Alhamisi, 26 Juni 2014

MWENGE WAZIUNDUA KIWANDA ISIMANI


 Mkuu wa Wilaya ya Iringa Dk. Retisia Warioba akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerlad Guninita, katika kijiji cha Ilambilole (Wilaya ya Iringa)
 Dr. Retisia Warioba mkuu wa Wilaya ya Iringa akifurahia kuupokea Mwenge wa Uhuru, ambao ulikimbizwa katikavijiji 13 vya Wilaya ya Iringa.

<<<HABARI>>>

WANANCHI wa kijiji cha Isimani kilichopo Kata ya Kihorogota – katika Wilaya ya Iringa wamefanikiwa kujenga kiwanda cha kukamulia Alizeti chenye thamani zaidi ya shilingi Milioni 165 kwa lengo la kuepukana na adha ya kuuza zao hilo la Alizeti kwa gharama ndogo.
                 
Hayo yamezungumzwa na Alfred Chakwe katibu wa kikundi cha Matumaini, wakati akitoa taarifa ya mradi huo mara baada ya kiwanda hicho kuzinduliwa rasmi na mbio za mwenge, kama ishara ya kubariki kazi hizo.

Chakwe amesema lengo la mradi huo ni kuongeza thamani ya zao la Alizeti kwa kuuza mafuta badala ya mbegu za zao hilo, kwakuwa kiwanda kitawawezesha kukamua nafaka hizo na kupata mafuta ambayo sasa yana soko kubwa nchini.

Aidha amesema kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo wa kiwanda cha kukamua mafuta kumechangia na Halmashauri ambayo imewasaidia kiasi cha shilingi Milioni 1 na laki 6 kwa kupitia mpango wa kuendeleza kilimo Wilayani DADPs.

Amesema katika kuinua kiwango cha zao hilo pia wamefanikiwa kujenga ghara la kuhifadhia Alizeti – jengo lenye uwezo wa tani 400,  litakaloondoa shida ya wakulima ya kuuza kwa bei ndogo alizeti hali iliyotokana na wakulima kukosa eneo la kuhifadhia.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Dk. Retisia Warioba amesema mbio za Mwenge wa uhuru zitapita katika vijiji 13, Kata 9 na tarafa 3 zenye umbali wa km 244, huku Mwenge huo ukizindia jumla ya miradi 11 ya maendeleo.

Dk. Warioba amesema thamani ya miradi hiyo ni zaidi ya shilingi milioni 585 ambayo baadhi yake itafunguliwa, mingine itazinduliwa, itakaguliwa na mingine kuwekewa mawe ya msingi.

Naye mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Iringa Pudensiana Kisaka amesema kati ya miradi itakayozinduliwa na Mwenge wa uhuru ni pamoja na ufugaji wa Ng’ombe wa maziwa mradi wenye thamani zaidi ya shilingi Milioni 5.

Aidha Kisaka amesema pia mwenge utazindua nyumba bora ya wanakikundi yenye thamani ya shilingi Milioni 9, pamoja na ujenzi wa nyumba ya mwalimu (Two in One) katika shule ya sekondari Ilalmbilole nyumba yenye thamani zaidi ya shilingi Milioni 50.

Kisaka amesema mwenge huo utazindua daraja Nyakavangala- Mkulula lenye zaidi ya thamani ya shilingi Milioni 151 pamoja na kukagua mradi wa madume ya Ng’ombe bora na wanyamakazi (Maksai) mradi wenye thamani zaidi ya shilingi Milioni 25.8.

Akitaja miradi mingine iliyozinduliwa na Mwenge huo wa Uhuru ni mradi wa kikundi cha Vijana cha Ufugaji Nyuki katika kijiji cha Ihominyi- wenye mizinga ya Nyuki 38 yenye thamani zaidi ya shilingi milioni 3.6.

Hata hivyo Kisaka amesema pia mbio za Mwenge huo wa Uhuru zimezindua matenki 6 ya kuvunia maji ya mvua yenye thamani zaidi ya shilingi Milioni 39.4 katika shule ya sekondari Furahia.

Amesema Mwenge umezindua kituo cha CTC chenye thamani zaidi yashilingi milioni 29 pamoja na mradi wa ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa  na ofisi moja ya mwalimu mkuu iliyogharimu zaidi ya shilingi Milioni 15.9.
MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni