Jumatatu, 30 Desemba 2013

BARABARA YA HIFADHI YA RUAHA YAKWAMISHA UTALII


 Wadau wa sekta ya Utalii wakisikiliza jambo katika moja ya vikao vya kujadili mikakati ya namna ya kuendeleza sekta hiyo ambayo ni kiini cha Pato la Taifa.
 Mmmoja wa viongozi wa mradi wa SHICs unaojihusisha na kuendeleza utalii wa mila na tamaduni mikoa ya Kusini (Iringa) akifafanua jambokatika ukumbi wa chuo kikuu cha Iringa, ambapo wadau wa sekta hiyo ya Utalii walikutana.
Yan Kuva meneja wa mradi wa SHICs unaojihusisha na kuendeleza utalii wa mila na tamaduni mikoa ya Kusini (Iringa) akifafanua jambo katika chuo kikuu cha Iringa, ambapo chuo hicho kimepewa dhamana hiyo.
 
MIUNDOMBINU mibovu, ajira za kindugu zisizozingatia utaalamu na kauli zisizofaa, ni moja ya vikwazo vinavyoikwamisha sekta ya utalii mkoani Iringa, licha ya mkoa huo kupewa heshima ya kuwa kitovu cha Utalii nyanda za juu kusini.

Hayo yamezungumzwa na wadau wa sekta ya Utalii mkoani Iringa, katika kikao chenye lengo la kuendeleza Utalii wa mila na tamaduni za jadi, lengo likiwa ni  kuwavutia watalii walio wengi kufika mkoani humo kujifunza maisha ya awali ya makabila ya mkoa wa Iringa, na hatimaye fedha za mapato ya watalii kusaidia kukuza uchumi na pato la Taifa.

Steven Mhapa ambaye ni mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Iringa na mdau wa utalii amesema ubovu wa barabara inayoelekea katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni changamoto kubwa katika kuyafikia malengo ya kuinua sekta ya utalii mkoni Iringa.

“Tunafahamu barabara barabara ni kiungo muhimu sana katika kuwafikisha watalii katika hifadhi, sasa barabara yetu ya Ruaha si rafiki kabisa kwa vivutio vya utalii, na kutokana na hali hiyo baadhi ya watalii wenye uwezo huamua kukodi usafiri swa anga yaani Ndege, huku wenye kipato cha kawaida wakitumia usafiri wa barabara, ambapo hao wamekuwa wakilalamikia sana barabara hiyo na hivyo pindi wanapomaliza utalii wao huwa hawarudi tena, ipo haja ndugu zangu kujipanga vyema hasa katika miundombinu ya barabara,” Alisema.


Afisa utamaduni Wilaya ya Iringa Bi. Joyce Nachilima amesema hata masuala ya utandawazi nayo yanabainishwa kuwa yanachangia baadhi ya vijana kutohitaji tena mambo ya mila na tamaduni za jadi, kuanzia mavazi na hata vyakula, wakihitajika vile tu vinavyokwenda na wakati.

“Vijana wetu wengi siku hizi wanafikilia tu kutunga nyimbo za Bongo fleva ambazo ndiyo zinaitwa za kizazi kipya, na unapowaambia wabuni nyimbo za jadi kama Mangala na Kiduo nyimbo za asili kwa makabila yao wao wanaona kama ni masauala yaliyopitwa na wakati, sasa jambo hilo linakuwa ni gumu sana kufanikiwa maramoja katika sekta ya Utalii wa tamaduni,” Alisema.

Naye Hawa Mwechaga afisa utalii Wilaya ya Iringa amesema wananchi mkoani Iringa wanapaswa kuanza wenyewe kuvitangaza vivutio vya mila na tamaduni za makabila yao, ikiwa pamoja na kuendelea kuvaa mavazi aina ya “Migolole” ambayo yalivaliwa na machifu wa kabila la Wahehe, na kuacha tabia ya kuiga mavazi ya makabila mengine kama ya Wamasai.

Hata hivyo Jimson Sanga ambaye ni katibu wa mradi wa kuendeleza Utalii wa mila na tamaduni mkoa wa Iringa, amesema wananchi mkoani humo wana fulsa nyingi katika kuboresha utalii, hasa kubwa ikiwa ni kipaumbele cha mkoa wa Iringa kupewa heshima ya kuwa ni kitovu cha Utalii nyanda za juu kusini.
MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni