Jumanne, 17 Machi 2015

DC- MABULA AAGIZA WAZAZI NA WALEZI WAKAMATWE


Mkuu wa Wilaya ya Iringa Angelina mabula- akisisitiza jambo katika moja ya mikutano yake.

<<<HABARI>>>

VIONGOZI wa serikali za mitaa- vijiji na vitongoji, wametakiwa kuwasaka kwa udi na uvumba wanafunzi wote ambao mpaka sasa hawajajiunga na  masomo ya elimu ya Sekondari, huku viongozi hao wakiagizwa kuwachukulia hatua za kisheria  wazazi ambao wataonekana ni sababu ya watoto wao kutoanza elimu hiyo ya sekondari.

Tamko hilo limetolewa na mkuu wa Wilaya ya Iringa Angelina Mabula, mara baada ya kupatiwa taarifa ya tatizo la utoro wa wanafunzi wa shule ya sekondari Mkwawa, iliyopo katika Manispaa ya Iringa, ambapo zaidi ya wanafunzi 40 mpaka sasa hawajaripoti kuanza masomo.

Mabula amesema ili kukabiliana na hali hiyo- watendaji wanapaswa kutambua idadi ya wanafunzi ambao mpaka sasa hawajaripoti shuleni, na taratibu za  kuwafuatilia majumbani zianze mara moja- ili kufahamu sababu za watoto hao kutoungana na wenzao kuanza kidato cha kwanza.

Evod Luwanda - mkuu wa shule ya Sekondari Mkwawa amesema jumla ya wanafunzi 120 pekee ndiyo wameshajiunga na elimu ya sekondari, na wanafunzi 40 hawajafika mpaka sasa- huku kati yao 16 akiwa hana taarifa zao, wakati wanafunzi 24 wakiwa wamejiunga na shule binafsi kwa ridhaa ya wazazi na walezi wao.

“Mh. Mkuu wa Wilaya.. mpaka sasa ni wanafunzi 120 ambao wamesharipoti na wanafunzi 24 wamekwenda kusoma shule nyingine kwa ridhaa ya wazazi na walezi wao, huku wengine 31 wazazi wao wakijipanga kuwaleta shuleni, na hiyo ni kulingana na hali ngumu ya uchumi,” Alisema Luwanda.

“Mh. Mkuu wa wilaya tatizo la utoro linatusumbua sana shuleni hapa, mfano katika matokeo ya mwaka jana 2014, waliofeli ni wale wanafunzi 7 watoro lakini mwaka huu tumedhamilia kukabiliana na hali hiyo kwa kuhakikisha utoro tunaupunguza kama siyo kuufuta kabisa,” Alisema  Mwalimu Luwanda.

Aidha Mwalimu Luwanda amesema changamoto nyingine inayowasumbua ni pamoja na shule kukosa Maabara, na kutokuwepo ushirikiano wa kutosha baina ya baadhi ya wazazi na walimu, hasa katika suala la michango.

Amesema ili kuendesha shughuli za shule zinazohitaji fedha, hulazimika kukopa fedha kwa wadau ambao ili kufanikisha masuala ya kitaaluma, na kuwa wadau huisaidia sana shule, na hiyo ndiyo sababu inayosababisha shule kuwa na madeni makubwa.

Kunibert Kivinge afisa mtendaji wa Kata ya Mkwawa- amesema watatumia njia ya mgambo kuwakamata wazazai wa wanafunzi ambao mpaka sasa hawajafika shule kwa madai kuwa idadi ya watoto hao inafahamika na kitakachofanyika ni kutafuta majina ya wazazi tu.

Hata hivyo wanafunzi hao ambao mpaka sasa hawajaanza masomo tayari wamepoteza siku 90 tangu shule za sekondari kote nchini zifunguliwe- January 2015.

Kuyakosa masomo kwa muda huo, mpaka sasa tayari wamepoteza  vipindi 420, kwa wastani wa masomo 7 kila siku, na idadi hiyo nikwa mahudhurio ya siku tano ndani ya wiki moja – kuanzia juma tatu hadi ijumaa kwa kipindi cha miezi hiyo mitatu.

MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni