Jumapili, 27 Aprili 2014

LILILOMSHTUA WAZIRI MWANRY LAWAWEKA NJIAPANDA MADIWANI


 Jengo la idara ya ujenzi wilaya ya kilolo, ambalo watumishi wake wametiliwa mashaka juu ya utendaji wao wa kazi.


 Jengo la halmashauti ya Wilaya ya Kilolo- Mkoani Iringa

<<<<HABARI>>>>

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo limemuagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo kufuatilia ofisi ya mhandisi wa halmashauri hiyo na wakandarasi juu ya watumishi wanaopewa kazi.

Madiwani hao wameonesha hofu ya kuwepo kwa rushwa katika idara hiyo ya  ujenzi hasa kutokana na kandarasi nyingi kujengwa chini ya kiwango, na hivyo kuigharimu serikali juu ya fedha ambazo ni kodi ya wananchi.

Kikao hicho kilichofanyika Ijumaa iliyopita mjini Kilolo kKatika kikao hicho, baadhi ya madiwani wake wamesema kazi nyingi za barabara zimekuwa zikitengenezwa chini ya kiwango na kuwa huenda wakandarasi wanaopewa kazi hizo ni wale wasio na sifa.

“Tuna hofu na hatuna sababu ya kuficha hisia zetu, huenda wakandarasi wanaopewa kazi hizi kwasababu zile zile zilizojificha wakawa ni wale wasio na sifa au wale wanaotumia leseni za watu wengine ili kujipatia fedha,” alisema diwani wa kata ya Idete, Bruno Kauka.

Kauka alisema barabara nyingi zinazotengenezwa wilayani humo huaribika baada ya muda mfupi na kuleta adha kubwa kwa watumiaji wake vikiwemo vyombo vya usafirishaji.

Bila kumtaja jina, alitoa mfano wa mkandarasi aliyepata tenda ya kujenga daraja linalounganisha kijiji cha Kiwalamo na Idete Juni, 2013.

Pamoja na kupewa fedha, mkandarasi huyo ameshindwa kuifanya kazi hiyo hali iliyosababisha mawasiliano ya barabara kati ya vijiji hivyo vinavyotengenishwa na mto Lukosi kukatika.

Alisema zaidi ya wananchi 2,600 wameathiriwa na ukosefu wa huduma hiyo hali inayofanya shughuli zao za kibinadamu zikiwemo za kwenda mashambani na kwenye vituo vya huduma za afya ziendelee kuathirika.

Alisema ili wananchi wa kijiji cha Kiwalamo waweze kufika kijiji cha Medege na kupata huduma mbalimbali zikiwemo za afya wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 20 kwa kuzunguka kupitia kijiji cha Kidabaga, badala ya tano kwa kupitia  darajani hapo.

Malalamiko ya diwani huyo yaliungwa mkono na madiwani wengine akiwemo Anna Msolla wa kata ya Ilula, Israel Mwilafi wa kata ya Ukwega, Fabiola Nzasule wa kata ya Mazombe, Mejusi Mlieveke wa kata ya Kimara na Auzilio Mbilinyi wa kata ya Mtitu.

Madiwani hao walisema halmashauri hiyo inaendelea kutoa tenda kwa wakandarasi wanaonesha kutokuwa na uwezo pamoja na kulipwa fedha nyingi.

“Hatuelewi hizi barabara za vijiji vya Idete, Kiwalamo, vijiji vya Winome, Mawambala, Ukumbi, Lulindi, Mkalanga, Makungu, vijiji vya kata ya Udekwa na Mtandika kwanini hazitengenezwi kwa muda mrefu huku kukiwepo na taarifa za wakandarasi waliopewa kazi hizo wamelipwa fedha... Wananchi wanalia sana juu ya barabara hizo,” alisema diwani Mbilinyi wa mtitu.

Akijibu malalamiko ya madiwani hao, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ubald Wampembe alisema kuwa wakandarasi waliowengi wanapatiwa tenda hizo wakati wa mvua hali inayosababisha wengi washindwe kuzitengeneza kwa hofu ya kuharibiwa na mvua hizo.

Wampembe amesema Halmashauri hiyo itachunguza uwezo na uhalali wa wakandarasi hao kupewa kazi hizo wakati wakiendelea kusubiri mvua zipungue ili ujenzi uendelee.

Kuhusu daraja la mto Lukosi, alisema Halmashauri walishamwandikia barua mkandarasi huyo kwa kushindwa kutengeneza daraja la muda wakati akiendelea kufanya harakati za kulitengeneza daraja hilo.

Idara hiyo pia iliwahi kutiliwa mashaka na Naibu Waziri wa TAMISEMI Agrey Mwanry, alipotembelea mkoa wa Iringa na kufanya ziara za kikazi kwa halmashauri zote za mkoa wa Iringa, na baada ya kukagua baadhi ya miradi ya barabara ya Wilaya ya Kilolo na kukuta kasoro, waziri huyo alilazimika kuomba cheti cha elimu ya darasa la saba cha mhandisi wa Wilaya hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni