Jumatano, 3 Desemba 2014

WAFINYANZI WALALAMIKIA ZANA DUNI ZA MIKONO

Bidhaa zinazotengenezwa kwa udongo.

Bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa kwa ugongo

WAFINYANZI wa kikundi cha wanawake  kilichopo Lungemba katika Wilaya ya Iringa, wameiomba serikali na wadau wa sekta ya uchumi na maendeleo,  kuwasaidia vifaa vya kisasa vya ufinyanzi, ili waweze kutengeneza vitu bora  vitakavyokubalika katika soko.

Hayo yamezungumzwa na wanawake hao wafinyanzi wa Lungemba, walipotembelewa na mkurugenzi mkazi wa Umoja wa Mataifa “UN” nchini Tanzania- Alvaro Rodrigues, katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya vikundi vya wajasiriamali, inavyosimamiwa na shirika la kazi duniani chini ya mpango wa uwezeshaji wa kiuchumi katika sekta isiyo rasmi.

Anna Nyongole ni mmoja wa akinamama wa kikundi cha ufinyanzi, amesema wanafanya kazi hiyo katika mazingira magumu, kwani bado wanatumia mikono pekee, badala ya kutumia vifaa vya kisasa, na hiyo inasababisha bidhaa zao  kukosa ushindani katika soko jambo linalowadumaza kiuchumi.

“Tunatengeneza Vyungu, Sufuria, majiko, Mitungi ya maji naya maua, na vitu mbalimbali, lakini changamoto yetu kubwa ni namna tunavyotengeneza, kwani hatuna mashine za kuumbia vitu hivyo wala hata mitambo ya kuchomea, tunaiomba serikali itusaidie, kwani tukipata vifaa vya kisasa tutaweza kutengeneza vitu vingi kwa muda mchache kuliko ilivyo sasa,” Anasema Nyongole.


Naye Zena Omary  amesema kukosekana kwa usafiri wa kusomba udongo, huwalazimu kutembea umbali wa kilomita 40 kwenda na kurudi, kutoka katika eneo la Ikekeke katika kijiji cha Kitelewasi, baada ya kukwama kulipia gharama za usafiri wa gari zaidi ya shilingi elfu 50.


“Tunakokwenda kuchimba udongo ni Ikekeke katika kijiji cha Kitelewasi, tunatembea km 20 kwenda na kurudi km 20, kwa hiyo unajikuta siku moja umeshindia kuchimba udongo na kusomba tu, napo hautosherezi maana huwa tunajitwisha kichwani,  huwezi kuchukua udongo mwingi,” Amesema Zena.

Aidha wafinyanzi hao wamesema pia kudumaa kwa soko lao kunachangiwa na baadhi ya jamii kubadili mtazano, juu ya matumizi ya vitu vya ufinyanzi, huku baadhi ya wananchi wakichukulia kama vitu hivyo kwa sasa ni kama mapambo tu,  hali hiyo ikiwa tofauti kabisa na siku za nyuma, ambapo vitu vilivyofinyangwa kwa udongo, vilitumika kwa shughuli za nyumbani kwa kiwango kikubwa.

“Hii hali ya mabadiliko inatusumbua sana, kwani wengi wanaokuja hapa ni wale wanaotaka vyungu vya mapambo na maua, hivi vya kupikia na mitungi ya maji haina wateja wengi, kutokana na watu kuacha kuitumia, kwa hiyo ukitengeneza vyungu na Mitungi unaweza kujikuta huuzi hata miezi mine hata sita huna hela,” Amesema Zena.


Licha ya kukabiliwa na changamoto mb alimbali, akinamama hao wamesema kupitia biashara hiyo ya ufinyanzi wamefanikiwa kuyabadili maisha yao, kwa kujenga nyumba bora na hata kuwasomesha watoto wao kwa kumudu gharama za ada.

“Hapa kila mmoja wetu anayo nyumba ya kisasa- ya tofari za kuchomwa na iliyoezekwa kwa bati, na pia tumefanikiwa kusogeza huduma ya maji ya bomba katika nyumba zetu, ili kupunguza usumbufu wa kuchota maji visimani, kama unavyoona bomba hiyo, kwa kweli biashara hii ya ufinyanzi imetusaidia lakini tukiboreshewa zaidi mazingira tutakua zaidi kiuchumi,” Walisema.

Hata hivyo Umoja wa Mataifa UN kupitia shirika la kazi duniani “ILO” Kwa mkoa wa Iringa pekee- limefanikiwa kuwasaidiaakinamama na vijana 1800 wa vikundi mbalimbali vya kiuchumi, huku wanachama wa vikundi hivyo wakipatiwa mikopo, elimu ya maambukizi mapya ya Virus vya Ukimwi,  pamoja na mafunzo ya ujasiriamali.

MWISHO 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni