Ijumaa, 12 Septemba 2014

WAKAA SAKAFUNI KWA KUKOSA MADAWATI


 Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Igombavanu iliyopo Wilayani Mufindi wakiwa katika moja ya darasa ambalo halina dawati hata moja- hapa wakiandika.
 Wanafunzi wa shule ya Igombavanu wakiandika.
   Mwanafunzi wa shule ya Igombavanu aakiandika.

 
 Baadhi ya wanafunzi wa shule Igombavanu.
 Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Igombavanu iliyopo Wilayani Mufindi wakiwa katika moja ya chumba cha darasa ambacho hakina dawati hata moja- hapa wakiandika.

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Igombavanu iliyopo Wilayani Mufindi wakiwa katika moja ya darasa ambalo halina dawati hata moja- hapa wakiandika.

<<<HABARI>>> 

LICHA ya idara ya elimu kuweka mikakati mbalimbali- ili kuinua sekta hiyo muhimu, bado kuna changamoto mbalimbali zinazokwamisha jitihada za walimu na wanafunzi kuyafikia malengo ya upatikanaji wa elimu bora na hivyo kusuasua kumtokomeza adui ujinga miongoni mwa watanzania walio wengi.

Changamoto kubwa katika sekta ya elimu ya msingi- ni pamoja na uchakavu wa miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo, kwa maana ya vyumba vya madarasa, huku baadhi ya shule zikiwa hazina nyumba za walimu na nyingine zikiwa hazifai kwa makazi ya wataalamu hao wa kada ya Ualimu.

Majengo mengi ya shule za msingi muonekano wake si rafiki kwa utoaji wa elimu, ambayo ndiyo inaimbwa kuwa ni “ufunguo wa maisha ya binadamu” na hiyo nikutokana na sekta hiyo kupewa kisogo- licha ya kuwa ndiyo muhimili wa elimu duniani.

Shule ya msingi Igombavanu iliyopo katika Kata ya Igombavanu- Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa nayo ni moja ya shule zinazokabiliwa na changamoto kama siyo matatizo rukuki, ambayo yanachangia kwa namna moja au nyingine kuidumaza elimu nchini.

Shule hii ya Msingi Igombavanu inakabiliwa na tatizo la uchakavu wa majengo, kwani kwa mujibu wa viongozi husika – shule hiyo haijawahi kufanyiwa ukarabati wa aina yoyote,tangu kuanzishwa kweke tangu miaka ya 70- hali inayosababisha majengo yake kuwa makuu kuu yasiyo rafiki kwa elimu- kwa Walimu na wanafunzi.

Shule ya Igombavanu vyumba vyake vya madarasa havina Sakafu- hali inayosababisha uwepo wa vumbi darasani, na hivyo kuwasababishia magonjwa yatokanayo na vumbi wanafunzi na hata walimu.

Changamoto nyingine katika shule ya Msingi Igombavanu, ni kukosekana kwa milango na madirisha kwa asilimia kubwa ya vyumba vya madarasa, hali hiyo inayodaiwa kusababisha upepo na baridi kali inayowaathiri wanafunzi na walimu.

Uhaba wa madawati ni changamoto nyingine ambayo ni kubwa inayosababisha baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo kukaa sakafuni, na mbaya zaidi darasa la awali wanafunzi wote wakilazimika kukaa chini kwa kukosa Madawati hata moja.

Pia shule ya Igombavanu inakabiliwa na uhaba wa Samani, kama Meza na Viti vya walimu, huku hali mbaya zaidi ikiwa ni Meza na Viti vya walimu madarasani, jambo linalowakwamisha walimu kukagua kazi za wanafunzi.

Uchakavu wa Ubao  (Mbao) za kuandikia darasani, asilimia kubwa ya mbao za shule zimefutika rangi na hivyo kuwawia vigumu walimu kuumba herufi, huku nao wanafunzi wakipata taabu ya kuona kile kilichoandikwa na Mwalimu ubaoni.
Aghai Luhanga na Nuhu Chota ni miongoni mwa wanafunzi wa shule ya Msingi Igombavanu- wanasema kutosakafiwa kwa vyumba vya madarasa kunawasababishia kukohoa, kuchafuka na kuwa uchakavu wa majengo unawatia hofu ya kuangukiwa na kuta za vyumba hivyo vya madarasa.

Angelina Ngogo na Agnes Urio wanafunzi wa darasa la tano shuleni hapo, wasema asubuhi badala ya kuingia darasani hulazimika kumwagilia maji vyumba vya madarasa ili kupunguza vumbi, huku akiiomba serikali iwasaidie kutatua tatizo la uhaba wa madawati.

Yasinta Kiponda, Neema Kalinga na Gilbati Msilu- wamesema uchakavu wa majengo hasa kutokuwepo kwa madirisha na milango kunawasababishia baridi na upepo wawapo darasani, huku upepo ukiwasumbua pindi wanapoandika au kusoma kwa kuwa madaftari na vitabu kupeperushwa na upepo.

Mwalimu Ronjesia Chalamila  na Beatus Kalinga ni walimu wa shule ya Msingi Igombavanu- wamesema kukosekana kwa meza na viti vya walimu darasani kunasababisha ugumu wa kukagua kazi za wanafunzi.

Mwalimu Zailati Kavikule amesema kukosekana kwa rangi za ubao ni changamoto inayowapa wakati mgumu walimu kuandika, kwani herufi hazionekani kwa urahisi na hivyo kutumia muda mwingi wa kipindi katika kazi hiyo.

Walimu wamesema hata nyumba wanazoishi hazina Staha kwani nyumba moja yenye vyumba viwili wanaishi walimu wawili wa jinsia tofauti jambo ambalo si busara, na limekuwa likiwakosesha amani katika majukumu yao ya kazi.
Zelea Komba ndiye mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Igombavanu – anasema shule yake ilianzishwa mwaka 1976 na mpaka sasa hakuna ukarabati uliofantika – jambo linalosababisha majengo kuwa chakavu – huku tatizo la kukosekana kwa milango na Madirisha wakati Sakafu haijasakafiwa kwa Simenti ni jambo linalosababisha Ugonjwa wa Kikohozi na mafua kwa walimu na wanafunzi.

Mwalimu Komba anasema tatizo la madawati shuleni kwake ni kubwa, kwani idadi iliyopo ni madawati 70 pekee huku mahitaji yakiwa ni madawati 191 kwa kuwa darasa la awali linalohitaji Madawati 30 halina hata dawati moja na hivyo kusababisha darasa zima la awali kukaa Sakafuni (Chini).

Mwalimu Komba anasema darasa la kwanza wanatumia vipande chakavu vya Madawati ambavyo nivya madawati ya siku nyingi.

“Tatizo kubwa hapa shuleni ni uchakavu wa majengo, majengo yetu kama unavyoyaona yamechakaa sana, nahii inatokana na shule hii tangu kuanzishwa mwaka 1976 kutokufanyiwa ukarabati, tatizo lingine kubwa ni upande wa madawati, madawati yaliyopo ni 70, na tunahitaji madawati 161 lakini pia tunahitaji madawati 30 kwa ajili ya wanafunzi wa awali kwani wao hawana hata dawati moja, na darasa la kwanza wanatumia vipande vipande vilivyounganisha na vipande hivyo nivya madawati ya muda mrefu,” Anasema Mwalimu Komba.

Mwenyekiti wa Kamati ya shule ye Msingi Igombavanu- Faustine Nyigo- amesema shule hiyo ni kongwe kwani ilianzishwa mnamo mwaka 1976, na tangu mwaka huo haijawahi kukarabatiwa na awali shule hiyo paa lake liliezuliwa na hivyo kuwalazimu kuegesha mabati, ambayo sasa wanahofia kikija kimbunga kinaweza kuleta madhara.

“Kwa upande wa wananchi kwa kweli wanajitahidi sana, kwani pale tunapohitaji michango wanachangia, kwa mfano choo ya wanafunzi wa kike ilititia na wananchi walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanachangia ujenzi wake, lakini hali halisi ya majengo ya shule hii kwa sasa ni hatari,” alisema Nyigo.

Aidha Nyigo ameiomba Halmashauri ya wilaya ya Mufindi kuiangalia kwa jicho la tatu shule hiyo kwani kuna uwezekano wa majengo yake yakadondoka na kuleta madhara makubwa kwa wanafunzi na walimu.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Igombavanu Venancy Kiponda anasema tatizo kubwa ambalo ni kero ni madawati, lakini kwa jitihada za wananchi na mchango kutoka kwa diwani wao walifanikiwa kujenga choo ambayo ilikuwa imebomoka.

Akizungumzia mpango wa upatikanaji wa Vibali vya uvunaji wa miti katika shamba la Taifa la Sao hill, Kiponda anasema hawana taarifa juu ya umiliki wa rasilimali hiyo, ila wamekuwa wanasikia tu, na endapo wangepata fulsa hiyo wangeondokana na tatizo la uhaba wa madawati kwa shule yao.

“Ee Katika hilo suala la vibari limekuwa ni haditrh kwani sisi huku tunasikia tu, kwani hakuna hata mwananchi mmoja ambaye anapata vibali, lakini sisi huku hicho kitu hatumkitambui, sasa nilikuwa ninaomba tupewe kipaumbele kwani hali ya michango kwa wananchi imekuwa ni kero lakini kama tukipewa kibali tunaweza kutatua changamoto zinazokikabili kijiji chetu,” Alisema

Rashid Mkuvasa ni diwani wa kata ya Igombavanu- anasema baada ya kupata kibali cha Kata cha uvunaji wa miti katika Shamba la taifa la sao hill alinunua Bati 50 kwa ajili ya shule ya msingi Lugodalutali, huku katika kijiji cha Igombavanu akitumia shilingi laki 8 kwa ajili ya kuchimba choo cha shule.

Aidha Mkuvasa amesema katika fedha hizo zilizotokana na Kibali cha kata - shilingi Milioni 1.4 zilisaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Matelefu, huku shule ya msingi Makongomi akiipatia Bati 24 na Mifuko 10 ya Saruji, pamoja na kuchimba kisima cha maji katika kijiji cha Lugodalutali – mradi uliogharimu kiasi cha shilingi laki 4 na elfu sitini.

Hata hivyo Mkuvasa ameiomba Halmashauri ya wilaya ya Mufindi kusaidia ujenzi na ukarabati wa shule za kata hiyo, kwa madai kuwa majengo yake ni chakavu, na wananchi pekee kamwe hawawezi kumudu gharama hizo.

Afisa elimu shule za msingi Wilaya ya Mufindi Mwasumilwe, amesema Wilaya ina madawati zaidi ya 27, huku wanafunzi wakiwa zaidi ya elfu 64, huku hitaji la madawati likiwa ni zaidi ya elfu 32 na hivyo upungufu kufikia madawati elfu 4269.

Mwasumilwe amesema katika kukabiliana na uhaba wa vyumba vya madarasa, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa kipindi cha mwaka 2014/ 2015 imeadhimia kujenga  vyumba 28 vya madarasa pamoja na nyumba 5 za walimu- lengo likiwa ni kuboresha mahali pa kuishi walimu na kuboresha mazingira ya elimu.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Evarista Kalalu akizungumzia changamoto hiyo ya Madawati na mazingira ya shule zake wilayani humo, anasema Wilaya yake ina mpango wa kukabiliana na uhaba wa Madawati

“Kweli tumekuwa na shule nyingi za msingi… lakini pia ongezeko la wanafunzi nalo limekuwa ni kubwa, serikali inaboresha mazingira ya shule kwa maana ya madarasa, Samani, walimu pamoja na Vitabu….

Lakini kitu ambacho kimekuwa midomoni mwa watu kwa kipindi kirefu ni madawati, lakini kimsingi katika Wilaya ya Mufindi wanafunzi wakipangwa watatu watatu hatuna upungufu wa  dawati hata moja, tunaziada ya madawati karibu elfu 4, tunapozungumzia upungufu wa madawati tunataka tuhamishe wanafunzi wanaokaa watatu watatu wakae wawili wawili wasome kwa nafasi ….na hili tumeshaanza kwani hata vibali ambavyo vimetoka hivi karibuni viongozi husika wa vijiji tumewahimiza kuwa suala la msingi nala kuanzia ni kwenda kwenye upungufu wa madawati,”   Alisema Kalalu.

Hata hivyo Mahamoodu Mgimwa, mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini- ambaye pia ni naibu waziri wa maliasili na Utalii- ambako shule hiyo ya msingi Igombavanu inapatikana- amesema amejipanga vyema kumaliza kabisa tatizo la uhaba wa madawati katika shule za jimbo lake na mpango wa kuelekeza mgao wa Vibali vya miti vijijini, umelenga kupunguza adha ya wananchi kuchangia masuala ya maendeleo hususani yahusuyo elimu.

MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni