Jumatatu, 4 Mei 2015

VIONGOZI WALIOSOMA MALANGALI SEKONDARI- WAITELEWKEZA -MAJENGO SASA NI HATARI TUPU


INAFAHAMIKA Kuwa afya ni suala mtambuka, ambalo kama litaenda mrama iwe kwa uzembe, kupuuzia au kwa kukosa kipato cha kuboresha mazingira, linaweza kugharimu usalama wa maisha na hata kusababisha kifo.

Wanafunzi wa shule ya sekondari Malangali, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi- mkoani Iringa, wao wapo katika hatari yakupata magonjwa ya mlipuko, yatokanayo na uchafu,  ukiwemo ugonjwa wa Kipindupindu, na hiyo ni kutokana na vyoo vya shule hiyo ya sekondari ya Malangali kuwa na uchafu uliokithiri.

Miundombinu duni ya mazingira ya shule hiyo inatokana na uchakavu mkubwa uliopo, na hiyo nikutokana na shule hiyo kuwa na zaidi ya miaka 50 tangu ianze kutoa elimu mwaka 1928, licha ya ukweli kuwa ukongwe wa shule hiyo hauna thamani kwani ni kama imetelekezwa.

Wakizungumzia hali halisi ilivyo na namna wanavyokabiliana na mazingira ya shule hiyo, ewanafunzi wa shule ya sekondari Malangali wamesema usalama wa maisha yao- sasa wameukabidhi mikononi mwa mwenyezi Mungu na hiyo ni kutiokana na tatizo la vyoo kuwa ni sugu.


Kwa hali ya kawaida uchafu haujitengi na wadudu wanaopenda mazingira ya aina hiyo, kwani wanafunzi wa shule ya sekondari Malangali kwa sasa wanalazimika kulala Sakafuni na kuviacha vitanda kwa kuhofia taabu ya kuteswa na wadudu wanaoitwa Kunguni, huku baadhi yao wakikimbia mabweni na kuhamia katika vyumba vya madarasa kwa hofu hiyo ya Kunguni.


Shule ya sekondari Malangali ni miongoni mwa shule kongwe nchini ambazo zinajivunia kutoa viongozi mbalimbali hususani wa ngazi za juu serikalini, lakini mazingira yaliyopo hayawiani na sifa ya shule hiyo.

Thomson Ngunyali ni mkuu wa shule ya sekondari Malangali, anakiri kuwepo na changamoto ya miundombinu dhaifu ya vyoo na kuwa idadi ya vyoo vilivyopo ambavyo vilijengwa mwaka 1928 vilikuwa kwa ajili ya wanafunzi 280 na sasa wapo zaidi ya wanafunzi 700 – mara tatu ya idadi iliyotarajiwa awali.

Kuhusiana na changamoto ya wadudu Kunguni Mwalimu Ngunyali anasema uongozi wa shule umeanza kulifanyia kazi tatizo hilo, kwakupilizia dawa za kuua wadudu, licha ya kuwa wadudu haoi wamekuwa wakiibuka mara kwa mara.

Hali ya wanafunzi kimalazi katika Mabweni ya wanafunzi wa shule ya sekondari Malangali ni tishio kwa sasa, kwani wanafunzi kila asubuhi hulazimika kutoa vitanda nje ili kuwaua wadudu kwa njia mbadala ya nishati ya jua, huku dali la bweni nalo liking’olewa kama ni sehemu ya kutafuta mwarobaini wa kukabiliana na wadudu hao ambao chakula chao kikuu ni damu ya binadamu au mnyama yeyote awaye.


Changamoto hizo zimeainishwa na wanafunzi, katika mahafali ya 18 ya kidato cha sita wa  shule hiyo ya sekondari ya Malangali, ambapo jumla ya wanafunzi 96 wameingia katika mtihani wa kuhitimu elimu yao ya kidato ycha sita, katika shule hiyo ambayo inasifa ya kuwa na ufaulu mzuri, ikiongozwa na sekondari ya wasichana ya Igowole zote za Mufindi- Iringa.

Albert Chalamila muhadhiri wa chuo kikuu cha Iringa (Tumaini) miongoni mwa wanafunzi waliosoma katika shule hiyo ya Malangali sekondari, aliyehudhuria mahafali hayo kama mgeni rasmi wa mahafali hayo ya 18 ya kidato cha sita shuleni Malangali, amesema kuna umuhimu wa kufanya kongamano la wanafunzi waliosoma katika shule hiyo, lengo likiwa ni kuichangia shule hiyo ili kunusuru majengo yake yasianguke na kupoteza Historia nzuri ya shule hiyo.

Hata hivyo Malangali sekondari shule ni shule ya Serikali inayotoa elimu kwa wanafunzi wa kiume, huku safu kubwa ya viongozi wa ngazi za juu wakiwa wa,mepata elimu katika shule hiyo, elimu ambayo kwa sasa imeyopelekea mafanikio ya wao kuwa katika ngazi hiyo za juu za uongozi.

Basi kuna umuhimu kwa waliosoma katika shule hiyo ya Malangali Sekondari- kukumbuka fadhila na kuigeukia shule hiyo, lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali za uanzishwaji wa shule- jitihada ambazo leo zimezaa matunda kwa kuwapata viongozi hao waliotokana na shule ya sekondari Malangali.

MWISHO



Jumatano, 22 Aprili 2015

IGOWOLE SEKONDARI - SHULE ILIYOONGOZA KITAIFA YENYE CHANGAMOTO RUKUKI


WANAFUNZI wa shule ya sekondari Igowole- iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, wapo katika hatari ya kuangukiwa na majengo ya mabweni wanayolala, na hiyo ni kutokana na majengo hayo kutokufanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.


Licha ya uchakavu wa majengo, pia shule hiyo ya Sekondari Igowole inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ya uhaba wa vitanda, jambo linalowalazimu wanafunzi kulala zaidi ya  mmoja huku baadhi yao wakilazimika kulala sakafuni, kutokana na vubovu wa Vitanda na uhaba usiowiana na idadi ya wanafunzi.

Hayo yamezungumzwa na wanafunzi katika mahafali ya sita ya kidato cha sita, ya shule ya sekondari Igowole, ambapo suala la uchakavu wa majengo ya bweni yameonekana kuwa ni kero ambayo inawanyima usingizi wanafunzi hao.


Mwani Mwilenga, Magreth Mkane na Diana Balali ni wanafunzi wa kidato cha tano Igowole, wamesema mazingira magumu yaliyopo shuleni hapo, endapo hayatatafutiwa ufumbuzi wa kina, yanaweza kusababisha shule hiyo kushuka kitaaluma licha ya kuwa shule hiyo kwa sasa inaongoza Kitaifa kwa kushika nafasi ya kwanza katika matokeo ya kidato cha Sita- “Tanzania One”.

Naye Upendo Kopa na Consia Frenk ni miongoni mwa wanafunzi wanaohitimu elimu ya kidato cha Sita, wamesema pia changamoto ya shule kukosa uzio ni hatari kwa wanafunzi hasa wa kike, huku suala la huduma ya maji nalo likitajwa kuwapa wakati mgumu wa kujisomea.

“Mimi ninamaliza elimu yangu ya kidato cha sita leo, lakini hali ya shule hii ni mbaya, kwani mabweni yapo katika hali ambayo si nzuri, kwa maana si rafiki kielimu, pia huduma ya maji tunaipata mbali, kwa hiyo wakati mwingine wanafunzi tunaacha vipindi vya masomo na kufuata huduma hiyo,” Alisema Upendo.

...“Kuna wakati hapa shuleni ulizuka ugonjwa wanafunzi tuliugua na baadhi yetu kufikia hatua ya  kulazwa kwa ajili ya matumizi ya maji yasiyo salama, kwa hiyo tunaiomba serikali iiangalie kwa jicho la pekee shule hii, kwani mazingira haya magumu yanaweza kuporomosha taaluma,” alisema Consia.


Mwalimu Andrew Kauta ni mkuu wa shule ya sekondari Igowole, amesema katika kukabiliana na hali hiyo, mbunge wa jimbo la Mufindi Kusini Mendrad Kigola alitoa msaada wa bati 260 na  mifuko ya saruji 100.

Mwalimu Kauta amesema kupitia msaada huo kuna mpango wa ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 130 hadi 150, ikiwa pamoja na kununua vitanda zaidi ya 100 ambavyo vitagharimu zaidi ya shilingi Milioni 15.

Kauta amekiri kutokuwepo uwiano wa Vitanda, Mabweni na idadi ya wanafunzi, na kuwa kuna upungufu, na kuwa baadhi ya mabweni hayapo katika viwango vinavyotakiwa, na mkakati wa shule ni kubomoa majengo hayo ili kujenga majengo yenye ubora unaofaa.

Hata hivyo hali halisi ya vitanda hivyo ni chakavu, kwani baadhi yake havina hata ngazi ya kupandia, na hiyo ni kutokana na vitanda vya bweni kuwa vya ghorofa, na hivyo hali ya kukosekana kwa miundombinu ya kupandia kunawapa wakati mgumu wanafunzi, huku baadhi ya wanafunzi  wasio wazoefu kwao kuwa katika hatari ya kuvunjika wakati wakiparamia vitanda hivyo muda wa kulala.

Vipo vitanda ambavyo vimevunjika na hivyo kutoa fulsa kwa wanafunzi kutumia mbinu mbadala ya kuvifunga kwa kamba, na hali hiyo kuwa tishio kwa baadhi ya wanafunzi kuhofia kuanguka.

Aina ya milango ya mabweni niya Bati, na baadhi yake haina bawaba – nyenzo inasaidia  mlango ufunge na kufunguka, kwa hiyo wanafunzi huegesha tu mlango huo na wanapotaka kutoka au kuingia ndani huunyanyua kuingia nao ndani au kuuweka pembezoni.

Pia suala majengo ya bweni, ni mafupi hali ambayo mwanafunzi anayelala kitanda cha juu – humuwia vigumu kuendelea kujisomea, kwani paa lake linamzuia mwanafunzi kukaa na hiyo ni kutokana na bati kutomruhusu kunyoosha shingo.

Licha ya changamoto zote hizo zinazowakabili wanafunzi wa Igowole, kero ambazo pia ni changamoto kwa walimu,  lakini shule hiyo ya sekondari Igowole, imeweza kuuweka mkoa wa Iringa kuwa katika sifa ya pekee, kwa kung’ara - katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita, kwani shule hiyo imeshika nafasi ya  kwanza Kitaifa katika matokeo hayo ya mwaka 2014.

Basi kuna kila sababu - wadau mbalimbali wa elimu kwa kushirikiana na Serikali kufanya kila liwezekanalo ili kuziondoa changamoto za kielimu zinazoikabili shule hiyo kongwe ambayo inatakribani miaka 27 tangu ianzishwe, lengo likiwa ni kuyafanya mazingira ya shule hiyo kuwa rafiki kwa kufundishia na kujifunzia.

MWISHO

SERIKALI KUPUNGUZA UTITIRI WA KODI


 Ni naibu waziri wa fedha na uchumi Mh. Mwigulu Nchemba, akisikiliza jambo katika sherehe ya uzinduzi wa Vicoba Day, vikundi vya kiuchumi vilivyopo katika jimbo la Mufindi kaskazini.
 Mwigulu Nchemba akiwa na naibu waziri wa maliasili na utalii, Mahamood Mgimwa, ambaye ni mbunge wa jimbo la Mufindi kaskazini- Iringa. katika uzinduzi wa "Vicoba Day"
 Mwigulu Nchemba akivikwa vazi maalumu la kusimikwa kuwa kiongozi bora.
 Mwigulu Nchemba (katikati) akiwa na Mahamood Mgimwa (kushoto) na Isaack Kaganga mlezi wa vicoba jimbo la Mufindi Kaskazini.
 Mwigulu Nchemba akitete jambo na kanal Mkisi kamanda wa kikosi cha jeshi la kujenga Taifa JKT Mafinga, na kulia ni mbunge wa Mufindi Kusini Mendrad Kigola- siku ya uzinduzi wa "Vicoba Day"
 Kanal Mkisi - kamanda wa jeshi la kujenga Taifa JKT Mafinga akimsikiliza Mwigulu Nchemba naibu waziri wa fedha.

<<<HABARI>>>

SERIKALI imekili uwepo wa utitiri wa kodi kwa mfanyabiashara, na kuwa sasa kuna mpango wa kurekebisha mifumo yake ya ukusanyaji wa kodi na ushuru mbalimbali ili kupunguza mbinyo uliopo, ambao unaowafanya baadhi ya wafanyabiashara nchi, kushindwa kuendesha shughuli zao.

Hatua hiyo inakuja wakati wafanyabiashara kote nchini wakitumia mbinu mbalimbali, ikiwemo njia ya kusitisha utoaji wa huduma kwa wananchi - kwa kufunga maduka, kwa lengo la kuishinikiza serikali kubadili mfumo wake wa ukusanyaji wa kodi, ikiwa pamoja na kupinga ongezeko la kodi kwa asilimia 100.


Hayo yamezungumzwa na naibu waziri wa fedha Mwigulu Nchemba, katika mkutano baina yake na wanachama wa vikundi vya benki za wananchi waishio vijijini Vicoba, katika siku ya uzinduzi wa “Vicoba day”- vikundi vilivyopo jimbo la Mufindi Kaskazini- Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.

Mwigulu amesema utitiri wa kodi uliopo sasa unadumaza shughuli za mfanyabiashara, kutokana na mgawanyiko wa ukusanyaji wa kodi hizo, huku akidai kuwa wizara yake imeitaka Tamisemi, na wizara ya viwanda na biashara kuondoa usumbufu uliopo unaoilazimu kila idara kukusanya kodi.

Aidha Mwigulu amesema sasa serikali imefuta mfumo wa awali uliokuwa ukitoa mwanya kwa matajiri kusamehewa kodi, na masikini wakibebeshwa mzigo huo wa ulipaji wa kodi, jambo ambalo halikuwa linatenda haki kwa wananchi.

“Ule utaratibu wa misamaha ya kodi kwa matajiri tumeifuta,..maana unakuta mtu anachimba mafuta halipi kodi, lakini mama anayeuza Dagaa au vitumbua asubuhi na mapema anabanwa alipe kodi, huu utaratibu wa kumbana masikini alipe kodi ili kumuhudumia tajiri tumeuondoa, tunataka kila mmoja alipe kodi anayostahili,” Alisema Mwigulu.

Amesema mfumo huo wa ulipaji kodi licha ya kuwa ni mzigo kwa masikini pia ulikuwa unajenga tabaka la watu wenyenacho na wasionacho, na kuwa serikali kupitia mikakati yake imeanza kuondoa tabaka hilo kwa kujenga shule za sekondari kila Kata.

….Amesema awali kabla ya shule za kata hazijajengwa, baadhi ya mikoa ilikuwa na idadi ndogo ya shule za sekondari na hivyo kukosekana kwa mwamko wa elimu kwa wananchi wa maeneo hayo.

Ameongeza kuwa mpango huo wa shule za sekondari kila kata na ujenzi wa Zahanati, utasaidia kuondoa tabaka lililopo la wenyenacho na wasionacho kwa kuwa kila mwananchi atakuwa na upeo mpana wa kufikiri namna ya kuzifikia fulsa za kiuchumi.


Pia amesema wizara yake haitawavumilia watumishi wa aina yoyote ambao hawatakuwa waaminifu kwa fedha za umma, na akitolea mfano idara ya afya, Mwigulu amesema huko  baadhi ya watumishi wanatabia ya kuchepusha dawa, ambazo zimelipiwa fedha na serikali kwa lengo la kuwahudumia wagonjwa.

“Wizara inatoa fedha kwa ajili ya kununua dawa, lakini mgonjwa akienda Hospitali anaambiwa dawa hakuna kanunue, hizi zilizolipiwa na serikali amekunywa nani? Na wakati mwingine kule bungeni tunabanwa tutoe hela za dawa, lakini hospitali au Zahanati dawa hakuna, nani kanywa hizi dawa?, alihoji Mwigulu.


Hata hivyo Mwigulu amesema atapambana na Halmashauri zote ambazo hazitengi asilimia 10 ya fedha za mapato yake ya ndani – kwa ajili ya makundi ya wanawake na vijana, na ili kudhibiti hali hiyo wale watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa pamoja na kuwafukuza kazi watumishi wa aina hiyo

Kuhusiana na masuala ya kiuchumi- Mwigulu amewahimiza wanachama wa Vicoba kutunza kumbukumbu za mahesabu yao ili waweze kupata mikopo katika taasisi za kifedha, na kuwa serikali ipo katika hatua za mwisho kuvitambua kisheria vikundi hivyo vya vicoba.

MWISHO.



Alhamisi, 19 Machi 2015

ALIYETUMBUKIA MTO RUAHA APATIKANA- POLISI NA ZIMAMOTO LAWAMANI


 Baadhi ya wazamiaji binafsi wakitazama eneo lingine la kutafuta mwili wa Azimio, aliyetumbukia katika mto Ruaha mkuu.
                    Mto Ruaha mkuu.

 Marehemu Azimio enzi za uhai wake.
    Marehemu Azimio- enzi za uhai wake.
 Mwili wa marehemu Azimio ukiwa umeonekana.

 Mwili wa marehemu Azimio ukiwa umeopolewa majini.
 Baadhi ya wananchi wakiwa wameuzunguka mwili.



 Askari Polisi wakiondoka na mwili eneo la tukio kuelekea Hospitali kwa ajili ya uchunguzi.

<<<HABARI>>>

WANANCHI wa Kata ya Ruaha katika eneo la Ipogolo, ndani ya Manispaa ya Iringa - nusura wazue tafrani ya patashika na nguo kuchanika, baada kudai kuchoshwa na uzembe unaofanywa na baadhi ya Polisi.

Wakilalamikia hali hiyo kwa madai ya  kutelekezewa ndani ya maji mwili wa marehemu,  anayedaiwa kuuawa na kisha kutupwa katika mto mkuu Ruaha mkuu, mwili ambao umekaa katika maji kwa muda wa siku tano.

Marehemu aliyefahamika kwa jina la Azimio Mwanilwa ambaye kwa jina alilopewa na wazazi wake aliitwa “Augustino Mwanila”,  kifo kinadaiwa kilitokana na kipigo, kutoka kwa majambazi, ambao walimvamia, alipokuwa njiani akielekea vijijini kununua bidhaa ya biashara yake, tukio lililotokea katika barabara ya Ipogolo – Kilolo Wilayani- katika eneo la Chuo cha maendeleo ya jamii Tagamenda  Manispaa ya Iringa.

Wananchi hao walisema idara ya Polisi inayojihusika na matukio ya majanga na vifo katika kituo cha Polisi kati Iringa, pamoja na kikosi cha zimamoto, wamekuwa wazembe kutekeleza wajibu wao kwa wakati, jambo linalosababisha hasira na hivyo kutokuwepo kwa ushirikiano mzuri.

Akizungumzia hali hiyo kandokando yam to Ruaha mkuu - Rehema Kidava amesema tangu litokee tukio la kuzama majini kijana “Azimio”, hakuna ushirikiano wa aina yoyote kutoka kwa idara hizo za jeshi la Polisi, jambo lililowalazimu wananchi kuhangaikia shughuli za kuutafuta mwili huo majini.

Grace Mgimwa  na Grolia Mbimbi nao wamekinyoshea kidole Kikosi cha zimamoto Iringa, kwa madai ya kutokuwa bega kwa bega nao, katika shughuli hiyo ya uokozi wa mwili wa marehemu,  jambo ambalo limewalazimu wananchi kuacha majukumu yao na kushinda katika eneo hilo la mto Ruaha wakihangaika uuopoaji wa mwili.

Zenaide Nzeukia amesema kumekuwa na tofauti juu ya matukio ya ukamataji na matukio ambayo wananchi wanaomba msaada, hususani yanayohusisha vifo, huku akisema yale ya kukamata wauzaji wa dawa za kulevya, wanywaji wa pombe za jadi “Kienyeji”, na hata wachezaji wa michezo ya kamali – Polisi wamekuwa wakifika kwa muda muafaka, tofauti na matukio yanayotoa usaidizi kwa wananchi.

Yakob Fyimagwa mwenyeviti wa mtaa wa Buguruni – Ipogolo, miongoni mwa mitaa inayozungukwa na mto mkuu wa Ruaha katika eneo la tukio, amesema kinachoudhi ni baadhi ya askari wa vikosi hivyo vya Polisi - kupuuzia majukumu yao, kwa madai kuwa shughuli hiyo ya uokoaji wa mwili uliopo ndani ya maji ni yao Polisi kitengo cha Zimamoto.

Fyimagwa amesema endapo Polisi hao hawatabadili utendaji wao wa kazi, basi kuna hatihati ya kuvunjika kwa ushirikiano baina ya wananchi na jeshi hilo.

“Tunashangazwa kweli na hawa Polisi kuwa mpaka leo hii ni siku ya tano hawajafika katika tukio hili licha ya kuwa taarifa zilitolewa mapema siku ile ile ya tukio, lakini yangekuwa ni matukio yanayohusiana na ukamataji wa waharifu au hata wanywaji wa pombe za jadi huko vilabuni, wangekuja kwa wakati tena wakiwa wengi utadhani wanakwenda vitani, …kwani wanajua baada ya kuwakamata watuhumiwa wananufaika kwa kupewa chochote, lakini hapa siku ya tano hawajafika kama unavyoona tunahangaika tu, na msiba unakuwa mrefu kwa sababu tu ya uzembe wa baadhi ya watu wachache ambao wanalipwa mishahara kwa kazi hii,” Walisema wananchi.

Kwa upande wa wazamiaji binafsi wa majini waliokuwa wakiendelea na shughuli ya uogeleaji kuutafuta mwili wa Marehemu Azimio, wao walidai kuwa kuna umuhimu kwa Jeshi la Polisi kikosi cha Zimamoto na Maokozi - kuona umuhimu wa kuwawezesha vifaa, ili kuifanya kazi hiyo kwa utaalamu na tahadhari.

Fredy Kibasa, Paulo Kitamuka, Saimoni Magubike na Fredy Kilumbi ni miongoni mwa waogeleaji (Waokozi Binafsi) wa majini, wamesema mto Ruaha una wanyama mbalimbali kama Viboko, Mamba na wengine ambao ni hatari kwa usalama wao, lakini hulazimika kuifanya shughuli hiyo ndani ya maji pasipokuwa na kifaa chochote jambo ambalo ni hatari kwao, na lengo likiwa ni kuopoa miili ya watu isiharibike au kupotelea majini.

Naye Ismail Mlenga ( Baba Mwadhani) mlezi wa kikundi hicho cha Uokozi majini, alisema matukio ya majini hayana tofauti na maafa, na hivyo kuna umuhimu kwa taasisi zinazohusika na shughuli hiyo, kwa maana ya Polisi na kikoisi cha zimamoto kufanya kazi zao kwa weredi, kwa madai kuwa kutelekeza mwili wa mtu aliyetumbukia majini ni kuwapa wakati mgumu ndugu wa marehemu na wananchi, kuomboleza kwa muda mrefu wakati wakiendelea kutafuta maiti.

Baba Mwadhani amesema Kikosi cha zimamoto kinapaswa kijitadhmini upya katika utekelezaji wake wa majukumu, huku nao Polisi wakiacha tabia ya kufanyakazi kwa mazoea  na sasa wanapaswa kutekeleza wajibu wao ipasavyo, bila kusubiri kushinikizwa wala kusukumwa.

Kamanda wa kikosi cha Zimamoto mkoa wa Iringa, Keneth Komba alipotafutwa kwa njia ya simu - ili kujua nini kinawakwamisha kufanya kazi hiyo ya uokozi iliyopo ndani ya idara yao, alisema yupo safarini kuelekea mkoani Ruvuma- ambako amepata taarifa ya mzazi wake kuugua, huku akiahidi kulishughulikia jambo hilo, kwa kuiagiza ofisi yake ifike katika eneo hilo.

Siku ya tano mwili ukiwa ndani ya maji ya mto mkuu Ruaha- majira ya saa sita na dk 35 kikosi binafsi cha wazamiaji majini, kilifanikiwa kuuona mwili huo wa kijana Azimio, ambapo viongozi wa mitaa iliyopo eneo hilo la Ipogolo kwa njia ya Simu walitoa taarifa kituo cha polisi juu ya kupatikana kwa mwili huo, kama ni moja ya taratibu ya vifo vya aina hiyo.

lengo la utaratibu huo ni kutambua sababu za kifo na kisha wananchi kupata ridhaa kutoka kwa polisi, kuzika mwili na hiyo huwa ni mara baada ya Daktari kupima… – lakini hali ilikuwa tofauti, baada ya polisi tena  kudaiwa kuchelewa kufika katika tukio hilo, kwa takribani saa tatu, huku mwili huo ukiwa juani ukieendelea kubadili muonekano wake wa awali, jambo lililozua hasira kwa wananchi.

Mara baada ya askari Polisi kuwasili eneo hilo, kilizuka kituo kingine, kwani wananchi waliwataka polisi hao  wafike eneo la tukio – jambo ambalo baadhi ya askari walisema wanashindwa kulifikia eneo lililokuwa limewekwa mwili huo, kwa kile walichodai kuwa kuna maji na tope na hivyo kuwawia vigumu kupita katika mazingira hayo.

Tope hilo lililowakwamisha baadhi ya askari ni lile linalotokana na mto Ruaha mkuu kuchepusha maji yake mara baada ya mvua kunyesha, suala ambalo wananchi hawakukubaliana nalo na endapo viongozi waliokuwepo wasingetumia busara kuwapoza ghadhabu wananchi hao basi ingetokea Vurugu ya majini.

Mmoja wa askari Polisi ambaye hakufahamika jina, aliyekuwa wa kwanza kuingia katika tope na maji ya eneo hilo pasipo kujali – alizungumza na wananchi kwa upole akiwataka wavute subira wakiwangoja wengine ambao walitumia muda mrefu tena kufika eneo hilo, kwani iliwalazimu kutafuta eneo kavu la kupita.

Busara za askari zilitawala!!,….Kwani hata wananchi walipotumia lugha za kuudhi askari  walionekana kutojali, na lengo hapo lilikuwa ni kupunguza ghadhabu za wananchi hao ambao walikuwa wakitamka maneno makali kwa hasira za kutelekezewa majukumu hayo ya uokozi wa mwili wa mpendwa wao.

Msemaji  wa kikosi cha polisi kilichotinga eneo la tukio, aliwasihi wananchi, huku akiwaeleza sababu za wao kuchelewa ikiwa ni pamoja na kumfuata daktari wa upimaji, na kuwaomba  wananchi  waache jazba na wafanye kazi kwa ushirikiano… jambo ambalo ndugu wa marehemu na wananchi zaidi ya 200 waliokuwepo katika eneo hilo walilidhia.

Idadi kubwa ya wananchi waliofika katika eneo la tukio hilo, iliwawia vigumu askari polisi kuwapanga katika utaratibu ambao ungefaa, ili  mwili huo ufanyiwe uchunguzi  papo hapo na daktari, na kuwawezesha wananchi kuendelea na taratibu za Mazishi.

Msongamano huo wa watu ulikwamisha mwili huo kufanyiwa uchunguzi, kama ilivyotakikana awali, jambo ambalo msemaji wa kikosi cha polisi aliwaeleza wananchi ugumu wa kufanya uchunguzi eneo hilo, na kisha kuwaomba baadhi ya ndugu wa marehemu waambatane pamoja kuelekea Hospitali ya Rufaa mkoa wa Iringa – ambako huko ndiko daktari angeweza kuifanya kazi yake hiyo kwa ufasaha jambo lililopokewa kwa mikono miwili.

Kwa mujibu wa Noel Mwanilwa- Pacha wa marehemu Azimio Mwanilwa – na David Charles Mwanilwa kaka mkubwa wa marehemu- majira ya saa moja jioni mwili wa marehemu Azimio ulizikwa katika eneo la Tagamenda, ambapo marehemu ameacha mke na watoto sita.

Marehemu Azimio alikuwa ni mfanyabiashara wa Kuku katika Kituo kidogo cha mabasi cha Ipogolo, na hata mauti yake kumfika, inasadikiwa kuwa alikuwa akielekea kununua Kuku katika Wilaya ya Kilolo- Iringa, ambapo watu wasiofahamika walimvamia majira ya saa kumi na moja alfajiri akiwa anakwenda kununua malighafi yake hiyo ya biashara.

MWISHO.