliyokuwa na Historia nzuri ya kufanya vizuri katika mitihani yake mbalimbali.

“Hapa tunaona kila jengo linalokuwa chakavu  hatimayake linafungwa, hakuna jitihada zozote za kusema yakarabatiwe au yajengwe, sasa kwa mtindo huu wa kufunga yanapochakaa ipo siku tutasikia shule hii nzima imefungwa kwa sababu tu majengo yake yamechakaa, …Shule hii kuna kiongozi mkubwa wa kisiasa  amesoma hapa,  na anaifahamu vizuri sana historia ya shule hii, lakini yeye na wenzake wote waliopata elimu hapa wamefumba macho na wala hawataki kusikia juu ya kilio chetu sisi wanafunzi wa Tosamaganga, vyoo kwa asilimia kubwa ni vichakavu mno hadi vinatishia usalama wa sisi wanafunzi, na baadhi yake vimefungwa na haviruhusiwi kabisa kutumika,” alisema kamugisha.

Akisoma risala katika mahafali hayo, mwanafunzi Martin Mtama muhitimu wa kidatio cha sita amesema baadhi ya huduma muhimu kama Vyoo, mabweni ya kulala na upungufu wa vifaa vya usafi, huku ukosefu wa maji safi na salama wakidai kuwa ni hatari kubwa kwao.

Mwenyekiti wa bodi ya shule ya sekondari Tosamaganga Pascal Muhongole amewataka wananchi wote waliopita katika mikono ya shule hiyo kuona aibu juu ya hali ya majengo ya shule yao, na kuona umuhimu wa kuchangia kwa hali na mali ujenzi na ukarabati wa shule hiyo.

Afisa elimu Sekondari Wilaya ya Iringa, mwalimu Leonard Msigwa amesema  serikali pekeyake haiwezi kukabiliana na hali halisi ya uchakavu wa majengo hayo, na hivyo kuwataka wananchi na wale waliosoma katika shule hiyo kuona umuhimu wa kuichangia shule hiyo ili ifanyiwe ukarabati na hata ujenzoi kwa majengo ambayo yamechoka.

Msigwa amesema ni jambo jema kwa wale wote waliosoma katika shule hiyo kuona maendeleo waliyonayo, uchumi walionao na mafanikio yao msingi na chanzo kikuu ni shule hiyo ya Tosamaganga. 

"Nitoe wito kwa waliopita katika shule hii, waone kuwa Ustadi na maarifa waliyonayo vimetokana na shule hii, na pia wadau wengine wenye nia njema na elimu waone ni kwa njia ipi wanaweza wakachangia ili kuongeza nguvu na shule iweze kurudi katika sifa yake, kwani serikali pekeyake haiwezi kutoa huduma kwa majengo haya yalivyo," Alisema Msigwa.

Naye mkuu wa shule hiyo ya sekondari ya Tosamaganga Mwalimu Damas Mgimwa akisoma taarifa ya shule hiyo, amesema shule inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ukiwemo uchakavu mkubwa wa majengo.

Mgimwa amesema “Uchakavu ni mkubwa sana katika majengo, Mabweni, Madarasa, nyumba za walimu, Maabara, vyoo na hata ukumbi wa mikutano, lakini uchakavu wa jengo la kupikia yaani Jiko ni tishio kubwa ambalo wakati wowote linaweza kudondoka na kupelekea kutokuwa na sehemu ya kupikia,”.

Amesema mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo ya Wilaya ya Iringa ametoa jumla ya shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kufanya ukarabati fedha ambayo amesema itawasaidia kutatua baadhi ya changamoto japo kidogo.  

 
Kulingana na hali ya uchakavu wa vyoo, baadhi ya wanafunzi wanalazimika kujisaidia haja ndogo katika chupa za maji, ili kuepukana na adha ya huduma ya vyoo, kwani haviendani na hali halisi ya shule hiyo.

Licha ya vyoo, jiko la shule hiyo linalotumika kwa ajili ya kutoa huduma ya chakula kwa kundi hilo la wanafunzi, lipo katika hatari kubwa ya kudondoka, na kusababisha majanga yanayoweza kuepukika.

Hata hivyo afisa elimu Leonard Msigwa amesema kuna mpango mkakati wa kukarabati majengo  ya shule hiyo kongwe, ikiwemo ya Ifunda, ili kurejesha heshima na historia sahihi ya shule hizo kwa kuyaboresha mazingira yake ya utoaji wa elimu kuwa rafiki kwa walimu na wanafunzi.

Tosamaganga ilianzishwa mnamo mwaka 1922 na Kanisa Kathoriki ikiwa kama seminari chini ya Askofu Cagliero, ambapo mwaka 1930 ilianza kutoa elimu ya masomo ya sekondari, huku mwaka 1963 ilianza kutoa elimu ya kidato cha tano nacha sita,  na mwaka  1970 shule hiyo ilichukuliwa na serikali.

 MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni