Jumatano, 22 Aprili 2015

IGOWOLE SEKONDARI - SHULE ILIYOONGOZA KITAIFA YENYE CHANGAMOTO RUKUKI


WANAFUNZI wa shule ya sekondari Igowole- iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, wapo katika hatari ya kuangukiwa na majengo ya mabweni wanayolala, na hiyo ni kutokana na majengo hayo kutokufanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.


Licha ya uchakavu wa majengo, pia shule hiyo ya Sekondari Igowole inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ya uhaba wa vitanda, jambo linalowalazimu wanafunzi kulala zaidi ya  mmoja huku baadhi yao wakilazimika kulala sakafuni, kutokana na vubovu wa Vitanda na uhaba usiowiana na idadi ya wanafunzi.

Hayo yamezungumzwa na wanafunzi katika mahafali ya sita ya kidato cha sita, ya shule ya sekondari Igowole, ambapo suala la uchakavu wa majengo ya bweni yameonekana kuwa ni kero ambayo inawanyima usingizi wanafunzi hao.


Mwani Mwilenga, Magreth Mkane na Diana Balali ni wanafunzi wa kidato cha tano Igowole, wamesema mazingira magumu yaliyopo shuleni hapo, endapo hayatatafutiwa ufumbuzi wa kina, yanaweza kusababisha shule hiyo kushuka kitaaluma licha ya kuwa shule hiyo kwa sasa inaongoza Kitaifa kwa kushika nafasi ya kwanza katika matokeo ya kidato cha Sita- “Tanzania One”.

Naye Upendo Kopa na Consia Frenk ni miongoni mwa wanafunzi wanaohitimu elimu ya kidato cha Sita, wamesema pia changamoto ya shule kukosa uzio ni hatari kwa wanafunzi hasa wa kike, huku suala la huduma ya maji nalo likitajwa kuwapa wakati mgumu wa kujisomea.

“Mimi ninamaliza elimu yangu ya kidato cha sita leo, lakini hali ya shule hii ni mbaya, kwani mabweni yapo katika hali ambayo si nzuri, kwa maana si rafiki kielimu, pia huduma ya maji tunaipata mbali, kwa hiyo wakati mwingine wanafunzi tunaacha vipindi vya masomo na kufuata huduma hiyo,” Alisema Upendo.

...“Kuna wakati hapa shuleni ulizuka ugonjwa wanafunzi tuliugua na baadhi yetu kufikia hatua ya  kulazwa kwa ajili ya matumizi ya maji yasiyo salama, kwa hiyo tunaiomba serikali iiangalie kwa jicho la pekee shule hii, kwani mazingira haya magumu yanaweza kuporomosha taaluma,” alisema Consia.


Mwalimu Andrew Kauta ni mkuu wa shule ya sekondari Igowole, amesema katika kukabiliana na hali hiyo, mbunge wa jimbo la Mufindi Kusini Mendrad Kigola alitoa msaada wa bati 260 na  mifuko ya saruji 100.

Mwalimu Kauta amesema kupitia msaada huo kuna mpango wa ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 130 hadi 150, ikiwa pamoja na kununua vitanda zaidi ya 100 ambavyo vitagharimu zaidi ya shilingi Milioni 15.

Kauta amekiri kutokuwepo uwiano wa Vitanda, Mabweni na idadi ya wanafunzi, na kuwa kuna upungufu, na kuwa baadhi ya mabweni hayapo katika viwango vinavyotakiwa, na mkakati wa shule ni kubomoa majengo hayo ili kujenga majengo yenye ubora unaofaa.

Hata hivyo hali halisi ya vitanda hivyo ni chakavu, kwani baadhi yake havina hata ngazi ya kupandia, na hiyo ni kutokana na vitanda vya bweni kuwa vya ghorofa, na hivyo hali ya kukosekana kwa miundombinu ya kupandia kunawapa wakati mgumu wanafunzi, huku baadhi ya wanafunzi  wasio wazoefu kwao kuwa katika hatari ya kuvunjika wakati wakiparamia vitanda hivyo muda wa kulala.

Vipo vitanda ambavyo vimevunjika na hivyo kutoa fulsa kwa wanafunzi kutumia mbinu mbadala ya kuvifunga kwa kamba, na hali hiyo kuwa tishio kwa baadhi ya wanafunzi kuhofia kuanguka.

Aina ya milango ya mabweni niya Bati, na baadhi yake haina bawaba – nyenzo inasaidia  mlango ufunge na kufunguka, kwa hiyo wanafunzi huegesha tu mlango huo na wanapotaka kutoka au kuingia ndani huunyanyua kuingia nao ndani au kuuweka pembezoni.

Pia suala majengo ya bweni, ni mafupi hali ambayo mwanafunzi anayelala kitanda cha juu – humuwia vigumu kuendelea kujisomea, kwani paa lake linamzuia mwanafunzi kukaa na hiyo ni kutokana na bati kutomruhusu kunyoosha shingo.

Licha ya changamoto zote hizo zinazowakabili wanafunzi wa Igowole, kero ambazo pia ni changamoto kwa walimu,  lakini shule hiyo ya sekondari Igowole, imeweza kuuweka mkoa wa Iringa kuwa katika sifa ya pekee, kwa kung’ara - katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita, kwani shule hiyo imeshika nafasi ya  kwanza Kitaifa katika matokeo hayo ya mwaka 2014.

Basi kuna kila sababu - wadau mbalimbali wa elimu kwa kushirikiana na Serikali kufanya kila liwezekanalo ili kuziondoa changamoto za kielimu zinazoikabili shule hiyo kongwe ambayo inatakribani miaka 27 tangu ianzishwe, lengo likiwa ni kuyafanya mazingira ya shule hiyo kuwa rafiki kwa kufundishia na kujifunzia.

MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni