Jumanne, 18 Februari 2014

CCM, CHADEMA NA CHAUSTA KUWANIA JIMBO LA KALENGA


 Wafuasi na wanachama wa CHADEMA wakisindikiza msafara wa mgombea wao kurudisha fomu ya ushiriki wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Kalenga.
              Wafuasi wa CHADEMA
Bw. Godfrey W. Mgimwa mgombea wa CCM akirudisha fomu kwa msimamizi wa uchaguzi jimbo la kalenga Bi. Pudensiana Kisaka.

Wafuasi na wanachama wa CCM wakimsindikiza mgombea wao kurudisha fomu ya kushiriki mchakato wa kampeni za kiti cha ubunge jimbo la Kalenga.

<<<<<<<<<<<<HABARI>>>>>>>>>>>

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na Chama Cha Mapinduzi CCM leo wamefanikiwa kurudisha fomu za kushiriki kugombea nafasi ya kiti cha Ubunge wqa jimbo la Kalenga mkoani Iringa, nafasi iliyoachwa wazi baada ya aliyekuwa mbunge wake, Dk William Mgima ambaye pia alikuwa Waziri wa fedha kupoteza maisha januari 1, mwaka huu nchini Afrika Kusini wakati akipatiwa matibabu.


CHADEMA, CCM  na CHAUSTA wamerudisha fomu hizo leo ikiwa ni siku ya mwisho ya kurejesha fomu, fomu ambazo zitawapa nafasi ya  kugombea nafasi hiyo, huku wagombea wa vyama vya NCCR-Mageuzi na Chausta wakiwa ndiyo wamechukua fomu hizo siku ii ya mwisho.

CCM ambayo ilikuwa ya kwanza kurudisha fomu za mgombea wake majira ya saa tano asubuhi na kufuatiwa na Chadema waliorejesha fomu zao majira ya saa saba mchana, kupitia wagombea wao Godfrey Mgimwa (CCM), Grace Tendega  (CHADEMA na Richard Minja wa CHAUSTA

Wagombea wa vyama vyote viwili walisindikizwa na maandamano ya wafuasi na wanachama wao na kufanya shamrashamra ziwavutie wananchi wengi mjini Iringa.

Akiwa na wafuasi zaidi ya 500, mgombea wa CCM, Godfrey Mgimwa aliyetokea ofisi za CCM Iringa Vijijini zilizopo mjini Iringa, alisindikizwa hadi kwa msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na baada ya domu zake kupokelewa aliendelea na maandamano yaliyoishi ofisi kuu za CCM Mkoa wa Iringa.

Grace Tendega aliletwa katika ofisi za msimamizi huyo wa Uchaguzi jimbo la Kalenga akiwa na msafara wa pikipiki 20 na magari 5, huku mgombea wa CCM pamoja na wafuasi na wanachama wake wakitembea kwa miguu hadi katika ofisi ya CCM Mkoa wa Iringa.


Katika nasaha zao kwa wapiga kura wa jimbo hilo, wagombea hao wamewataka wafuasi wao kufanya kampeni za amani na kuepuka lugha au matendo yanayoweza kuhatarisha amani na ustaarabu.

Akizungumzia kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya hivikaribuni inayowataka wana CCM kuacha unyonge, Mgimwa alisema haikuwa na maana kwamba wana CCM hawawezi kupambana na wapinzani wao.

“Kauli ile ilikuwa na maana tuwafundishe wenzetu ustaarabu ili waache siasa za vurugu na machafuko,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa, Delphina  Mtavilalo alisema hawawezi kutumia silaha kupambana na wapinzani wao, watatumia maneno kupambana nao.

“Tulipata uhuru bila kumwaga damu; tunatoa onyo kwa vijana wetu wakiona kuna mapambano yanayohatarisha maisha yao watoe taarifa kwenye vyomo vya dola, kwa kufanya hivyo watakuwa wanaondoa uonnyonge wao,” alisema.

Naye Mgombea wa Chadema, Tendega aliwataka wafuasi wa chama hicho kuondokana na dhana waliyonayo ya baadhi ya watu kuona kwamba wao ni watu wa fujo, na akiwataka sasa  kufanya kampeni za kistaarabu.

“Nawaomba wana Kalenga na wana Chadema kwa ujumla, tufanye kampeni za amani katika kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini,” alisema.

Kampeni za uchaguzi huo mdogo zitaanza kesho Februari 19 na kuhitimishwa Machi 15, ambapo tarehe 16 mwezi huo wa tatu ndiyo utafanyika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo la kalenga.

Hata hivyo …majira ya saa kumi na moja mtandao huu ulifanya mawasiliano na msimamizi wa uchaguzi Bi. Pudensiana Kisaka kujua kama vyama vya NCCR na CHAUSTA kama vimefanikiwa kurejesha fomu zao na majibu yalikuwa ni “Chama cha NCCR kimechelewa kurudidisha fomu na licha ya hivyo bado baadhi ya masharti kilikuwa bado hakijakidhi, kwa hiyo nimewaondoa kwenye ushiriki wa kugombea kiti cha Ubunge jimbo la kalenga na CHAUSTA wao wamefanikiwa kukidhi vigezo, kwa hiyo vyama vitakavyoshiriki uchaguzi huo mdogo ni CHADEMA, CCM na CHAUSTA”, alisema Pudensiana Kisaka.

MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni