Alhamisi, 19 Machi 2015

ALIYETUMBUKIA MTO RUAHA APATIKANA- POLISI NA ZIMAMOTO LAWAMANI


 Baadhi ya wazamiaji binafsi wakitazama eneo lingine la kutafuta mwili wa Azimio, aliyetumbukia katika mto Ruaha mkuu.
                    Mto Ruaha mkuu.

 Marehemu Azimio enzi za uhai wake.
    Marehemu Azimio- enzi za uhai wake.
 Mwili wa marehemu Azimio ukiwa umeonekana.

 Mwili wa marehemu Azimio ukiwa umeopolewa majini.
 Baadhi ya wananchi wakiwa wameuzunguka mwili.



 Askari Polisi wakiondoka na mwili eneo la tukio kuelekea Hospitali kwa ajili ya uchunguzi.

<<<HABARI>>>

WANANCHI wa Kata ya Ruaha katika eneo la Ipogolo, ndani ya Manispaa ya Iringa - nusura wazue tafrani ya patashika na nguo kuchanika, baada kudai kuchoshwa na uzembe unaofanywa na baadhi ya Polisi.

Wakilalamikia hali hiyo kwa madai ya  kutelekezewa ndani ya maji mwili wa marehemu,  anayedaiwa kuuawa na kisha kutupwa katika mto mkuu Ruaha mkuu, mwili ambao umekaa katika maji kwa muda wa siku tano.

Marehemu aliyefahamika kwa jina la Azimio Mwanilwa ambaye kwa jina alilopewa na wazazi wake aliitwa “Augustino Mwanila”,  kifo kinadaiwa kilitokana na kipigo, kutoka kwa majambazi, ambao walimvamia, alipokuwa njiani akielekea vijijini kununua bidhaa ya biashara yake, tukio lililotokea katika barabara ya Ipogolo – Kilolo Wilayani- katika eneo la Chuo cha maendeleo ya jamii Tagamenda  Manispaa ya Iringa.

Wananchi hao walisema idara ya Polisi inayojihusika na matukio ya majanga na vifo katika kituo cha Polisi kati Iringa, pamoja na kikosi cha zimamoto, wamekuwa wazembe kutekeleza wajibu wao kwa wakati, jambo linalosababisha hasira na hivyo kutokuwepo kwa ushirikiano mzuri.

Akizungumzia hali hiyo kandokando yam to Ruaha mkuu - Rehema Kidava amesema tangu litokee tukio la kuzama majini kijana “Azimio”, hakuna ushirikiano wa aina yoyote kutoka kwa idara hizo za jeshi la Polisi, jambo lililowalazimu wananchi kuhangaikia shughuli za kuutafuta mwili huo majini.

Grace Mgimwa  na Grolia Mbimbi nao wamekinyoshea kidole Kikosi cha zimamoto Iringa, kwa madai ya kutokuwa bega kwa bega nao, katika shughuli hiyo ya uokozi wa mwili wa marehemu,  jambo ambalo limewalazimu wananchi kuacha majukumu yao na kushinda katika eneo hilo la mto Ruaha wakihangaika uuopoaji wa mwili.

Zenaide Nzeukia amesema kumekuwa na tofauti juu ya matukio ya ukamataji na matukio ambayo wananchi wanaomba msaada, hususani yanayohusisha vifo, huku akisema yale ya kukamata wauzaji wa dawa za kulevya, wanywaji wa pombe za jadi “Kienyeji”, na hata wachezaji wa michezo ya kamali – Polisi wamekuwa wakifika kwa muda muafaka, tofauti na matukio yanayotoa usaidizi kwa wananchi.

Yakob Fyimagwa mwenyeviti wa mtaa wa Buguruni – Ipogolo, miongoni mwa mitaa inayozungukwa na mto mkuu wa Ruaha katika eneo la tukio, amesema kinachoudhi ni baadhi ya askari wa vikosi hivyo vya Polisi - kupuuzia majukumu yao, kwa madai kuwa shughuli hiyo ya uokoaji wa mwili uliopo ndani ya maji ni yao Polisi kitengo cha Zimamoto.

Fyimagwa amesema endapo Polisi hao hawatabadili utendaji wao wa kazi, basi kuna hatihati ya kuvunjika kwa ushirikiano baina ya wananchi na jeshi hilo.

“Tunashangazwa kweli na hawa Polisi kuwa mpaka leo hii ni siku ya tano hawajafika katika tukio hili licha ya kuwa taarifa zilitolewa mapema siku ile ile ya tukio, lakini yangekuwa ni matukio yanayohusiana na ukamataji wa waharifu au hata wanywaji wa pombe za jadi huko vilabuni, wangekuja kwa wakati tena wakiwa wengi utadhani wanakwenda vitani, …kwani wanajua baada ya kuwakamata watuhumiwa wananufaika kwa kupewa chochote, lakini hapa siku ya tano hawajafika kama unavyoona tunahangaika tu, na msiba unakuwa mrefu kwa sababu tu ya uzembe wa baadhi ya watu wachache ambao wanalipwa mishahara kwa kazi hii,” Walisema wananchi.

Kwa upande wa wazamiaji binafsi wa majini waliokuwa wakiendelea na shughuli ya uogeleaji kuutafuta mwili wa Marehemu Azimio, wao walidai kuwa kuna umuhimu kwa Jeshi la Polisi kikosi cha Zimamoto na Maokozi - kuona umuhimu wa kuwawezesha vifaa, ili kuifanya kazi hiyo kwa utaalamu na tahadhari.

Fredy Kibasa, Paulo Kitamuka, Saimoni Magubike na Fredy Kilumbi ni miongoni mwa waogeleaji (Waokozi Binafsi) wa majini, wamesema mto Ruaha una wanyama mbalimbali kama Viboko, Mamba na wengine ambao ni hatari kwa usalama wao, lakini hulazimika kuifanya shughuli hiyo ndani ya maji pasipokuwa na kifaa chochote jambo ambalo ni hatari kwao, na lengo likiwa ni kuopoa miili ya watu isiharibike au kupotelea majini.

Naye Ismail Mlenga ( Baba Mwadhani) mlezi wa kikundi hicho cha Uokozi majini, alisema matukio ya majini hayana tofauti na maafa, na hivyo kuna umuhimu kwa taasisi zinazohusika na shughuli hiyo, kwa maana ya Polisi na kikoisi cha zimamoto kufanya kazi zao kwa weredi, kwa madai kuwa kutelekeza mwili wa mtu aliyetumbukia majini ni kuwapa wakati mgumu ndugu wa marehemu na wananchi, kuomboleza kwa muda mrefu wakati wakiendelea kutafuta maiti.

Baba Mwadhani amesema Kikosi cha zimamoto kinapaswa kijitadhmini upya katika utekelezaji wake wa majukumu, huku nao Polisi wakiacha tabia ya kufanyakazi kwa mazoea  na sasa wanapaswa kutekeleza wajibu wao ipasavyo, bila kusubiri kushinikizwa wala kusukumwa.

Kamanda wa kikosi cha Zimamoto mkoa wa Iringa, Keneth Komba alipotafutwa kwa njia ya simu - ili kujua nini kinawakwamisha kufanya kazi hiyo ya uokozi iliyopo ndani ya idara yao, alisema yupo safarini kuelekea mkoani Ruvuma- ambako amepata taarifa ya mzazi wake kuugua, huku akiahidi kulishughulikia jambo hilo, kwa kuiagiza ofisi yake ifike katika eneo hilo.

Siku ya tano mwili ukiwa ndani ya maji ya mto mkuu Ruaha- majira ya saa sita na dk 35 kikosi binafsi cha wazamiaji majini, kilifanikiwa kuuona mwili huo wa kijana Azimio, ambapo viongozi wa mitaa iliyopo eneo hilo la Ipogolo kwa njia ya Simu walitoa taarifa kituo cha polisi juu ya kupatikana kwa mwili huo, kama ni moja ya taratibu ya vifo vya aina hiyo.

lengo la utaratibu huo ni kutambua sababu za kifo na kisha wananchi kupata ridhaa kutoka kwa polisi, kuzika mwili na hiyo huwa ni mara baada ya Daktari kupima… – lakini hali ilikuwa tofauti, baada ya polisi tena  kudaiwa kuchelewa kufika katika tukio hilo, kwa takribani saa tatu, huku mwili huo ukiwa juani ukieendelea kubadili muonekano wake wa awali, jambo lililozua hasira kwa wananchi.

Mara baada ya askari Polisi kuwasili eneo hilo, kilizuka kituo kingine, kwani wananchi waliwataka polisi hao  wafike eneo la tukio – jambo ambalo baadhi ya askari walisema wanashindwa kulifikia eneo lililokuwa limewekwa mwili huo, kwa kile walichodai kuwa kuna maji na tope na hivyo kuwawia vigumu kupita katika mazingira hayo.

Tope hilo lililowakwamisha baadhi ya askari ni lile linalotokana na mto Ruaha mkuu kuchepusha maji yake mara baada ya mvua kunyesha, suala ambalo wananchi hawakukubaliana nalo na endapo viongozi waliokuwepo wasingetumia busara kuwapoza ghadhabu wananchi hao basi ingetokea Vurugu ya majini.

Mmoja wa askari Polisi ambaye hakufahamika jina, aliyekuwa wa kwanza kuingia katika tope na maji ya eneo hilo pasipo kujali – alizungumza na wananchi kwa upole akiwataka wavute subira wakiwangoja wengine ambao walitumia muda mrefu tena kufika eneo hilo, kwani iliwalazimu kutafuta eneo kavu la kupita.

Busara za askari zilitawala!!,….Kwani hata wananchi walipotumia lugha za kuudhi askari  walionekana kutojali, na lengo hapo lilikuwa ni kupunguza ghadhabu za wananchi hao ambao walikuwa wakitamka maneno makali kwa hasira za kutelekezewa majukumu hayo ya uokozi wa mwili wa mpendwa wao.

Msemaji  wa kikosi cha polisi kilichotinga eneo la tukio, aliwasihi wananchi, huku akiwaeleza sababu za wao kuchelewa ikiwa ni pamoja na kumfuata daktari wa upimaji, na kuwaomba  wananchi  waache jazba na wafanye kazi kwa ushirikiano… jambo ambalo ndugu wa marehemu na wananchi zaidi ya 200 waliokuwepo katika eneo hilo walilidhia.

Idadi kubwa ya wananchi waliofika katika eneo la tukio hilo, iliwawia vigumu askari polisi kuwapanga katika utaratibu ambao ungefaa, ili  mwili huo ufanyiwe uchunguzi  papo hapo na daktari, na kuwawezesha wananchi kuendelea na taratibu za Mazishi.

Msongamano huo wa watu ulikwamisha mwili huo kufanyiwa uchunguzi, kama ilivyotakikana awali, jambo ambalo msemaji wa kikosi cha polisi aliwaeleza wananchi ugumu wa kufanya uchunguzi eneo hilo, na kisha kuwaomba baadhi ya ndugu wa marehemu waambatane pamoja kuelekea Hospitali ya Rufaa mkoa wa Iringa – ambako huko ndiko daktari angeweza kuifanya kazi yake hiyo kwa ufasaha jambo lililopokewa kwa mikono miwili.

Kwa mujibu wa Noel Mwanilwa- Pacha wa marehemu Azimio Mwanilwa – na David Charles Mwanilwa kaka mkubwa wa marehemu- majira ya saa moja jioni mwili wa marehemu Azimio ulizikwa katika eneo la Tagamenda, ambapo marehemu ameacha mke na watoto sita.

Marehemu Azimio alikuwa ni mfanyabiashara wa Kuku katika Kituo kidogo cha mabasi cha Ipogolo, na hata mauti yake kumfika, inasadikiwa kuwa alikuwa akielekea kununua Kuku katika Wilaya ya Kilolo- Iringa, ambapo watu wasiofahamika walimvamia majira ya saa kumi na moja alfajiri akiwa anakwenda kununua malighafi yake hiyo ya biashara.

MWISHO.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni