WANAFUNZI wa
shule ya sekondari Igowole- iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi
mkoani Iringa, wapo katika hatari ya kuangukiwa na majengo ya mabweni
wanayolala, na hiyo ni kutokana na majengo hayo kutokufanyiwa ukarabati kwa
muda mrefu.
Licha ya
uchakavu wa majengo, pia shule hiyo ya Sekondari Igowole inakabiliwa na changamoto
mbalimbali, ikiwemo ya uhaba wa vitanda, jambo linalowalazimu
wanafunzi kulala zaidi ya mmoja huku baadhi yao wakilazimika kulala sakafuni,
kutokana na vubovu wa Vitanda na uhaba usiowiana na idadi ya wanafunzi.
Hayo
yamezungumzwa na wanafunzi katika mahafali ya sita ya kidato cha sita, ya shule
ya sekondari Igowole, ambapo suala la uchakavu wa majengo ya bweni yameonekana
kuwa ni kero ambayo inawanyima usingizi wanafunzi hao.
Mwani Mwilenga, Magreth
Mkane na Diana Balali ni wanafunzi wa kidato cha tano Igowole, wamesema
mazingira magumu yaliyopo shuleni hapo, endapo hayatatafutiwa ufumbuzi wa kina,
yanaweza kusababisha shule hiyo kushuka kitaaluma licha ya kuwa shule hiyo
kwa sasa inaongoza Kitaifa kwa kushika nafasi ya kwanza katika matokeo ya kidato cha
Sita- “Tanzania One”.
Naye Upendo Kopa
na Consia Frenk ni miongoni mwa wanafunzi wanaohitimu elimu ya kidato cha Sita,
wamesema pia changamoto ya shule kukosa uzio ni hatari kwa wanafunzi hasa wa kike,
huku suala la huduma ya maji nalo likitajwa kuwapa wakati mgumu wa kujisomea.
“Mimi ninamaliza
elimu yangu ya kidato cha sita leo, lakini hali ya shule hii ni mbaya, kwani
mabweni yapo katika hali ambayo si nzuri, kwa maana si rafiki kielimu, pia
huduma ya maji tunaipata mbali, kwa hiyo wakati mwingine wanafunzi tunaacha
vipindi vya masomo na kufuata huduma hiyo,” Alisema Upendo.
...“Kuna wakati
hapa shuleni ulizuka ugonjwa wanafunzi tuliugua na baadhi yetu kufikia hatua ya kulazwa kwa ajili ya matumizi ya maji yasiyo
salama, kwa hiyo tunaiomba serikali iiangalie kwa jicho la pekee shule hii,
kwani mazingira haya magumu yanaweza kuporomosha taaluma,” alisema Consia.
Mwalimu Andrew
Kauta ni mkuu wa shule ya sekondari Igowole, amesema katika kukabiliana na hali
hiyo, mbunge wa jimbo la Mufindi Kusini Mendrad Kigola alitoa msaada wa bati
260 na mifuko ya saruji 100.
Mwalimu Kauta
amesema kupitia msaada huo kuna mpango wa ujenzi wa bweni lenye uwezo wa
kuchukua wanafunzi 130 hadi 150, ikiwa pamoja na kununua vitanda zaidi ya 100
ambavyo vitagharimu zaidi ya shilingi Milioni 15.
Kauta amekiri kutokuwepo uwiano wa Vitanda, Mabweni na idadi ya wanafunzi, na kuwa kuna upungufu, na kuwa baadhi ya mabweni hayapo
katika viwango vinavyotakiwa, na mkakati wa shule ni kubomoa majengo hayo ili
kujenga majengo yenye ubora unaofaa.
Hata hivyo hali
halisi ya vitanda hivyo ni chakavu, kwani baadhi yake havina hata ngazi ya
kupandia, na hiyo ni kutokana na vitanda vya bweni kuwa vya ghorofa, na hivyo
hali ya kukosekana kwa miundombinu ya kupandia kunawapa wakati mgumu wanafunzi, huku baadhi ya wanafunzi wasio wazoefu kwao kuwa
katika hatari ya kuvunjika wakati wakiparamia vitanda hivyo muda wa
kulala.
Vipo vitanda ambavyo vimevunjika na hivyo kutoa
fulsa kwa wanafunzi kutumia mbinu mbadala ya kuvifunga kwa kamba, na hali hiyo
kuwa tishio kwa baadhi ya wanafunzi kuhofia kuanguka.
Aina ya milango ya mabweni niya Bati, na baadhi
yake haina bawaba – nyenzo inasaidia
mlango ufunge na kufunguka, kwa hiyo wanafunzi huegesha tu mlango huo na
wanapotaka kutoka au kuingia ndani huunyanyua kuingia nao ndani au kuuweka
pembezoni.
Pia suala majengo ya bweni, ni mafupi hali
ambayo mwanafunzi anayelala kitanda cha juu – humuwia vigumu kuendelea
kujisomea, kwani paa lake linamzuia mwanafunzi kukaa na hiyo ni kutokana na
bati kutomruhusu kunyoosha shingo.
Licha ya
changamoto zote hizo zinazowakabili wanafunzi wa Igowole, kero ambazo pia ni changamoto kwa walimu, lakini shule
hiyo ya sekondari Igowole, imeweza kuuweka mkoa wa Iringa kuwa katika sifa ya pekee,
kwa kung’ara - katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita, kwani shule hiyo imeshika nafasi ya kwanza Kitaifa katika matokeo hayo ya mwaka 2014.
Basi kuna kila
sababu - wadau mbalimbali wa elimu kwa kushirikiana na Serikali kufanya kila liwezekanalo ili kuziondoa
changamoto za kielimu zinazoikabili shule hiyo kongwe ambayo inatakribani
miaka 27 tangu ianzishwe, lengo likiwa ni kuyafanya mazingira ya shule hiyo kuwa
rafiki kwa kufundishia na kujifunzia.
MWISHO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni