Jumatano, 18 Desemba 2013

KATIBU TARAFA AHIMIZA UJENZI WA VYOO BORA



 KATIBU tarafa wa tarafa ya Pawaga Bw. Nasson Mwaulesi (Mwenye suti nyeusi aliyesimama) akisisitiza jambo katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Waziri Willium Lukuvi.

 Waziri Lukuvi akijaribu moja ya Pikipiki huku katibu tarafa Mwaulesi akiangalia kitendea kazi hicho, ambapo Waziri huyo alikabidhi Pikipiki nne ambazo kati yake zilipelekwa  tarafa ya Isimani na Idodi.

 
KATIBU tarafa wa tarafa ya Pawaga Mkoani Iringa Bw. Nasson Mwaulesi amewataka wananchi kujenga vyoo bora na vya mfano ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama Kipindupindu.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kimande, katibu tarafa huyo amesema hakuna njia mbadala ya kukwepa magonjwa ya matumbo pasipo kuboresha mazingira ukiwemo ujenzi wa vyoo hivyo bora.

Aidha Mwaulesi amesema ili kufanikisha mpango huo na kuondokana na vyoo duni atahakikisha ofisi ya afya wilaya ya Iringa inapeleka mchoro wa choo bora kinachotumia ujenzi wa gharama nafuu, ukiwa ni msisitizo wa kuachana na matumizi hayo ya vyoo duni .

"Kuna vyoo vya ajabu sana hapa, vilivyo vingi hata mlango havina, wengine wameweka magunia katika vyoo vyao, na baadhi ya nyumba hazina vyoo kabisa, uongo??...Sasa jamani achaneni na tabia hiyo, kwani uzuri wa nyumba ni choo," Alisema.

Pia aliwataka wananchi na ofisi za vijiji vyote 12 vya tarafa hiyo ya Pawaga kukamilisha ujenzi wa vyoo hivyo ifikapo April mwaka 2014, ambapo alimuagiza mkuu wa Polisi tarafa ya Pawaga kuwachukulia hatua za kisheria wananchi wote watakaokaidi agizo hilo.

Hata hivyo mbunge  wa  jimbo la Isimani ambae ni  waziri  wa nchi  ofisi  ya  waziri mkuu  sera na uratibu wa bunge Mh. Wiliam Lukuvi akikabidhi  gari  la  wagonjwa  lenye  thamani  ya  zaidi  ya Tsh milioni 180 katika kituo cha afya  Kimande Pawaga  amewataka wananchi hao kujiunga na mpango wa huduma ya afya jamii (CHF) ili kuepukana na gharama kubwa za matibabu.

Waziri Lukuvi pia alikabidhi Pikipiki nne zenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni saba, ambapo Pikipiki mbili zilikuwa ni ahadi ya mh. rais Jakaya Kikwete na mbili zilinunuliwa na Waziri Lukuvi, kwa ajili ya ufuatiliaji wa miundombinu ya mradi wa maji bomba.


Katika kuhakikisha wananchi hao hawana vyoo bora Waziri Lukuvi alishindwa kumpata mwananchi hata mmoja mwenye choo bora cha mfano katika kijiji hicho, hatua iliyoonyesha baadhi ya wananchi hao kutolitilia mkazo suala hilo la ujenzi wa vyoo bora.

MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni