Jumatano, 14 Mei 2014

MADIWANI MUFINDI WAIBANA TANROAD


  Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi wakiwa katika kikao hicho.
  Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi wakiwa katika kikao hicho.
 Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi wakiwa katika kikao hicho.

 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bw. Willium Ntinika akiwa katika kikao cha baraza la madiwani wilayani Mufindi, akisikiliza jambo kwa umakini mkubwa.


 Diwani Efrehem Lukunga akisikiliza jambo kwa umakini katika baraza hilo.



Wa kwanza kulia ni diwani Ernei Nyeho wa Kata ya Mdabulo, akiwa na diwani Tasil Mgoda wa kata ya Sao hill Mufindi, wakijadili jambo, baada ya kutoka katika baraza la madiwani.


 Moja ya alama ya "X" ambayo huwekwa na TANROAD kama ni  irani ya kuondolewa jengo eneo lenye alama hiyo, alama ambazo zimelalamikiwa na baraza la madiwani Mufindi.

<<<HABARI>>>
BARAZA la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, limeilalamikia  Wakala wa barabara mkoa wa Iringa TANROAD kwa madai ya kushindwa  kujenga barabara kwa kiwango kinachotakiwa,  na hivyo miundombinu hiyo kulazimika kutengenezwa mara kwa mara.

Madiwani hao wamesema ujenzi wa barabara chini ya kiwango, unaofanywa na TANROAD kamwe hauwezi kufumbiwa macho, huku wakiitaka mamlaka hiyo kuwashirikisha wataalamu wa Wilaya husika katika jenzi zake, tofauti na ilivyo sasa ambapo wamedai TANROAD inafanya mambo yake pasipo kutaka ushauri wa wahandisi wenyeji.
 
Ernei Nyeho- Diwani Kata ya Mdabulo amesema barabara nyingi zinazojengwa na TANROAD zimekuwa chini ya kiwango kinachotakiwa, licha ya kuwa serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi tofauti naza Halmashauri, ambazo barabara zao licha ya kupatiwa kiwango kidogo cha fedha, lakini zimekuwa ni imara na bora.

“Ukiangalia barabara zetu za Halmashauri ambazo tunapatiwa fedha kidogo katika kuzijenga na znuri sana tofauti kabisa na hizi za TANROAD, sasa mwenyekiti tunakuomba utufikishie ujumbe kuwa hao TANROAD tunawataka wanapokuja Wilayani kujenga barabara wawahusishe wataalamu wetu wahandisi wa Halmashauri, hii itasaidia kupewa ushauri kwa maana ya vifusi,” Alisema Nyeho.


Tasil Mgoda – diwani Kata ya saohill amesema ipo haja kwa serikali kuwa imara kuhakikisha TANROAD inatengeneza barabara kwa kiwango kinachotakiwa, huku akitolea mfano wa barabara ya Kinyanambo kwenda Kibengu kuwa imechakaa na haina hadhi ya kuwa imetengenezwa na TANROAD.


Edna  Mwikola- Diwani V/maalumu tarafa ya Ifwagi, amesema hata alama za  “X”  zilizowekwa katika nyumba za watu kwa zaidi ya miaka 3  hazionyeshi dalili zozote za ujenzi wa barabara kuanza,  licha ya uwekaji wa alama hizo za  “X” kwenye nyumba za wananchi  kusababisha madhara makubwa.

“Baadhi ya wananchi wamepoteza maisha, wamekufa baada ya nyumba zao kuwekewa alama za “X”, hii inaumiza sana kwani barabara hizo mpaka leo hazina dalili zozote za kujengwa, tunaiomba serikali itemize ahadi zake za kuzijenga barabara hizo ambazo zimewekewa “X”   kwani mpango huo umeleta madhara makubwa kwa jamii”, Alesema Mwikola.

Naye mwenyekiti wa halmashauri hiyo ya Wilaya ya Mufindi Peter Tweve amesema ushirikishwaji wa masuala ya ujenzi wa miundombinu ya barabara utasaidia kutatua changamoto iliyopo, kwani wataalamu kutoka TANROAD wakati mwingine wamekuwa wakitumia Maram na vifusi visivyofaa kutokana na kutokuwa na wataalamu wenyeji.

"Hapa kinachotakiwa ni uwepo wa ushirikishwaji na ushirikiano, hii itasaidia kupunguza na hata kumaliza tatizo hili, mfano kuna wakati unakuta wataalamu wa TANROAD wanatumia Maramu na vifusi ambavyo haviendani na udongo wa eneo wanalotengeneza barabara, lakini kama wakiwashirikisha wataalamu wetu wa halmashauri wataepukana na hali hiyo," Alisema Tweve.

Meneja wa TANROAD mkoa wa Iringa Injinia Paul Ryakurwa, akizungumzia mpango wa uwekaji wa alama za “X” amesema hatua hiyo inasaisia kuwatahadharisha wananchi wasifanye maendelezo yoyote katika hifadhi za barabara na kuwa mpango wa ujenzi wa barabara hizo upo lakini umekwamishwa na uhaba wa fedha.

MWISHO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni