Watuhumiwa wawili wa ujambazi waliokamatwa Zanzibar juzi na
kupigwa na wananchi na askari wa Kikosi cha Kupambana na Ujambazi,
wamefariki dunia wakati wakiwahishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi
Mmoja, Zanzibar kwa matibabu.
Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Mkoa wa Mjini
Magharibi Unguja, Simon Pasua alisema jana kuwa mmoja wa marehemu hao,
Khamis Othman Mzee (45), mkazi wa Matale, Mji mdogo wa Chakechake Pemba
ametambuliwa na ndugu zake.
Alisema marehemu mwingine aliyejulikana kwa jina
la Khamis Mabunduki ambaye alikuwa mshtakiwa maarufu kwa kufunguliwa
kesi za ujambazi, hajatambuliwa.
Pasua alisema polisi walipata taarifa kutoka kwa
Wakala wa Tigo Pesa kuwa ameporwa mfuko uliokuwa na simu sita aina ya
Tecno katika mtaa wa Mnazi Mmoja na watu waliokuwa katika gari aina ya
Noah na kutoweka.
Alisema baada ya kupokea taarifa hizo, walifungua jalada na kuwasaka watuhumiwa hao.
Alisema majambazi hao waliowakamata saa 8.00
mchana, kabla ya kukamatwa walikuwa wanawakimbia kwa kuendesha gari kwa
kasi na hatimaye waliwagonga watu wanne katika Manispaa ya Mji wa
Zanzibar.
Alisema walipowakamata na kupekua gari lao
walikuta bunduki aina Rifle iliyokatwa kitako, risasi 33 na magamba saba
yaliyokuwa tayari yametumika, mapanga mawili na simu za mkononi.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni