Bidhaa zinazotengenezwa kwa udongo.
Bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa kwa ugongo
WAFINYANZI wa
kikundi cha wanawake kilichopo Lungemba
katika Wilaya ya Iringa, wameiomba serikali na wadau wa sekta ya uchumi na maendeleo,
kuwasaidia vifaa vya kisasa vya
ufinyanzi, ili waweze kutengeneza vitu bora
vitakavyokubalika katika soko.
Hayo
yamezungumzwa na wanawake hao wafinyanzi wa Lungemba, walipotembelewa na
mkurugenzi mkazi wa Umoja wa Mataifa “UN” nchini Tanzania- Alvaro Rodrigues, katika
ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya vikundi vya wajasiriamali, inavyosimamiwa
na shirika la kazi duniani chini ya mpango wa uwezeshaji wa kiuchumi katika
sekta isiyo rasmi.
Anna Nyongole ni
mmoja wa akinamama wa kikundi cha ufinyanzi, amesema wanafanya kazi hiyo katika
mazingira magumu, kwani bado wanatumia mikono pekee, badala ya kutumia vifaa
vya kisasa, na hiyo inasababisha bidhaa zao
kukosa ushindani katika soko jambo linalowadumaza kiuchumi.
“Tunatengeneza
Vyungu, Sufuria, majiko, Mitungi ya maji naya maua, na vitu mbalimbali, lakini
changamoto yetu kubwa ni namna tunavyotengeneza, kwani hatuna mashine za
kuumbia vitu hivyo wala hata mitambo ya kuchomea, tunaiomba serikali itusaidie,
kwani tukipata vifaa vya kisasa tutaweza kutengeneza vitu vingi kwa muda
mchache kuliko ilivyo sasa,” Anasema Nyongole.
Naye Zena Omary amesema kukosekana kwa usafiri wa kusomba
udongo, huwalazimu kutembea umbali wa kilomita 40 kwenda na kurudi, kutoka
katika eneo la Ikekeke katika kijiji cha Kitelewasi, baada ya kukwama kulipia
gharama za usafiri wa gari zaidi ya shilingi elfu 50.
“Tunakokwenda
kuchimba udongo ni Ikekeke katika kijiji cha Kitelewasi, tunatembea km 20
kwenda na kurudi km 20, kwa hiyo unajikuta siku moja umeshindia kuchimba udongo
na kusomba tu, napo hautosherezi maana huwa tunajitwisha kichwani, huwezi kuchukua udongo mwingi,” Amesema Zena.
Aidha wafinyanzi
hao wamesema pia kudumaa kwa soko lao kunachangiwa na baadhi ya jamii kubadili
mtazano, juu ya matumizi ya vitu vya ufinyanzi, huku baadhi ya wananchi
wakichukulia kama vitu hivyo kwa sasa ni kama mapambo tu, hali hiyo ikiwa tofauti kabisa na siku za
nyuma, ambapo vitu vilivyofinyangwa kwa udongo, vilitumika kwa shughuli za
nyumbani kwa kiwango kikubwa.
“Hii hali ya
mabadiliko inatusumbua sana, kwani wengi wanaokuja hapa ni wale wanaotaka
vyungu vya mapambo na maua, hivi vya kupikia na mitungi ya maji haina wateja
wengi, kutokana na watu kuacha kuitumia, kwa hiyo ukitengeneza vyungu na
Mitungi unaweza kujikuta huuzi hata miezi mine hata sita huna hela,” Amesema
Zena.
Licha ya
kukabiliwa na changamoto mb alimbali, akinamama hao wamesema kupitia biashara
hiyo ya ufinyanzi wamefanikiwa kuyabadili maisha yao, kwa kujenga nyumba bora
na hata kuwasomesha watoto wao kwa kumudu gharama za ada.
“Hapa kila mmoja
wetu anayo nyumba ya kisasa- ya tofari za kuchomwa na iliyoezekwa kwa bati, na
pia tumefanikiwa kusogeza huduma ya maji ya bomba katika nyumba zetu, ili
kupunguza usumbufu wa kuchota maji visimani, kama unavyoona bomba hiyo, kwa
kweli biashara hii ya ufinyanzi imetusaidia lakini tukiboreshewa zaidi
mazingira tutakua zaidi kiuchumi,” Walisema.
Hata hivyo Umoja
wa Mataifa UN kupitia shirika la kazi duniani “ILO” Kwa mkoa wa Iringa pekee- limefanikiwa
kuwasaidiaakinamama na
vijana 1800 wa vikundi mbalimbali vya kiuchumi, huku wanachama wa vikundi hivyo
wakipatiwa mikopo, elimu ya maambukizi mapya ya Virus vya Ukimwi, pamoja na mafunzo ya ujasiriamali.
MWISHO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni