Ijumaa, 20 Februari 2015

SIDO IRINGA YAWAKOPESHA WAJASIRIAMALI WADOGO ZAIDI YA SH MILIONI 229.9

 
 na fredy mgunda,iringa
 
SHIRIKA la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO), mkoani Iringa limetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 229.9 kwa wajasiriamali wa mkoa huo, katika kipindi cha July mpaka Desembea mwaka jana.
 
Akizungumza na uhuru, Kaimu meneja wa SIDO mkoani Iringa, Niko Mahinya alisema lengo la mkopo huo ni kuwawezesha wajasiriamali wadogo kupata mitaji, na kuinua uchumi wao ili waondokane na umaskini.
 
Alisema mikopo hiyo ilitolewa kwenye vikundi mbalimbali vya wilaya zote za mkoa wa Iringa na wajasiriamali mmoja mmoja, ambao kupitia SIDO wamefanikiwa kiuchumi.
 
 “SIDO imekuwa ikitoa mikopo kwa wajasiriamali kwa masharti naafuu tofauti na taasisi nyingine za kifedha ili na riba ndogo ili kukuza mitaji yao, ”alisema.
 
Alisema lengo la kutoa mikopo hiyo, ni kuwasaidia wajasiriamali na wananchi wasiokopesheka kwenye mabenki na taasisi nyingine za kifedha.
 
Alisema mikopo hiyo ni rahisi zaidi kwa vikundi kwa madai kuwa wanachama wamekuwa wakidhaminiwa na vikundi vyao, ambavyo ikiwa mwanachama huyo atakimbia basi kikundi hicho kitabeba mzigo wa kumlipia.
 
Alitaja changamoto kubwa inayowakabili hasa kwa wajasiriamali wa mijini kuwa ni kutorejesha mikopo yao, jambo ambalo linasababisha usumbufu kwa SIDO na kuwafanya wengine wasikopeshwe fedha hizo.
 
Hata hivyo alisema kuwa mbali na mikopo hiyo, SIDO imekuwa ikitoa mafunzo ya biashara kwa wajasiriamali, ili iwe rahisi kwao kufanya biashara kwa utaalam na kuweza kukuza biashara zao.
 
“Pamoja na mikopo tumekuwa tukitoa mafunzo kwa wajasiriamali wetu na kuwawezesha kushiriki kwenye maonyesho mbalimbali ndani na nje ya nchi, ili kutanua uelewa wa biashara zaidi,”alisema Mahinya.
 
Hata hivyo aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kufanya kazi na SIDO ili waweze kuondokana na ugumu wa maisha ambao umekuwa ukiwakabili kwa kuamua kuwa wajasiriamali.
 
Alisema ikiwa vijana watajikita kwenye ubunifu wa biashara, itakuwa rahisi kuaminiwa na SIDO na hatimaye kupatiwa mikopo midogo midogo inayoweza kuwafikisha kwenye hatua ya kukopesheka na taasisi nyingine.
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni