Jumanne, 24 Juni 2014

NSSF- WAAJIRI WACHANGIA ONGEZEKO LA WATOTO WA MITAANI



 
 Baadhi ya watumishi wa shirika la Taifa la hifadhi ya jamii  NSSF mkoa wa Iringa walipowatembelea watoto Yatima wa kituo cha Tosamaganga Wilaya ya Iringa.
 Watumishi wa shirika la Taifa la hifadhi ya jamii  NSSF mkoa wa Iringa wakiwa na baadhi ya watoto Yatima wa kituo cha Tosamaganga Wilaya ya Iringa.
 Baadhi ya watumishi wa NSSF mkoa wa Iringa wakiwa na baadhi ya watoto yatima wa kituo cha Tosamaganga na mlezi wa kituo sister Helena Kihwele.


 <<<HABARI>>>
WAAJIRI wasio wajali wafanyakazi wao ni moja ya sababu ya ongezeko la watoto wa mitaani na waishio katika mazingira magumu na hatarishi – kutokana na wazazi au walezi wao kutopata haki stahiki ya kazi wanazofanya.

Hayo yamezungumzwa na Marko Magheke meneja wa shirika la Taifa la hifadhi ya jamii  NSSF mkoa wa Iringa, wakati akikabidhi misaada mbalimbali kwa watoto yatima wa kituo cha Tosamaganga Wilayani Iringa.

Magheke amesema uwepo wa waajiri wasiojali maslahi ya waajiriwa wao, kwa kutowalipa mishahara wafanyakazi wao kwa wakati,  ni moja ya changamoto ya ongezeko la watoto hao ambao wanakabiliwa na ukosefu wa mahitaji kutoka kwa wazazi au walezi wao.

Aidha Magheke amesema pia changamoto kubwa inayolikabili shirika hilo la NSSF ni waajiri kutowasirisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati- hatua ambayo imekuwa ikileta usumbufu mkubwa kwa wafanyakazi na hata katika familia zao.


Magheke ameitaka jamii kujitolea kwa dhati kuwasaidia watoto hao wenye mahitaji, ikiwa pamoja na kuwatembelea ili kujenga upendo kwa makundi maalumu yenye uhitaji- kwa lengo la kupunguza changamoto zinazoyakabiri makundi hayo.

Sister Helena Kihwele ni msimamizi mkuu wa kituo cha watoto Yatima cha Tosamaganga- amesema kituo kina jumal ya watoto 75 ambao hawajafikisha mwezi mmoja hadi miaka sita, na kuwa changamoto kubwa ni walezi kuwasahau watoto.

“Changamoto hii inatusumbua sana maana baadhi ya walezi hawaji kuwasalimia wala kuwachukua watoto sasa tunapata shida wakati wanapotakiwa kurudi nyumbani, maana umri wa mwisho wa kukaa kituoni hapa ni miaka 6,” alisema.

Amesema kituo kinapokea watoto wasio na mama au wenye mama ambaye ni anatatizo la akili, na kuwa baadhi ya ndugu ndiyo wamekuwa wakiwatelekeza watoto mara tu wanapowafikisha kituoni hapo.

Changamoto nyingine zinazowakabili watoto ni baadhi ya wazazi kushindwa kuwaendeleza kielimu watoto, kwani baadhi ya walezi huwa hawana mwamko wa kuwaendeleza watoto hao, na hivyo kusababisha watoto hao kutoendelea na masomo.

Sister Kihwele amesema licha ya jamii kuwa na mwamko wa kuwatembelea watoto hao lakini serikali imekuwa na mkono mzito katika kuchangia mahitaji ya watoto, tofauti na wananchi ambao wamekuwa wakifika mara kwa mara kituoni hapo na kutoa misaada mbalimbali ya kijikimu.


Hata hivyo sister Epifania Mbigi ambaye ni mmoja wa walezi wa kituo cha watoto hao amesema jambo kubwa wanalokosa watoto hao ni upendo wa wazazi, nkwani  baadhi ya walezi baada ya kupokelewa watoto wamekuwa wakiwatelekeza na hivyo watoto kukosa mwelekeo hata muda wa kuishi kituoni unapokwisha.

Sister Mbigi amesema licha ya upendo mkubwa wanaouonyesha kwa watoto hao kwa kuwapa mahitaji mbalimbali – lakini upendo wa mzazi humfanya mtoto awe na furaha ya moyo, huku akisema changamoto kubwa ya kimalezi ni baadhi ya watoto kutokuwa na afya njema.

Amesema uwepo wa ugonjwa hatari wa ukimwi ni moja ya sababu ya ongezeko la watoto yatima na waishio katika mazingira magumu, huku hali hiyo ikisumbua pia baadhi ya watoto ambao wanakuwa bado hawajagunduliwa kuwa wanaukosefu wa kinga mwilini “Ukimwi” ambao wanakuwa wameambukizwa na wazazi wao.

Mkoa wa Iringa bado unakabiliwa na changamoto ya watoto yatima wanaorandaranda mitaani, licha ya kuwa uongozi wa mkoa umefanya jitihada za kuwapunguza watoto hao kwa kuzitaka Halmashauri kuhakikisha watoto hao wanarudishwa nyumbani kwao na kuacha tabia ya kuombaomba mitaani.
MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni