Jumapili, 27 Aprili 2014

UMBALI WAWAKOSESHA HUDUMA ZA FYA


Dr. Retisia Warioba  kaimu mkuu wa Mkoa wa Iringa, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa akiwahutubia wananchi wa Ulata, juu ya umuhimu wa chanjo kwa watoto.
 Dr. warioba akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ulata, kilichopo Kata ya Wasa Iringa vijijini.
 Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ulata, waliofika na watoto wao kupatiwa huduma ya chanjo wakimsikiliza Dr. Warioba, aliyezindua rasmi shughuli za chanjo mkoa wa Iringa.
 Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, wakijitambulisha kwa wananchi wa kijiji cha Ulata, ambako maadhimisho ya siku wiki ya chanjo yamefanyika huku kimkoa.
 Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ulata wakisikiliza jambo kutoka kwa Dr. Warioba katika uzinduzi wa wiki ya chanjo.
Watatu kulia ni mganga mkuu wa Wilaya ya iringa- Dr. Ignus Mlowe akiwa na watumizshi wenzake wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, katika kijiji cha Ulata siku ya chanjo ambayo kimkoa ilifanyika katika kijiji cha Ulata Kata ya Wasa.

<<<<HABARI>>>>
WANANCHI wa kijiji cha Ulata na Ngonamwasi  vilivyopo Kata ya Wasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wanakabiliwa na changamoto kuwa ya upatikanaji wa huduma ya fya, kwa kulazimika kutembea umbali wa zaidi ya km 30.

Wananchi hao wanalazimika kutembea umbali wa km 32 kuifikia huduma ya afya katika Zahanati ya Wasa, jambo linalowafanya akinamama wajawazito na wagonjwa kushindwa kupata huduma hiyo muhimu.

Licha ya umbali, pia upatikanaji wa usafiri ni mgumu, huku miundombinu ya barabara ikiwa si rafiki kwa maendeleo na usalama wa wananchi, kwani baadhi ya maeneo ya barabara yamebomoka na hivyo wananchi kuwa ndiyo wenye jukumu la kuyafanyia ukarabati.

Wananchi hao wameyazungumza hayo katika uzinduzi wa zoezi la chanjo, lililofanyika katika kijiji cha Ulata, zoezi lililozinduliwa na kaimu mkuu wa Wilaya ya Iringa Dr. Retisia Warioba ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Iringa.

“Hapa unaona tumekuja watu wachache, siyo kama hawataki, wanakwepa kutembea mwendo mrefu ,  kilomita 16 kwenda na kurudi ni km 32, sasa unakuta wale wasio na uwezo wa kutembea hawawezi, na hiyo ndiyo inasababisha wengine kudiriki kutumia hata dawa za kienyeji kwa sababu kwenda Wasa na kurudi hizo mk 32 hawezi,” Walisema.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Ulata Stanley Mgao amesema changamoto kubwa inayowakabiri ni uhaba wa zahanati, huku akiiomba serikali kukiangalia kwa jicho la huruma kijiji hicho, kwa kuwa wananchi wake wanapata shida.

Akizungumzia hali hiyo, diwani wa Kata ya Wasa Masumbuko Choga amesema ni kweli wananchi wa kijiji cha Ulata na Ngonamwasi hutembea kilomita 32 kuifuata huduma ya afya, huku baadhi yao wakipoteza maisha kwa kuimosa huduma hiyo muhimu.

“ Kata yangu inavijiji saba, na katika vijiji hivyo saba kuna Zahanati tatu tu, Wasa, Ihomasa na Usengerindete, na kutoka Ulata hadi Wasa ni mwendo wa km 32 kwenda na kurudi, sasa inakuwa ni tatizo kwa akinamama wajawazito na wazee na hata wagonjwa, kwani hata miundombinu ya barabara zetu ni changamoto kubwa ambazo zinakwamisha hata uwepo wa usafiri,” Alisema Choga.

Aidha amesema kumekuwa na matukio ya vifo vya wagonjwa majumbani na hata njiani wakati wakifuata huduma na matibabu na kutokana na hilo jitihada za wananchi tayari wamefyatua tofari kwa ajili ya kujenga zahanati katika kijiji cha Ikungwe jingo lipo hatua ya kupauliwa na  katika kijiji cha Ufyambe mvua zikimalizika wataanza ujenzi.

Amesema ili kukabiliana na changamoto ya vifo, wamekuwa wakiwahamasisha wananchi kuwafikisha wagonjwa na wahitaji wa huduma ya fya mapema katika Zahanati na vituo vya afya, kwa lengo la kuepukana na vifo vitokanavyo na ukosefu wa matibabu.

Choga ameiomba serikali kutenga fungu la fedha za kutosha upande wa sekta ya afya, ili kufanikisha mpango wa ujenzi wa Zahanati kila kijiji, ili kuwawezesha wananchi kuipata huduma ya afya mapema.

Mganga mkuu wa Wilaya ya Iringa Dr. Ignus Mlowe amesema changamoto ya umbali na miundombinu ya barabara, na kuwa tayari wananchi kwa kutumiua nguvu zao wameanza ujenzi wa zahanati ili kujikwamua na adha hiyo.

Dr. Mlowe amesema Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ina Hospitali moja pekee Teule ya Tosamaganga,  Zahanati zikiwa 63 na kuwa Vituo vya afya ni 10, na kuwa mpango mkakati wa Wilaya kufikia 2015/ 2016  ni kuwa na Vituo vya afya 14 huku kila kijiji kikiwa na Zahanati.

Mratibu wa chanjo mkoa wa Iringa Naftari Mwalongo akisoma taarifa ya chanjo mbele ya kaimu mkuu wa Mkoa wa Iringa ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Iringa Dr. Retisia warioba amesema- Changamoto inayowakabiri katika utoaji wa huduma ya chanjo ni baadhi ya halmashauri kutokufikia kiwango cha uchanjaji kwa asilimia 95 kiwango cha kitaifa.

Mwalongo amesema changamoto nyingine ni huduma ya mkoba kutokufanyika kikamilifu,  hasa katika vijiji na vitongoji kwenye baadhi ya Halmashauri, huku tatizo la upungufu wa watumishi waliopata mafunzo na ujunzi wa kutoa chanjo kwenye vituo wakiwa hawaendani na ongezeko la chanjo nchini.

Amesema kuna upungufu wa majokofu na vifaa vingine  kwa ajili ya kuhifadhia chanjo kwa baadhi ya Zahanati, uhaba wa vyombo vya usafiri kwa ajili ya huduma ya Mkoba “Out reach Services”.

Pia amesema kuna wanakabiliwa na upungufu wa nishati ya Gesi kwa ajili ya majokofu ya Chanjo, huku baadhi ya vituo kutokufikika hasa wakati wa masika, na hivyo baadhi ya watoto kutokufikiwa na huduma hiyo muhimu ya chanjo.

Hata hivyo Mwalongo amesema pamoja na changamoto hizo mkoa umeweza kufanya jitihada za kuimarisha huduma na ulinzi elekezi katika Halmashauri na vituo vya kutolea huduma, kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya chanjo katika mpango kabambe wa huduma za afya kwa halmashauri.

Na kuwa mkoa umezishauri Halmashauri kutenga fedha kwenye bajeti zao kwa ajili ya kununua majokofu pamoja na nishati ya Gesi na kuajiri watumishi wenye elimu na ujuzi wa kutosha.
MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni