Jumamosi, 26 Julai 2014

MSIGWA- MALIASILI BADO HAWAJAWAJIBISHWA



SAKATA la kampuni ya Green Miles Safaris Ltd, kufutiwa vibali vya uwindaji nchini, limeibuka upya baada ya waziri kivuli wa maliasili na utalii mchungaji Peter Msigwa kusema kamwe hakubaliani na hatua zilizochukuliwa na waziri Lazaro Nyalandu.

Kauli hiyo imetolewa na mchungaji Msigwa ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Iringa mjini – kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA, katika mkutano wake wa hadhara, baina yake na wananchi wa Kata ya Mivinjeni Manispaa ya mji wa Iringa.

Mchungaji Msigwa amesema bado kuna hatua za muhimu zinazopaswa kuchukuliwa na Wizara hiyo ya maliasili na utalii, ikiwa pamoja na kuwawajibisha watumishi wote ambao hawakuwajibika ipasavyo, kwa kuruhusu kampuni hiyo kuvunja taratibu na sheria za uwindaji.

Akitaja watumishi wa idara hiyo wanaopaswa kuwajibishwa, Mchungaji Msigwa amesema mtaalamu wa uwindaji “Professional Hunter”  ni miongoni mwa watu wanaotakiwa kuchukluliwa hatua kwa kushindwa kuzuia kampuni hiyo kuendelea na shughuli zake baada ya kukiuka sheria za uwindaji.

“Katika masuala yale ya uwindaji waziri amechukua baadhi ya hatua yu, lakini kuna madai  mengine  hajayafanyia kazi, mimi kama waziri kivuli nilimuagiza afanye, kwanza nilisema watendaji wote ambao  wamehusika kwa kutosimamia uwindaji kisheria walipaswa wachukuliwe hatua lakini sijaona wamechukuliwa hatua kazi zaao ipasavyo ilipaswa wasimamishwe, lakini sijamuona waziri amechukua hatua yoyote.

…Lakini katika masuala ya uwindaji kuna mtu anaitwa “Profeshno hanta” ambaye  yeye kama uwindaji unakiukwa kwenye vitalu anatakiwa awasimamishe, na kama wanagoma kusimama anatakiwa atoe  ripoti wizarani, kwamba hawa wawindaji walikiuka sheria, kwa mfano hiyo kampuni ya  Green Miles Safaris Ltd walikuwa wanaua wanyama wa kike, walikuwa wanawaua wanyama wadogo, lakini kulikuwa na muwindaji mwenye umri wa miaka 16, jambo ambalo kiuwindaji haliruhusiwi, kwa hiyo waziri bado hajafanya mambo hayo,” alisema Mchungaji Msigwa.


Pia amesema wale wote waliohusika kwa kutosimamia ipasavyo sheria ya uwindaji - nao wanapaswa kuchukuliwa hatua ikiwa pamoja na kuwajibishwa kwa kutokuwajibika na siyo kuiwajibisha kampuni ya uwindaji pekee.

Hata hivyo Msigwa amepongeza hatua ya waziri wa malisili na utalii- Lazaro Nyalandu kwa kuvunja idara ya uwindaji , na badala yake kuweka mamlaka – ambapo amemtaka pia waziri Nyalandu  kuvifanyia uchunguzi wa kina vibali vyote vya uwindaji ili kuokoa wanyamapori hao ambao ni rasilimali kuu ya Taifa.

Alisema endapo hatawawajibisha watendaji wa idara hiyo ya uwindaji, kikombe walichokinywa mawaziri wa idara hiyo waliopita, kamwe Nyalandu naye hakitamuepuka, kwa madai kuwa waziri huyo naye atapaswa kuwajibishwa au kuwajibika mwenyewe.

Kufutwa  kwa leseni za uwindaji kwa kampuni hiyo kulitajwa na waziri Nyalandu kuwa kunatokana na  ukiukwaji wa sheria ya mwaka 2009 ya uwindaji wanyamapori – ambapo kwa kupitia sheria hiyo kifungu namba 5 kinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana kufuta vitalu vya uwindaji kwa kampuni yoyote inayokiuka taratibu zilizowekwa.
MWISHO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni