Jumanne, 17 Machi 2015

TIGO WAZINDUA MNARA MAGUBIKE





KAMPUNI ya simu za mkononi ya Tigo, imefanikiwa kufikisha huduma ya mawasiliano kwa wananchi wa kijiji cha Ilalasimba na Magubike, vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ambao awali walikuwa hawana huduma hiyo na hivyo kushindwa kuendesha kilimo cha biashara ambacho kinatajwa kuwa ndiyo chenye tija.

Ujenzi wa mnara wa mawasiliano kwa njia ya simu, umetajwa kuwa utawainua wananchi hao wa Ilalasimba na Magubike, kwa madai kuwa utawawezesha kutafuta masoko ya uhakika na hivyo kuuza mazao yao kwa wakati pasipo kulanguliwa na wafanyabiashara.

Faustino Nyangalima mkazi wa kijiji cha Magubike, amesema awali wametumia muda mwingi kutafuta maeneo yenye mawasiliano (Network) kwani hupanda katika mawe marefu, vichuguu au katika mlima wa Bega kwa Bega ambao upo umbali wa zaidi ya kilomita moja na hali hiyo huwa shida majira ya usiku.

Atanas Lunyali amesema kukosekana kwa huduma ya mawasiliano ya simu kijijini hapo, kumesababisha kudumaa kwa uchumi, kwani licha ya kuendesha kilimo cha mazao ya chakula na biashara lakini wanashindwa kuuza kwa bei inayoendana na wakati, kwa kutokuwa na taarifa za masoko.

Aidha wamesema ujio wa mawasiliano uliowekwa na kampuni ya Tigo utasaidia kukuza uchumi wao, kwani wataweza kujua bei za mazao sokoni kwa njia ya siku, na hivyo kuuza mazao yao kwa bei iliyopo sokoni kwa wakati huo jambo litakaloleta msukumo wa kuendesha kilimo, kwani kitakuwa na tija.

“Tumelima  sana bila mafanikio, na mazao mengi hapa Magubike yanastawi sana, ukichukulia kama zao la Mahindi, Alizeti, Tumbaku, Mahindi  na hata Nyanya yanastawi sana hapa, lakini hali ya maisha ni kama unavyoina, kwa sababu hata tukilima bei ya sokoni hatuijui, na upenyo huo ndiyo waliutumia walanguzi kununua mazao yetu kwa bei ya chini, lakini ujio wa mnara huu wa Tigo – utatuwezesha kufanya mawasiliano kwa njia ya simu kujua bei iliyopo sokoni,  alisema Lunyali.

Renata Mbilinyi- Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Magubike amesema ujio wa mawasiliano kwa wananchi wa kijiji chake, utapunguza migogolo ya kifamilia, ambayo ilikuwa inasababisha hata kuunjika kwa ndoa, kwani baadhi ya wanandoa walikuwa wakitumia mwanya huo kufanya ngono zembe jambo ambalo ni hatari.


Jackson Kiswaga, ni meneja wa Tigo nyanda za juu kusini amesema mawasiliano yanachangia ukuaji wa uchumi kwa asilimia 6, na hivyo kukamilika kwa mnara huo kutaboresha maisha ya wananchi  na kuyafikia maendeleo.

Aidha Kiswaga amesema ujenzi wa mnara huo umegharimu zaidi ya shilingi Milioni 250, na utasaidia kuleta tija katika sekta ya kilimo, jambo litakalowainua wakulima kiuchumi  na hivyo kuwa na maendeleo na maisha bora

John Kiteve- Kaimu mkuu wa Mkoa wa Iringa, ambaye ni mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa wa Iringa- akizindua mnara huo wa Tigo- amesema awali wananchi hao walipata shida ya kutambua soko la mazao kwani hawakuwa na huduma ya mawasiliano na sasa ujio wa Mtandao wa Tigo utarahisisha kuwasilina kibiashara huku wakiendele ana shughuli nyingine.

Hata hivyo  Cecile Tiano mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Tigo amesema mkakati wa Tigo kwa sasa nikuyafikia maeneo yote ya pembezoni mwa miji ambayo awali ilikuwa haina mawasiliano, ambapo minara 843 inataraji kusimikwa,  na kati ya hiyo asilimia 40 itawekwa mikoa ya nyanda za juu kusini.

MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni