Jumamosi, 17 Mei 2014

UKAWA YAWEKEWA KIZINGITI MAFINGA- YAPOKEWA KWA MABANGO.


  Wananchi waliofika na mabango yenye ujumbe mbalimbali, katika uwanja wa Mashujaa, katika mkutano wa hadhara wa UKAWA- Mafinga mjini- katika Wilaya ya Mufindi- Iringa.
 Baadhi ya vijana wakiwa katika uwanja wa Mashujaa mjini Mafinga, katika mkutano wa hadhara wa UKAWA, Wilayani Mufindi Iringa.
  Moja ya bango likiwa limeshikwa na mwananchi ambaye hakufahamika jina lake, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mashujaa mjini Mafinga- Wilaya ya Mufindi Iringa.
  Wananchi waliofika na mabango yenye ujumbe katika uwanja wa Mashujaa, katika mkutano wa hadhara wa UKAWA.
 Wananchi waliofika na mabango yenye ujumbe katika uwanja wa Mashujaa, katika mkutano wa hadhara wa UKAWA.
 Shekh Rajab Katimba- Mw/kiti wa jumuiya ya maimam Tanzania, akizungumza na wananchi katika uwanja wa Mashujaa Mafinga mjini- katika Wilaya ya Mufindi - Iringa.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Taifa Martine Juju Danda, akizungumza na wananchi katika uwanja wa Mashujaa wa mjini Mafinga- Mufindi Iringa.
 Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa mashujaa Mafinga, wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.


<<<HABARI>>>

UMOJA wa katiba ya wananchi wanaopigania rasimu mpya -UKAWA, ambao viongozi wake wanafanya ziara ya mikutano katika maeneo mbalimbali nchini,  umekutaka na kikwazo kikubwa katika moja ya mikutano yake mkoani Iringa.

Viongozi wa UKAWA wakiongozwa na mwenyekiti wa CUF Ibrahim Lipumba, wamejikuta katika sintofahamu, baada ya baadhi ya wananchi kutinga katika mkutano huo, huku wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali ambazo zipo kinyume na Mkutano huo.

Mkutano huo ambao umefanyika katika uwanja wa Mashujaa wa mjini Mafinga- wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, umekutana na zengwe baada ya kundi la wananchi kuwasili na mabango yenye ujumbe mbalimbali.

Mabango hayo ndani ya Uwanja huo yameleta sintofahamu, baada ya viongozi na wafuasi wa UKAWA waliofika katika uwanja huo kusikiliza viongozi, jambo ambalo limemfanya katibu wa CHADEMA Mkoa wa Iringa Allen Kilewela kuitaka hadhara hiyo kuimba wimbo wa Taifa, ili kutuliza vurugu hizo.

Aidha Killewela aliliomba jeshi la polisi kuingilia kati tatizo hilo, ambalo lilikuwa linatishia usalama wa wananchi waliofika katika mkutano huo, kwani aadhi yao ambao hawakuridhika na mabango hayo walijikuta wakirushiana maneno makali huku baadhi yao wakishikana mashati na kupigana.

“Jamani huu mkutano ni halali, polisi wako wapi?? Naona kuna vijana wamekuja hapa kwa nia ya kuvuruga mkutano huu, tunawaomba polisi waingilie kati suala hilo, wananchi waliokuja hapa wawe ni wale ambao wamekuja kuwasikiliza viongozi na si vinginevyo,” Alisema.

Hatua hiyo ilimfanya kaimu mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Taifa Martine Juju Danda kupanda jukwaani na kutoa onyo juu ya wale wanaofanya vurugu katika mkutano huo.

“Nataka niwaambie ndugu zangu!!, Usije ukapima uimara wa ukuta kwa kupiga ngumu, Utaumia, tunawatumia salamu wale waliowatuma, kwamba zoezi lenu halitafanikiwa, na kama mnataka muondoke salama kama mlivyotoka majumbani kwenu tunawaomba msikilize tutaelewana, kwani huu ni mkutano wa wananchi wanaotaka kujua nchi yao ipo wapi na inaelekea wapi,” Alisema Danda.

Naye Shekh Rajab Katimba- Mw/kiti wa jumuiya ya maimam Tanzania, amesema katika mkutano huo hawahitaji vurugu, bali wanatoa elimu juu ya umuhimu wa serikali tatu, ambazo zitaondoa kero za Muungano.

Aidha Shekh Katimba alisema katika kuijadili Katiba, upo umuhimu wa siasa zikabaki katika mustakabari wake, kuliko baadhi ya viongozi kuchanganya masuala ya siasa na dini, huku akiwataka viongozi hao kuacha vitisho kwa wananchi na waumini katika madhabahu matakatifu.

Katimba amesema katika mchakato wa katiba, wananchi wenyewe ndiyo wanahaki ya kuamua wanataka Katiba ipi, na kuwa wananchi hawataki ufisadi, na wao ndiyo wanakataa hali hiyo ya kujilimbikizia mali watu wachache.

“Sisi tunaukataa ufisadi, kwani nchi hii siyo maskini bali ni tajiri sana, na utajiri huu tunataka wanaofaidi wawe ni wananchi wote wa Tamzania na siyo watu wachache kama ilivyo, na ili kumaliza tatizo hili tuikubali serikali tatu ili kupunguza hata idadi kubwa ya baraza la mawaziri,” alisema.

Aidha Shekh Katimba amesema nchi ina rasilimali nyingi kama maji ya kila aina, kama Bahari, mito, maziwa, madini ya almasi, Tanzanite pamoja na Gesi ambayo ni utajiri mkubwa, huku akisema nchi ya Tanzania ni mali ya kila mmoja, mwenye dini, asiye na dini, wasio na vyama na wenye vyama na hata masikini.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na vijana hao yalikuwa na ujumbe uliosomeka “vijana Mafinga tuna mashaka na ndoa ya Ukawa, watauza nchi” na bango la waendesha bodaboda lilisomeka “ Rudisheni posho kwanza mjengoni dodoma.”

Mengine na ujumbe wake kwenye mabano ni lililowatambulisha wafanabiashara wa sokoni lililosomeka “Mafinga Sokoni, serikali tatu sio suluhisho la matatizo ya wananchi”, na la wapiga debe Mafinga stendi lilisomeka “Karume Oyee, Nyerere Oyee, Muungano Saafi.”

Bango la waliojitambulisha kuwa ni machinga lilisomeka “tunataka serikali inayojali wajasiliamali, sio kujali matumbo yao”, na lile la wakulima lilisomeka “kilimo kwanza, utaifa kwanza.”

Wakati mabango hayo yakizungushwa katika mkutano huo muda ambao Profesa Lipumba akihutubia, usikivu ulipotea kwa zaidi ya dakika 20 baada ya sehemu ya kundi la vijana lililokuwa likimsikiliza kuelekea upande waliokuwa vijana wenye mabango hayo.

Mmoja wa Polisi aliyekuwa akiwatuliza vijana hao alisema “Jamani huu ni mkutano halali wa kisiasa, acheni wenzenu wafanye mkutano wao, yatoeni mabango yenu.”

Akielezea vurugu hizo, Profesa Ibrahim Lipumba amesema zinafanywa na vijana waliotumwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwasababu ya msimamo wao wa kutaka serikali mbili, tuhuma zilizokanushwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu aliyehojiwa baaada ya mkutano huo.

“Siamini kama mkutano huu ungekuwa unahutubiwa na Mwenyekiti wa CCM wa Taifa Jakaya Kikwete wangekuja na mabango hayo na kufanya vurugu hizi?”  

Hata hivyo baada ya vurugu hizo kutulia, Profesa Lipumba aliruhusu maswali huku akifafanua sababu mbalimbali zilizosababisha wasusie bunge la Katiba na kuanzisha UKAWA.

Profesa Lipumba alisema milango ya Ukawa ipo wazi kwa mtu yoyote ndani na nje ya bunge la Katiba, wakiwemo wabunge na viongozi wa CCM, “Tutafurahi kuwapata wana CCM, tunawakaribisha Ukawa ili kwa pamoja tushirikiane kupata Katiba inayotokana na wananchi,” alisema.

Winfreda Ngoti mwananchi aliyepata fulsa ya kuuliza swali, aliyesema harakati za kudai serikali tatu hazitakuwa na maana yoyote endapo matatizo ya wananchi hayatashughulikiwa.

“Watanzania wana matatizo lukuki, vituo vya huduma za afya havina wataalamu, dawa, wakulima hawapati pembejeo kwa wakati na bei zake ni kubwa, wafanyabishara wadogo wanabanwa na kukamuliwa kodi, walimu hawapati mishahara kwa wakati, askari wana mishahara midogo na wanakula rushwa,” alifafanua.

Katika majibu yake, Profesa Lipumba amesema hayoyote yatafanyiwa kazi kukiwa na Katiba bora itakayosisitiza uwajibikaji na uadilifu.

Alisema rushwa na ufisadi vimekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya Taifa, katika sekta zote ikiwemo elimu, afya, kilimo, biashara, miundombinu na sekta nyingine.
MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni