Jumatatu, 9 Machi 2015

MANISPAA YA IRINGA LAWAMANI KWA KUUZA ENEO LA UJENZI WA SHULE

 Baadhi ya wananchi wa Nyamuhanga- katika Kata ya Kitwiru Manispaa ya Iringa, wakiwa katika mkutano wa dharula wakijadili uuzwaji wa kiwanja ambacho kilitakiwa kujengwa shule ya sekondari.
Baadhi ya wakazi wa Nyamuhanga kisikiliza jambo kwa makini.
 Baadhi ya viongozi wa Kata ya Kitwiru na watumishi wa Manispaa  ya Iringa wakiwa katika mkutano huo wa mgogoro wa ardhi iliyotolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari.. inayodaiwa kuuzwa na Manispaa kwa watu binafsi.


<<<HABARI>>>

WANANCHI wa Nyamuhanga na mitaa iliyopo katika Kata ya Kitwiru mjini Iringa – wameitupia lawama Manispaa ya Iringa kwa  kuuza eneo la kiwanja – lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari, kiwanja kilichotolewa na mmoja wa wananchi wa eneo hilo.

 Mgogolo huo umezuka baada ya awali wananchi hao kudai kuchangia nguvu kazi pamoja na fedha, kwa ajili ya ujenzi wa shule yao ya sekondari katika kiwanja hicho, nguvu kazi ambazo zilielekezwa kwenye ujenzi wa shule ya sekondari Ipogolo.

Wakizungumza katika mkutano wa dharula uliofanyika katika eneo la Pipe line Nyamuhanga- mjini Iringa, wananchi hao wamesema ujenzi wa shule hiyo ulipaswa kuanza mwaka 2012 na ungekuwa umekamilika, lakini umecheleweshwa na maamuzi ya baadhi ya viongozi wa Kata na Manispaa ya Iringa.

Emmanuel Kabongo mjumbe wa mtaa wa Nyamuahanga “C” amesema katika eneo lililotakiwa kujengwa shule, tayari kuna nyumba imejengwa, na hivyo kuwataka viongozi kufuatilia jambo hilo ili kuwapunguzia adha umbali ya kutembea umbali mrefu wanafunzi - kwenda katika shule ya sekondari Ipogolo.

Janeth Myovela mmoja wa watoto wa mwananchi aliyetoa ardhi hiyo ambayo inatakiwa ijengwa shule, amesema ameshangazwa na taarifa za kuwa baba yake “George Myovela” kuwa anamgogolo wa ukoo juu ya kiwanja hicho, kwani baba yake alitoa ardhi hiyo na kuipa jina shule kuwa itaitwa Temihanga Sekondari jina la baba yake na George Myovela.

“Mimi kwa kweli hapa ninashangaa kusikia eti kiwanja hiki kinamgogolo wa kiukoo, hili ndiyo ninalisikia leo, baba yangu alitoa eneo hilo ili ijengwe shule huku akitoa na mawe ili shule itakayojengwa iitwe jina la marehemu baba yake, yaani babu yetu mzee Temihanga,.. mimi kama mtoto wa mzee George Myovela hilo jambo la ugomvi wa kiwanja sijawahi kulisikia au mnamzushia kwa vile baba anaumwa!!?, Alisema Janeth.

Bahati Chaula mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Nyamuhanga “B” amesema mkutano huo umekuja baada ya wananchi kusikia kuwa eneo walilopewa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari kuna jengo la nyumba huku ujenzi mwingine ukiendelea.

Peter Siwa Mwenyekiti wa mtaa wa Kisiwani, amesema kiwanja hicho walipewa mnamo mwaka 2010, ambapo walianza kukusanya mawe na nguvukazi mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari, lakini walipewa taarifa ya kuhamishwa kwa mawe na kupelekwa eneo la Kitwiru katika ujenzi wa shule ya sekondari Ipogolo.

Siwa amesema baada ya kuhoji utaratibu uo wa uhamishaji wa nguvu kazi zao, waliambiwa na viongozi kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa sekondari ya Ipogolo, wangeelekeza nguvu ya pamoja katika ujenzi wa shule katika eneo hlo la Nyamuhanga, na sasa wameshtushwa kuona eneo hilo linaendelezwa ujenzi wa nyumba za watu binafsi.

Baraka Kimata mwenyekiti wa mtaa wa Nyamuhanga .. amesema kukosekana kwa shule katika eneo hilo kutasababisha wanafunzi kukosa baadhi ya masomo kwani eneo hilo halina shule na hivyo wanafunzi hulazimika kutembea umbali wa zaidi ya km 5 kuifuata elimu katika sekondari ya Ipogolo na ..

Kimata amesema licha ya kukosekana kwa shule pia eneo la Nyamuhanga halina huduma za msingi kama Zahanati, Kituo cha Polisi, Soko wala shule ya watoto wadogo - licha ya kutokuwepo kwa maeneo ya wazi.

Aidha Kimata amesema kama ujenzi huo ungekuwa umeanza mapema shule hiyo ingekuwa imeanza kutoa wanafunzi wa kidato cha nne mara tatu, lakini mpaka sasa kiwanja hicho hakina kitu chochote zaidi ya majengo yanayoanza kujengwa na watu binafsi.

Wananchi hao wamesema kamwe hawatakuwa tayari kuchangia michango yoyote ya shughuli za maendeleo, kwani michango mingi waliyotoa haina tija kwao, kwa kuwa imekuwa ikichangia maendeleo katika maeneo mengine na wao wakiendelea kupata taabu ya kuzifikia huduma muhimu za kijamii.

Erneus Kivili mkazi wa Kitwiru, amesema haoni kama kuna uhalali wa kuendelea kuchangia ujenzi mwingine katika shule ya sekondari Ipogolo kwani awali waliambiwa baada ya kujenga majengo matatu ya shule ya Ipogolo– nguvu ya wananchi wote ingehamia katika ujenzi wa shule eneo la Nyamuhanga jambo ambalo kwa zaidi ya miaka 8 sasa halijaanza.

Kivili amesema kumekuwa na michango mbalimbali juu ya ujenzi wa maabara katika shule ya Sekondari ya Ipogolo – michango ambayo inawachanganya, kutokana na ujenzi wa shule yao kutopewa kipaumbele.

Hata hivyo wananchi hao wamesema wamepata tetesi za kuwa Kata ya Kitwiru itagawanyika, na kuwa Kata mbili tofauti, jambo ambalo litakuwa ni hasara kwao wakazi wa Nyamuhanga- kwani michango yao mingi imeelekezwa upande wa eneo litakalokuwa Kata nyingine na hivyo wao kubaki hawana shule, Soko, wala kituo cha afya.

Afisa ardhi wa Manispaa ya Iringa Wicklif Benda amesema manispaa haijauza viwanja katika eneo hilo, na sababu za kutojengwa shule katika kiwanja hicho ni kukosekana kwa vigezo kikiwemo cha kiwanja  kutolipiwa fidia, kukosa mchoro wa mipango miji na pia eneo hilo lina mgogolo wa kifamilia.


Naye Charles Lawiso Mwanasheria wa Manispaa  ya Iringa amesema mgogolo huo utaundiwa timu ya kamati ndogo ya wataalamu ili kutafuta suluhu, na kuwataka wananchi kuwa na subira mpaka kamati itakapotoa majawabu ya nini kifanyike.

MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni