Alhamisi, 22 Mei 2014

WAFUNGA BARABARA KWA TAKATAKA KUISHINIKIZA MANISPAA KUWAJIBIKA


 Baadhi ya wananchi wakiendelea na usafi katika mtaa wa Mlandege manispaa ya Iringa.

 Hali ya takataka katika dampo la Mlandege, tuchafu ambao unadaiwa haujazolewa kwa zaidi ya miezi miwili.

 Moja ya kontena  lililowekwa jirani na manispaa ya Iringa likiwa limechakaa, na hili likiwa na unafuu kwa mengine yanayotumika.
 
 Afisa afya mkuu wa Manispaa ya Iringa, akiwa ofisini kwake akizungumza na mmiliki wa mtandao huu ulipofika katika ofisi hiyo.
 

<<<HABARI>>>
WANANCHI wa Kata ya Mlendege katika Manispaa ya Iringa wamefunga barabara ya Meya wa Manispaa ya Iringa wakiishinikiza manispaa hiyo ya Iringa kuondoa takataka katika madampo ya mjini Iringa, likiwemo la Mlandege ambalo wamesema limetelekezwa kwa zaidi ya miezi mitatu.

Wakilalamikia hali hiyo, wakazi hao wa Mlandege wamesema mlundikano wa takataka katika eneo lao na maeneo mengine ya mji wa Iringa, ni hatari juu ya kuibuka kwa maradhi ya mlipuko huku wakitilia shaka ugonjwa wa Dengue.

Chagu Michael Chali amesema takataka hizo ambazo zinatoka katika maeneo mbalimbali hazijaondolewa kwa miezi mitatu na hivyo kuwepo kwa tishio hasa kwa wakazi jirani na dampo hilo, na hivyo kuamua kufunga barabara inayoelekea nyumbani kwa Meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi ili kuishinikiza Manispaa kupeleka kifaa cha kuhifadhia takataka.

“Tumeamua kufunga barabara hii anayopita Meya, maana kama kuongea tumeongea vya kutosha lakini hakuna lolote tunalosaidiwa, wanatupiga kiswahili kila siku hawa Manispaa, sasa ni bora tufunge barabara hii, hizi takataka ni hatari sana kwa magonjwa ya mlipuko, na hasa huu ugonjwa wa Dengue unaoenezwa na Mbu anayeng’ata mchana, ugonjwa huo unaweza ukazuka kupitia takataka hizi, maana hapa tumezungukwa na vilabu 7 vya pombe za kienyeji, takataka na uchafu wenye maji maji unamwagwa kwenye dampo hili, wanataka kutuua hawa Manispaa,” alisema Chagu.

Said Mohamed amesema kukithiri kwa uchafu katika eneo hilo pia kumechangiwa na Manispaa kuliondoa dampo kwa zaidi ya miezi mitatu, na hivyo wananchi kulazimika kutupa takataka chini, jambo linalosababisha adha kwenye nyumba jirani na Dampo hilo, kwa kuwa takataka zimekuwa zikipeperushwa na upepo na kuingia katika makazi ya watu.

Enock Sanga amesema mlundikano wa uchafu huo ni hatari zaidi kwa kundi la watoto ambao wamekuwa wakicheza nje ya nyumba zilizo jirani na takataka hizo, na hivyo kuitaka manispaa kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa kujituma bila kushinikizwa.

Akijibu tuhuma hizo, Meya Mwamwindi amekiri kuwepo kwa uchafu katika eneo hilo, na kuwa sababu kubwa ni kuwa barabara inayoelekea katika Dampo hilo ilikuwa inatengenezwa kwa kiwango cha Lami, na hivypo magari ya kuchukua takataka kushindwa kuingia kabla ya Lami hiyo kukauka.

Aidha Mwamwindi amelaani vitaka hatua iliyochukuliwa ya wananchi hao kufunga barabara ikiwa pamoja na kufanya maandamano, na kuwa kulikuwa na njia mbadala ya mazungumzo baina ya wananci hao na viongozi wao wa eneo husika.

“Hoja ya kwamba dampo lipo kwenye makazi ya watu si sahihi, kwani Skip Baket zinatakiwa kutengwa katika maeneo ya wazi, na mwenye kupanga dampo likae wapi ni kamati ya maendeleo pamoja na mamlaka siyo mtu mwingine, lakini kilichojitokeza pale ni kwamba barabara pale ilikuwa inatengenezwa, sasa nimeongea na watu wa barabara waone kama magari yanaweza kuingia pale, tulikuwa tunafanya maendeleo kwani ujenzi wa barabara ni meneleo na uondoaji wa takataka nayo ni shughuli ya kimaendeleo, kwa hiyo niombe wawe na subira, lakini hatua waliyoichukua siyo sahihi, siyo ya kiungwana na siyo ya kistaarabu, na mimi siikubari kabisa,” Alisema Mwamwindi.

Amesema tatizo kubwa lililopo ni uhaba wa makontena ya kuhifadhia takataka, kwa kuwa yaliyokuwepo awali kwa asilimia kubwa yameharibiwa kwa kuchomwa kwa moto, na hivyo maeneo mengi kutokuwa na huduma hiyo.

Mwamwindi amesema kontena moja linauzwa zaidi ya shilingi Milioni 8, na uhitaji wa Manispaa ya Iringa ni kontena 100, na hiyo ni kutokana na mji wa Iringa kutanuka na mahitaji  yake kuongezeka kutokana na uzalishaji wa takataka kuongezeka.

Amesema Manispaa inahitaji jumla ya Kontena 100  ambayo ni sawa na shilingi Milioni 800  fedha ambazo ni mapato ya ndani ya Manispaa, na walichokifanya ni kuyafanyia ukarabati makontena 10 ili yaweze kupunguza tatizo hilo.

Afisa afya wa Manispaa ya Iringa Mercy Kiwenekejo amesema suala la usafi wa mazingira linaiguza Manispaa pamoja na jamii, ili kuhakikisha manispaa yao inakuwa safi, na changamoto ni uhaba wa makontena.

Amesema Manispaa ya Iringa ina magari mawili ambayo yanatuimiwa kubeba  Kontena,  na kuwa sasa Kontena zimebaki 28 pekee  kutoka 56 zilizokuwepo mwaka 2000 kupitia mradi wa Sustainable Iringa Project (SIP).

Kewenekejo amesema mahitaji ya sasa ni makubwa na upungufu wa  Kontena ya kuhifadhia takataka unatokana na Kontena mengi kuwa chakavu, na hiyo ni kutokana na baadhi ya wananchi kutupa takataka zikiwa na majivu yenye moto ambao umeyaunguza  madampo hayo.

Hata hivyo Kewenekejo amesema juhudi za halmashauri zinaendelea na katika hatua ya awali Halmashauri imekarabati Kontena (Skip Baket), na katika mwaka bajeti ya mwaka 2015- 2016 kupata Skip Bajet 50 mpya kutoka mradi wa benki ya dunia (Word Bank) huku Manispaa ikiwa na mkakati wa kununua  gari jipya la takataka.

MWISHO



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni