Jumatatu, 9 Februari 2015

USHINDI WA IVORY COAST WAZAA SIKUKUU

Ivory Coast imetangaza Jumatatu kuwa siku ya mapumziko kusherehekea ushindi wake dhidi ya Ghana katika fainali ya kombe la mataifa ya
Afrika.

Ushindi wa mikwaju ya penalti 9-8 usiku wa Jumapili ni wa pili wa kombe hilo katika fainali ambayo ilikuwa ni kama marudio ya fainali ya 1992.

Ushindi huo ulipokelewa kwa shangwe na hoi hoi katika jiji kubwa la nchi hiyo, Abidjan.


Ushindi wa Ivory Coast umemaliza kiu cha miaka 22 ambapo walipoteza mara mbili katika fainali kwa mikwaju ya penati.

Rais Alassane Ouattara alitangaza siku ya mapumziko kwa njia ya redio na televisheni baada ya mechi hiyo.

Sherehe ziliendelea hadi alfajiri katika jiji la Abidjan.

Timu hiyo ilitazamiwa kurejea nyumbani Jumatatu jioni na kukaribishwa katika sherehe kubwa katika uwanja wa kandanda wa Felix Houphouet-Boigny.

Na mashabiki wameambiwa wasihudhurie sherehe hizo kwa kuwa tiketi zote 35,000 zimekwishagawiwa.


 Wachezaji wa Ivory Coast wakishangilia goli
By Caunter Mgaya Jr.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni