Alhamisi, 10 Aprili 2014

WAACHA MASOMO KWA KUKOSA VYOO

 Kibao cha shule ya msingi Ibumila, Iliyopo jimbo la Kalenga, Wilaya ya Iringa.
                      Kuelekea Ibumila.
 Shule ya msingi Ibumila inayotumiwa na wanafunzi 379, ambao sasa wamefunga shule yao kwa utaratibu usio rasmi, walimu wakihofia kuibuka kwa majanga.
 Choo mbadala ambacho kinatakiwa kutumiwa na wanafunzi 379

 Majengo ya vyoo vya awali ambavyo vilititia
 Mashimo ya vyoo hivi si hatari tu kuyatumia, bali nihatari hata kuyasogelea.





Ibumila ikiwa imezizioma baada ya kukosa wanafunzi, kwa kukosa huduma ya vyoo, jambo ambalo linaweza kuibua majanga kwa wanafunzi na Taifa hilo la kesho.

<<<<HABARI>>>>

WANAFUNZI shule ya msingi Ibumila iliyopo Kata ya Mgama katika Wilaya ya Iringa wamelazimika kuacha masomo, na hivyo kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi, baada ya shule kufungwa kwa kuhofia usalama wa maisha yao.

Wanafunzi hao ambao wamekutwa wakifanya biashara mbalimbali, wengine wakiwa katika mapori waking’oa Uyoga na baadhi yao wakichunga mifugo zikiwemo Ng’ombe, wamesema wamelazimika kuwa katika mazingira hayo, baada ya vyoo vya shule kubomoka na uongozi wa shule kuamua kuifunga shule hiyo.

Rahely Nyanginywa mwanafunzi wa darasala la kwanza na dada yake Nida Nyanginywa wa darasa la nne wamesema wanalazimika kufanya biashara ya Uyoga ambao wamekuwa wakiuuza na kusaidia pato la familia.

Sara Nyanginywa na Joshua Nyang’inywa mwanafunzi wa shule ya msingi Ibumila wamesema shule yao baada ya kubomoka walimu waliwataka warudi nyumbani mpaka vyoo vitakavyokamilika, na muda huo wanautumia kuwasaidia wazazi wao.

Sophina Kihaka mmoja wa wazazi wa wanafunzi wa shule ya msingi Ibumila ameiomba serikali iwasaidia ujenzi wa vyoo hivyo ili kuwawezesha watoto wao kuendelea na masomo, kwani hali iliyopo kwa sasa shuleni hapo ni hatari kwa usalama wa wanafunzi.


Suzan Chilimila mwalimu wa shule hiyo amesema shida kubwa nikwea wanafunzi wa kike waliobarehe ambao wanashindwa kumudu haja zao pindi wanapokuwa katika siku zao (Hedhi) na kuwa kukosekana kwa vyoo ni athari kubwa kwa watoto hao wa kike.

Chilimila amesema baada ya kubomokam vyoo vya muda ambavyo vilitandikwa magogo juu ya mashimo, walimu na wanafunzi walijenga uzio wa Nyasi usio na shimo ili kupatikana kwa huduma ya haja ndogo.

Akizungumzia tatizo hilo kaimu mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ibumila Wilfred Mheluka amesema hatua ya kufunga shule imekuja baada ya wanafunzi 379 wa shule hiyo kuwa hatarini kupata magonjwa ya mlipuko kama Kipindupindu baada ya kukosekana kwa huduma hiyo muhimu ya  vyoo.

Mheluka amesema walifiaka hatua hiyo baada ya kuona hatari iliyopo kwa wanafunzi wao, kwani vyoo vyote vimetitia na hivyo wanafunzi kukosa mahali pa kujistiri kwa haja ndogo na kubwa.

Aidha amesema awali waliwataka wanafunzi wa darasa la nne na la saba waendelee na masomo, lakini idadi ya wanafunzi hao iliwafanya washindwe kumudu uwepo wa vyoo viwili vya walimu ambavyo walipanga vitumike na wanafunzi hao.


Amesema hali hiyo ya vyoo vya Nyasi imeonekana ni hatari zaidi kutokana na vyoo vyenyewe kutokuwa na Mahimo na kipindi hiki cha msimu wa mvua mikojo kutapakaa, jambo ambalo linaweza kuibua magonjwa ya mlipuko kwa wanafunzi.

Chilimila alisema tatizo hilo la kukosekana kwa vyoo ni sugu na pia lipo kwa upande wa walimu, kwani nao hulazimika kurudi nyumbani kujisaidia kutokana na uhaba wa huduma hiyo ya vyoo, kwa kuwa vilivyopo ni viwili pekee.

“Vyoo hivi kama unavyoviona, havina staha, mwalimu unaingia wanafunzi wanakuona, havina mlango juu havijaezekwa, kwahiyo mwalimu ukiingia humo unaonekana, kwa hiyo tatizo hili la vyoonikwa upande wa walimu na wanafunzi, tunalazimika kurudi nyumbani, huko nyumbani ukifika unakuta kunamajukumu ndipo hapo unachelewa kurudi shule na kupoteza vipindi vya wanafunzi,” Alisema Chilimila.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Ibumila Gidion Kilipamwambu, Mtendaji wa Kata ya Mgama Willium Msofu na mratibu wa elimu Kata ya Mgama Boazi Ngalutila wamekiri kuwepo kwa tatizo hilo, na kuwa wanajenga vyoo vya muda vya Nyasi ili kumaliza tatizo hilo la vyoo.

Msofu na Ngalutila wamesema kukwama kwa ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo, kunatokana na migogoro ya mara kwa mara, baina ya wananchi na baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji, jambo linalokwamisha shughuli nyingi za maendeleo, hususani jenzi mbalimbali.


Viongozi hao wamesema suala hilo linahitaji ufumbuzi wa haraka zaidi ili kuwanusuru wanafunzi ambao kwa sasa ambao wanatangatanga mitaani, huku baadhi yao wakifanya shughuli hatarishi ambazo zitasababisha kuikosa elimu.

Viongozi hao walikwenda mbali zaidi na kusema baadhi ya wanafunzi wanaweza wakakumbwa na changamoto mbalimbali huko mitaani na katika mapori wanapookota Uyoga, na kubwa zaidi ni wanafunzi wa darasa la nne nala saba kufanya vibaya katika mitihani yao.

MWISHO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni