Mwenyekiti wa umoja wa "wanakihesa" Mussa wanguvu akizungumza jambo mbele ya Naibu Waziri wa maliasili na utalii Mh. Mahamoodu Mgimwa, (Mwenyemiwani kushoto) katika sherehe ya siku hiyo ikiwa pamoja na furaha ya wanaumoja wa Kihesa kutimiza mwaka mmoja tangu umoja huo uanzishwe.
Moja ya jengo la Hotel ya Country Sid ambapo wanaumoja huo walifanyia sherehe zao, moja ya Hotel ya mkazi wa Kihesa.
<<<<HABARI>>>>
WAJASIRIAMALI
kote nchini wametakiwa kuchangamkia fulsa zilizopo katika wizara ya maliasili na Utalii, ili kwenda
sambamba na hali halisi ya maisha kwa kufanya biashara ambazo zinamvuto kwa
watalii kwa lengo la kukuza uchumi.
Rai hiyo
imetolewa na naibu waziri wa maliasili na utalii Mh. Mahamoodu Mgimwa, wakati
wa sherehe ya umoja wa “Wanakihesa”,
kikundi kilichopo mjini Iringa ambacho kilikuwa kinatimiza mwaka mmoja
tangu kuanzishwa kwake.
Mgimwa amesema
fulsa zilizopo katika sekta ya maliasili na utalii ni nyingi na zikichangamkiwa, zitaleta tija kwa jamii na
hivyo kukuza uchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla, kwa madai kuwa serikali
imejipanga vyema kwa kuelekeza nguvu zake katika sekta hiyo ya utalii kwa mikoa ya Kusini.
Mgimwa amesema
kwa sasa mkoa wa Iringa unafulsa nyingi za utalii, hususani katika hifadhi ya
mbuga ya Taifa ya Ruaha ambayo ni ya pili kwa ukubwa Afrika na hivyo kuwataka wananchi kutumia
nafasi hiyo pasipo kuwaachia wageni kutoka nje ya nchi.
Aidha amewataka
wananchi kuelekeza nguvu katika ujenzi wa Hotel za kisasa ambazo zitasaidia
kuwapokea watalii, ili wavutiwe na makazi na malazi ya kufikia, ikiwa pamoja na
kuboresha elimu kwa wahudumu wa Hoteli hizo.
“Tatizo la sisi
watu wa nyanda za juu kusini hatuwa tayari kutumia fulsa zilizopo, maana kwa
maana ya utalii – utalii upo nyanda za juu kusini, lakini watu bado
hawajachangamkia fulsa hiyo, tunayo
hifadhi ya Ruaha ambayo niya pili kwa ukubwa Afrika, kuna maenepo mengi sana ya
utalii kama Kitanzinie yaliyotumika kunyongea watu, Kalenga sasa labda
niwahimize wananchi wa kusini watumie fulsa zilizopo kama wanavyofanya wenzetu
wa nyanda za mikoa ya Kaskazini,” Alisema Mgimwa.
Amesema wakazi
wa mikoa ya kusini wanapaswa kufunguka katika fulsa hizo, huku akitaja uwepo wa
vivutio mbalimbali vya kusini vikiwemo Vyura vinavyozaa badala ya kutaga mayai,
vilivyopo katika maporomoko ya Kihansi
kwa madai kuwa vyura hivyo havipo popote duniani.
Katibu wa umoja
huo July Sawani amesema changamoto kubwa inayoukabiri umoja huo ni pamoja na
uwepo wa idadi kubwa ya watoto Yatima na waishio katika mazingira hatarishi,
ambao wamekwama kuipata elimu, na Umoja umeanzisha mfuko wa elimu.
Sawani amesema
changamoto nyingine ni uwepo wa baadhi ya watu wasioutakia mema umoja, ambao
wanatafuta njia mbalimbali za kukwamisha mipango, na kuwa wanakabiliana na
kundi hilo kwa kuwapa elimu ili waondokane na dhana hiyo isiyo na mlengo wa
maendeleo.
Naye mwenyekiti
wa Umoja wa Wanakihesa Mussa Wanguvu amesema tayari wamefungua Saccos kwa ajili
ya kuinua hali ya uchumi wa wanachama wao, na mpango mkubwa ni kufanikisha
mikakati ya kufungua benki ya wananchi.
“Tunawanachama
zaidi ya wanachama 1000, na lengo letu ni kufungua benki, kwa sasa tumefanikiwa
kufungua Saccos yenye wanachama 200 na mtaji wa zaidi ya mtaji wa Milioni 10 na
adhma ya mpango huo wa Saccos ni kuwa na zaidi ya shilingi Milioni 25,”
Alisema.
Wanguvu amesema
lengo ni kuwashirikisha wananchi wote wa Kata tatu ya Gangilonga, Kihesa na
Mtwivila ili kulifikia lengo hilo la ufunguaji wa Benki hiyo ya wananchi, huku
akiwaomba wananchi kujiunga na umoja huo.
Hata hivyo Mussa Wanguvu amesema tayari umoja huo
unavikundi mbalimbali vinavyofanya shughuli za kiuchumi, ukiwemo utengenezaji
wa vitenge vya Batiki na vitu vya utalii kama ni sehemu ya kuchangamkia fulsa
iliyopo katika Wizara ya Maliasili na utalii.
MWISHO.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni