Jumanne, 20 Mei 2014

WAUGOMEA UWAKIRISHI WA BUNGE LA KATIBA



 Baadhi ya watoto wenye mahitaji maalumu, wanaohudumiwa na shirika la Compassion, wa vituo 12 vya mkoa wa Iringa wakipatiwa mafunzo ya kuwajenga kiakili, kimwili na kiroho, katika ukumbi wa chuo cha maendeleo ya jamii - Lungemba.
 Afisa ustawi wa jamii Manispaa ya Iringa Josephine Mwaipopo akizungumza na watoto katika ukumbi wa chuo cha maendeleo ya jamii - Lungemba, katika kambi ya siku tatu ya watoto hao ambao walifika katika kongamano hilo kujifunza mambo mbalimbali.

 Baadhi ya walimu wakiwa nje ya majengo ya chuo cha maendeleo ya jamii- Lungemba mara baada ya kumaliza mafunzo kwa watoto walikokutana katika kambi hiyo ya kujifunza masuala mbalimbali.
 Baadhi ya walimu wa vituo vya shirika la Compassion, wakiwa nje ya uwanja wa chuo cha maendeleo ya jamii - Lungemba Wilayani Mufindi mkoa wa Iringa.
 Walimu wa vituo 12 vya shirika la Compassion, mkoa wa Iringa wakiwa katika picha ya pamoja, katika chuo cha maendeleo ya jamii- Lungemba, mara baada ya kambi ya watoto wa wanaohudumiwa na shirika la Compassion kumalizima rasmi.

 Walimu wa vituo 12 vya Compassion, wakiwa katika picha ya pamoja, katika chuo cha maendeleo ya jamii- Lungemba, mara baada ya kambi ya watoto wa wanaohudumiwa na shirika la Compassion kumalizima rasmi.

 <<<HABARI>>>

WAKATI bunge la katiba likiwa limesitishwa kwa muda, kulipisha bunge vikao vya bunge la bajeti linaloendelea  hivi sasa Dodoma,  jumuiya ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, wameilalamikia serikali kwa kutowashirikisha katika mchakato wa kuijadili rasimu ya mapendekezo ya katiba mpya.

Hayo yamezungumzwa na watoto wanaohudumiwa na shirika la Compassio mkoani Iringa, katika Kongamano la watoto zaidi ya 300, waliokutana katika kambi ya chuo cha maendeleo ya jamii Lungemba, kilichopo katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.

Kongamano hilo   ambalo limevikutanisha viyuo 12 vinavyohudumiwa na shirika la Compassion  mkoani Iringa, lengo likiwa ni kubadilishana mawazo watoto hao juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabiri.

Watoto hao wamesema katika bunge la katiba, hawaoni umuhimu wa wao kutengwa na kuwatumia watu wazima kama wawakirishi, wakati wao watoto wanao uwezo mzuri wa kujieleza juu ya masuala mbalimbali yanayowasibu.

Wamesema tatizo la ukatili kwao limekuwa likiongezeka siku hadi siku, jambo ambalo wangependa iwekwe sheria kali ya kuwaadhibu wale wote wanaotenda uovu huo kwa kundi lao la watoto, na kwa uwakirishi uliopo mambo mengi yanayowasumbua hayatazungumziwa kwa madai kuwa wawakirishi hao huenda wakati wakiwa watoto hawakukutana na matatizo kama yanayowakumba wao sasa.

Julius Kivike ni kati ya watoto wanaolelewa na shirika la compassion amesema hakuna haja ya wao watoto kuwakirishwa kwani wanao uwezo mzuri wa kutetea haki zao, na sasa serikali ione umuhimu wa kupeleka mwakirishi kutoka kundi la watoto ili kufikisha changamoto zao wanazotaka ziingizwe kwenye katiba mpya.

Akizungumzia sababu ya kuhitaji nafasi hiyo, Julius amesema uwakirishi unaofanywa na watu wazima hauna manufaa kwao, kwani kuna uwezekano mkubwa mwakirishi huyo akawa hajapitia changamoto zinazowakabiri wao.

“Hatutaki kuwakirishwa na watu wazima, sisi wenyewe tunao uwezo wa kuzungumza mambo yetu, unaweza kuona huyu anayetuwakirisha yeye wakati mtoto alilelewa kwenye familia yenye uwezo, kwa hiyo hafahamu machungu tunayoyapa sisi watoto, tunataka wenyewe ndiyo tukajisemee mambo yetu,” Alisema.

Aidha Julius amesema matatizo yanayowakumba baadhi yao hufikia kupoteza maisha, kwa kukosa huduma muhimu na sababu kubwa ni kukosa wazazi wote wawili huku wengi wao wakiwa hawana wazazi wote na hivyo kushindwa kupata mahitaji yao muhimu.

“Wengine hapa hatuna wazazi wote wawili, na baadhi wanamzazi mmoja, kwa hiyo maisha ya kulelewa na ndugu wengi wetu tunanyanyasika na ndiyo tunafikia hatua ya kukimbia nyumbani na kukimbilia mitaani,” Alisema Julius.

Regina makombe naye mmoja wa watoto hao, amesema kwa upande wao watoto wa kike wanakumbana na changamoto kubwa, ikiwemo ya kufanyiwa vitendo vya ukatili kama kubakwa na kufanyishwa kazi zilizo juu ya uwezo wao.

Regina amesema vitendo vya ubakaji wanavyofanyiwa  baadhi ya watoto wa kike, vinasababisha  ongezeko kubwa la watoto wa mitaani, kwani wanaume wanaofanya vitendo hivyo huwa hawako tayari kuwahudumia, na hivyo watoto nao kuingia katika kundi hilo kwa kukosa mahitaji.

Baadhi yetu wanakolala huko wanakutana na mengi sana, wengine wanabakwa, na hili ndiyo linachangia ongezeko la watoto wa mitaani, unakuta mwanaume aliyembaka au kumpa mimba msichana hataka kufahamika na hivyo mtoto akizaliwa hapatu huduma, naye anaingia kwenye kundi la watoto wa mitaani,” Alisema Regina.

Aidha amesema baadhi ya walezi na wasamalia wema ambao hujitokeza kuwasaidia wamekuwa wakiwafanyisha kazi ngumu, ambazo zipo juu ya uwezo wao jambo ambalo n alo pia ni ukatili, kwani wengi wao huwachukua watoto wa kike kwa kisingizio cha kuwasaidia lakini huwafanyisha kazi kama wafanyakazi wa ndani.

“Tunaiomba serikali iingilie kati hali hii, kwani sisi ndiyo Taifa la kesho, tukikosa elimu basi taifa letu litakosa watu wa kuliongoza,” Walisema.

Watoto hao wenye uwezo mkubwa wa akili na fikra yakinifu, zinazokwenda sambamba na wakati wameitaka jam ii kubadili mawazo juu yao kwakuwa katika jamii wanaonekana kama ni watoto watukutu na wasio na uwezo wa akili.

“Tunaiomba jamii itusaidie, isiyaachie mashirika kama haya au ya dini na asas za kiraia, tunawaomba watusaidie kwa kutupa mahitaji muhimu, kwani na sisi ni sawa kabisa na watoto wengine ila tu tumekosa wazazi na mahitaji,” Walisema kwa huruma.

Zakaria Kisinda- mkurugenzi wa kituo TZ – 133 wa kanisa la Tanzania Assemblies of  God TAG amesema jumla ya watoto waliohudhuria kongamano hilo ni 320, huku walimu wao wakiwa 20, na tatizo kubwa linalowakumba watoto hao ni pamoja na wazazi na walezi wao kutowajibika hatua inayopelekea baadhi ya watoto kukimbia makazi yao kwa kukosa huduma.

“Kambi letu lilikuwa na madhumuni makubwa ya kuwakutanisha watoto hawa ambao tunawahudumia, ili wapate kitu cha pamoja kwani tumewaandalia masomo mbalimbali ikiwa pamoja na kubadilishana mawazo kwa kutambua changamoto zitakazoweza kuwakumba kwani baadhi yao hapa wapo kwenye umri wa ujana, na hao tunawapa masomo ya madhara ya Ngono,” alisema Kisinda.

Amesema kambi hilo linalofahamika kama “Vijana wenye matumaini kwa Yesu” limeandaa masomo yanayowahamasisha kujituma kwa bidii shuleni, kuwaheshimu  na kuwatii wakubwa wao, ikiwa pamoja na madhara ya Ugonjwa wa ukimwi na madhara yake.

Kisinda amesema uwepo wa watoto hao ni wazazi wengi kutowajibika na kujisahau kwa kutotimiza wajibu wao kwa kutotoa mahitaji ya msingi kwa watoto wao, kama kuwafuatilia katika masomo, kwa kuwa baadhi yao wanakwama kwenda shule kwa kutokufuatiliwa.

“Kitu ambacho tumekigundua ni wazazi wengi wamejisahau na kuona kutoa huduma kwa watoto ni jukumu la serikali, mashirika na asas za kiraia,  hawawapi mahitaji ya msingi kama ya kielimu pamoja na upendo, lakini changamoto kubwa ni kutokujali, wazazi na walezi wengi hawaoni umuhimu wa kuwajibika, nahii inatokana na ukosefu wa “elimu ya uzazi na malezi,”  wengi wanasema sababu kubwa ni kipato duni, hiyo si sababu ya mzazi kutomuhudumia mtoto wake.

Amesema jamii pia inapaswa kuwajibika kuwasaidia watoto hao kwa kuwapati mahitaji muhimu hasa ya kielimu, kwa kuwa watoto hao wanao uwezo mkubwa wa kusoma huku wengi wao wakiwa na malengo mbalimbali ya kuwa Wabunge, wachungaji nk, na ili wafikie malengo hayo jamii inatakiwa kujitoa kuwasaidia kwa hali na mali.

Zakaria Kisava- Mkurugenzi wa kituo cha Compassion TZ – 232 ELCT Kihesa amesema jumla ya watoto 3600 wanahudumiwa na shirika la Compassion mkoa wa Iringa huku kukiwa na vituo 12, ambapo vituo 8 vinapatikana Manispaa ya Iringa huku vituo 4 vikipatika eneo la Ilula katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.

Kaimu afisa ustawi wa jamii mkoa wa Iringa, ambaye ni afisa ustawi wa jamii Manispaa ya Iringa  Josepnine Mwaipopo amesema chanzo cha uwepo wa kundi hilo wa watoto Yatima na waishio katika mazingira magumu na hatarishi ni ugonjwa wa Ukimwi.

Mwaipopo amesema asilimia kubwa ya watoto wa mitaani wazazi wao wamefariki kwa ugonjwa wa Ukimwi, huku baadhi yao wakiwa na mzazi mmoja, na kutokana na uwezo mdogo wa mzazi au mlezi aliyeachiwa mtoto/watoto ndipo huamua kukimbilia mitaani kutafuta riziki.

Aidha Mwaipopo amewataka watoto hao kutoa ushirikiano wa kuwataja watu wanaowafanyia ukatili, ili sheria iweze kuchukuliwa dhidi yao katika kufanikisha mpango wa kutokomeza tatizo hilo kwa watoto.

“Watoto wengi mnafanyiwa ukatili na wazazi wenu, walezi wenu na hata watu baki lakini mmekuwa wasiri hamuwataji, tunawombeni mtoe ushirikiano wa kuwataja wanaowafanyia vitendo hivyo, uwe umefanyiwa wewe au umemuona mwenzio kafanyiwa ukatili toeni taarifa,” alisema Mwaipopo.

Hata hivyo Mwaipopo amesema nao akinamama na wanawake ambao waume zao wanawafanyia ukatili watoto wao wamekuwa hawatoi ushirikiano wa kuwataja, kwa kuhofia wenza wao hao  kufungwa na hivyo familia kukosa malezi, na kuwa ugumu huo na kukosekana kwa ushirikiano baina ya maafisa na mashuhuda ndiyo sababu ya kesi nyingi kukwama kwa kukosa ushahidi.

MWISHO



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni