Jumapili, 27 Aprili 2014

ATANGAZA KUUZA FIGO AJIKWAMUE KIUCHUMI


 Ramadhani Mrisho almaarufu MAKOSA, mtu maarufu mkoani Iringa, ambaye sasa ametangaza rasmi kuuza Figo yake ili kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi.
  MAKOSA akiwa katika pozi.


JINA Makosa si geni masikioni mwa wakazi wa mji wa Iringa na mikoa ya nyanda za juu kusini na hata kwingineko, Makosa ni mkazi wa Manispaa ya Iringa, licha ya kufanya kazi zake mbali mbali siku za nyuma.

Makosa jina lake halisi ni “Ramadhani Mrisho” aliwahi kuwa tajiri wa kusifiwa njini Iringa, kwa kumiliki baadhi ya majumba, magari, kituo cha Luninga IMTV, ukumbi wa IDYDC awali Cat’s  iliyo mkabala na maktaba ya mkoa wa Iringa huku akiwa na Zahanati iliyojibebea umaarufu mkubwa mjini Iringa iliyoitwa kwa jina lake “MAKOSA DISPENSARY”.

Makosa aliweza kuwa na utajiri huo baada ya kustaafu kazi yake ya Ubaharia mwanzoni mwa miaka ya tisini, na pia amewahi kujitolea kupanda miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya matunda Manispaa nzima ya Iringa, miti ambayo kwa sasa ni urembo unaounakshi Mji wa Iringa, kwa kuwa na ukijani wa kuvutia katika kila nyumba ambazo ziliuendeleza utamaduni wake wa kupenda mazingira.

Wakati akifika mjini Iringa, MAKOSA akiwa na itikadi za watu wanaosuka nywele ndefu (rasta), alikuwa si mnywaji wa pombe, mnyenyekevu na alijikita katika kuisaidia jamii ya watu wa Iringa kuhifadhi mazingira likiwempo hilo la kupanda miti, ya aina mbalimbali inayoupendezesha mji.

Licha ya kufanya kazi hizo na hata kuisaidia serikali juu ya uhifadhi ya mazingira, historia ya MAKOSA kwa baadhi ya watu sasa ni kama vile imesahaulika kwasababu hakuna anayemuenzi kwa kazi kubwa hiyo aliyoifanya.

Sijui ndiyo yale yale ya kutaka kumsifu na kumuenzi baada ya kupoteza uhai wake, lakini ingekuwa vyema watu wa aina hii wakapewa sifa zao na hata kuendelea kutumia mawazo yao ili kuwavutia na wengine kufanya hayo ambayo ni mfano bora katika jamii.

Pamoja na harakati hizo MAKOSA ndio mtu wa kwanza mjini Iringa kuingiza mabasi madogo ya kusafirisha abiria aina ya Coaster yaliyokuwa yakifanya kazi katika maeneo mbalimbali ya mjini Iringa hasa Iringa, Ilula na Ruaha mbuyuni.

Licha ya kuwa mtu huyu MAKOSA amefanya mengi na makubwa lakini hakumbukwi, leo hii natumia pia safu hii japo kumpa sifa zake, bila kusubiri desturi ya kumsifia mtu mpaka anapopoteza uhai wake.

"Makosa ni mtu mcheshi, asiye na makuu, mchangamfu, anayejua kumzoea mtu hata asiyemfahamu, hana ubaguzi kwake kila mmoja ni rafiki, awe kijana au mzee, asiye na aibu kueleza shida yake, hahofii kuchekwa anapotaka kujifunza kitu, muwazi na mkweli".

Miezi kadhaa iliyopita Makosa alitangaza kujinyonga katika uwanja wa hayati samora Masheli uwanja wa mjini Iringa, huku akitangaza ,kiingilia kuwa watoto ni sh. 500 nawa kubwa sh. 100 fedha ambazo zingeweza kusaidia kununua Madawati ili mji shule za Iringa ziepukane na uhaba wa madawati unaosababisha wanafunzi wake kukaa Sakafuni, huku baadhi yao wakitumia njia mbadala ya kukalia madawati yaliyotengenezwa kwa  Udongo na Nyasi.

Leo hii Makosa amekuja na kali mpya ya mwaka ya kutangaza kuuza moja kati ya FIGO zake.

“Hali yangu kiuchumi sio nzuri nalazimika kuuza moja kati ya figo zangu ili nipate fedha itakayonisaidia kuendesha maisha,” alisema wakati akizungumza na mtandao huu.

MAKOSA ambaye hivikaribuni amejipachika jina lingine akijiita MOBUTU SESESEKO amesema amefanya maamuzi hayo akiwa na akili timamu na akaomba watakaopata taarifa hii wasimzanie akili yake imekuwa tofauti.

“Nina akili timamu, nimeamua kuchukua uamuzi huu kama nilivyosema kwa lengo la kujikwamua kiuchumi,” alisema bila kufafanua bei ya FIGO yake kama atapata mteja.

Amesema: “Najua wapo watu wenye matatizo ya FIGO na wamekuwa wakisafiri mbali na nchi kutafuta,kama kuna yoyote amekosa au yupo nchini na anahitaji basi aje ili tukubaliane bei.

Katika dhana ile ile ya kupata fedha zitakazosaidia kuendesha familia yake, Julai 2012 MAKOSA alitangaza kujinyonga katika tukio alilopanga lifanyike ndani ya uwanja wa Samora kwa sharti la mashuhuda wake kulipa kiingilio ambacho kingekusanywa na familia yake.

MAKOSA alinukuliwa wakati huo akisema kuliko familia yake kuendelea kutaabika ni bora ajitoe muhanga ili zikusanywe fedha zitakazosaidia kuinusuru familia yake na kiasi kingine kusaidia watoto yatima.

“Mpango wangu huo haukuzaa matunda, nikiwa katika maandalizi watu mbalimbali wakiwemo Polisi walijitokeza na kunipatia ushauri nasaha jambo lililosababisha nisitishe uamuzi wa kujingonga,” alisema.

Sasa nimekuja na mpango mpya, mpango huu si mwingine zaidi ya huu wa kuuza FIGO yangu moja, naamini nikifanikiwa nitapata fedha”, amesema.

Taarifa kutoka kwake mwenyewe biashara zote hizo haziko tena mikononi mwake na ugumu wa maisha unazidi kumuandama, na kuwa sasa anatafuta kujikwamua na njia halali anayoiona mbele yake ambayo ni kuuza FIGO yake moja.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni