Alhamisi, 8 Mei 2014

KALOLO AAGWA KWA AINA YAKE- MJI WAZIZIMA








 Mwili wa marehemu Gervas Kalolo ikiwasiri katika makaburi ya Kihesa kwa ajili ya safari yake ya mwisho hapa duniani.
 Ndugu wakiweka mchanga wa mwisho kama ishara ya kumuaga mpendwa wao.
 Hali ilivyokuwa Kanisani, ni baadhi tu ya waombolezaji waliohudhuria misa hiyo ya kumuaga mpendwa wao.



 Marehemu Gervas John Kalolo, akiwa katika moja ya mikutano ya chama chake cha demokrasia na maendeleo CHADEMA enzi za uhai wake.
Jeneza lenye mwili wa marehemu Gervas Kalolo likitolewa ndani kwa safari ya  kuelekea Kanisani kwa ajili ya misa Takatifu ya kumuombea marehemu. 
 Marehemu Gervas Kalolo, akiwa na mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freemn Mbowe katika moja ya mikutano ya  CHADEMA enzi za uhai wake.
 Marehemu Gervas John Kalolo, enzi za uhai wake.
 <<<<<<<<<<<HABARI>>>>>>>>>>

HATIMAYE aliyekuwa kiongozi wa Chama Cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA mjini Iringa Gervas John Kalolo, aliyefariki siku ya jumatatu usiku jijini Dar es salaam amezikwa leo katika makaburi ya Kihesa mjini Iringa.

Umati wa watu waliofurika katika msiba huo, umeandika historia ya pekeyake, kwa wananchi na wakazi wa mji wa Iringa na viunga vyake, ambapo waombolezaji katika msiba huo wamefanya maandamano makubwa ya matembezi ya waenda kwa miguu, waendesha Pikipiki, Bajaj, Magari madogo na makubwa.

Maandalizi ya maziko ya Kalolo ambayo yalianza mara tu baada ya kutokea kifo chake, yamefanyika nyumbani kwake katika mtaa wa Mashinetatu, katikati ya mji, eneo maarufu mjini Iringa, lenye maduka kadha wa kadharika, ambapo  leo tangu majira ya asubuhi maduka na shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo hufanywa  katika maeneo hayo zimesitishwa, huku maduka yote yakifungwa  kwa lengo la wafanyabiashara hao kumsindikiza Kalolo katika safari yake ya mwisho.

Majira ya saa sita mchana, jeneza lililokuwa na mwili wa Marehemu Gervas Kalolo lilitolewa nje ya nyumba yao Mashine tatu-kwa ajili ya kuianza safari ya kuelekea katika Kanisa la  Mshindo mjini Iringa, huku waombolezaji hao wakiandamana kwa miguu na kuyaacha magari hadi wakisindikiza gari lililokuwa limebeba Sanduku/ Jeneza lenye mwili wa Kalolo hadi katika kanisa la Mshindo.

Msafara huo uliongozwa na gari la CHADEMA Double Cabin - M4C lililokuwa limebeba Sanduku lenye mwili wa marehemu, pamoja na baadhi ya ndugu wa karibu wa marehemu, huku nyuma kulikokuwa na jeneza kukipambwa na viongozi wa CHADEMA waliokuwa wamevalia Suti nyeusi, Tai nyekundu na miwani mieusi.

Nyuma ya gari hilo zilifuatia Pikipiki, Bodaboda na Bajaj zinazofanya shughuli zake mjini Iringa, huku nyuma kukiwa na umati mkubwa wa waombolezaji, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wenye mapenzi mema na marehemu Kalolo wakitaka kushuhudia safari hiyo ya mwisho ya mpendwa wao.

Umati huo mkubwa ambao ulijaa ndani ya Kanisa Kathoriki la Mshindo, huku misa ikiongozwa na Padre, huku washiriki wa misa hiyo wakiwa mchanganyiko kwa maana ya kuwa ..hata wale wasio na imani ya dhehebu hilo nao wakishiriki misa hiyo takatifu, lengo likiwa ni moja tu, kumuombea marehemu wao.

Majira ya saa nane na nusu misa ilimalizika ambapo waombolezaji waliuaga mwili wa marehemu Kalolo ndani ya kanisa hilo, na baada ya kumaliza zoezi hilo, safari ya kuelekea malaloni katika makaburi ya Kihesa ilianza, huku utitiri wa magari na kila aina ya usafiri  uliosababisha msongamano wa aina yake katika barabara kuu mbili za mjini Iringa, kwani kila mmoja alitaka kuwa shuhuda wa maziko hayo.

Katika msafara huo kulikuwa na zaidi ya Pikipiki 30, Bajaji 15 magari yasiyopungua 200 makubwa na madogo yalielekea katika makaburi ya Kihesa, ambako huko ndiko wamelala (wamezikwa) wanandugu wa ukoo wa akina Kalolo.

Zoezi la mazishi liliaanza huku  likichukua zaidi ya masaa matatu,  likiongozwa tena kwa misa ambayo iliendeshwa na Katekista wa kanisa Katoriki la Mshindo, hali hiyo inatokana na marehemu kuwa muumini mzuri na mshiriki wa shughuli mbalimbali za Kanisa.

Mazishi ya Kalolo yalianza,  jeneza lake lilishushwa katika Kaburi lililojengwa kwa matofari na saruji/Sement,  huku Mshereheshaji MC akiwaomba waombolezaji - baadhi ya ndugu wa karibu pekee ndiyo watakaohusika katika kuweka udongo wa mwisho kama ni ishara ya kumuaga mpendwa wao, kauli iliyotolewa ili kulinda muda, kutokana na utitiri wa watu walkiofika katika tukio hilo.

Mfuniko wa Kaburi uliwekwa juu ya kaburi, ambapo watoto 4 wa marehemu Kalolo wakiongozwa na mtoto mkubwa wa kiume John Kalolo walizindua zoezi la kuweka Mashada, wakifuatiwa  na wawakirishi wa ndugu, jamaa, marafiki, majirani nk.

Wasifu na historia ya marehemu ilifuatiwa, huku historia ikigawanyika katika mafungu matatu-:
1.  Historia ya uongozi ndani ya Chama cha mapinduzi CCM
2. Historia ya uongozi ndani ya Chama cha Demokrasia na  maendeleo CHADEMA.
3. Historia ya familia tangu kuzaliwa, kusoma mpaka mauti yanamfika.

Katika misiba mingi imezoeleka kuwa kwenye maziko wananchi na waombolezaji huanza kuondoka makaburini mara tu mazishi yanapomalizika kwa maana ya tukio lenyewe la kuufukia mwili wa marehemu kaburini, lakini hali ilikuwa tofauti katika mazishi ya Kalolo, ambapo waombolezaji walibaki hadi dakika ya mwisho licha ya kuwa zoezi hilo lilikuwa limechukua masaa mengi.

Kwa kifupi Kalolo amewahi kuwa barozi wa mtaa wa mashine tatu, mwenyekiti wa mtaa huo wa mashinetatu, diwani wa Kata ya Miyomboni/ Kitanzini, ambapo mwaka 2010 katika uchaguzi mkuu hakufanikiwa kukitetea kiti chake cha Udiwani, ambacho kilichukuliwa na Mariam Nyanginywa kwa sasa ni Marehemu.

Marehemu Kalolo alibadili mlengo na kuingia chama cha CHADEMA ambapo mpaka kifo kinamkuta alikuwa ni kiongozi wa CHADEMA mkoa wa Iringa, huku akiwakirisha vema nafasi yake hiyo, kutokana na kuwa na uwezo mkuwa wa kujenga na kutetea hoja.

Baadhi tu ya sifa alizokuwanazo Marehemu Gervas Kalolo, ambazo zilimfanya afahamike, kama si kujulikana ndani na nje ya mji wa Iringa na viunga vyake, kwa watoto, vijana, watu wazima, watu wa makamo, wazee na vikongwe ni UCHESHI, UWAZI, UKWELI, HURUMA, USHIRIKIANO, UWEZO MKUBWA WA KUFIKIRI NA KUYACHAMBUA MAMBO MBALIMBALI, KUJIAMINI, MSIMAMO nk.

Kutokana na sifa hizo ambazo baadhi ya watu licha ya kuwa nazo lakini huogopa kuzitumia kama Ukweli na uwazi, Kalolo sifa hizo zilimfanya awe Mwenyekiti mtarajiwa Iringa Mjini.

Baadhi ya viongozi walioshiriki katika mazishi hayo ni Mbunge wa Iringa mjini CHADEMA Mchungaji Peter Msigwa, Meya wa mji wa Iringa Amani Mwamwindi, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Abeid Kiponza, kamanda wa Vijana mkoa wa Iringa Salim Abri Asas, Madiwani wa Manispaa ya Iringa, Kiongozi wa M4C Kanda ya Kusini Frenk Mwaisumbe.

Kalolo alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumanne jijini Dar es Salaam alikokuwa amekwenda kwa shughuli zake binafsi, ikiwa pamoja na kupatiwa matibabu, ambapo ameacha watoto wanne, na wengine watoto wa hiari, ambao ni watoto Yatima, waishio katika mazingira magumu na hatarishi, ambao alikuwa akiwalea na kuwapatia mahitaji mbalimbali muhimu kama kuwalipia ada/Karo za shule pamoja na kuwapatia mahitaji mbalimbali.

Mwili wa Kalolo uliwasili mjini Iringa siku ya Jumatano asubuhi na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa wakati ndugu wakiendelea na taratibu mbalimbali za mazishi yake.

"BWANA ALITOA, BWANA AMETWAA, JINA LA BWANA LIHIMIDIWA......Amen!!"

MWISHO.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni