Mto Ruaha mkuu.
Marehemu Azimio enzi za uhai wake.
Marehemu Azimio- enzi za uhai wake.
Mwili wa marehemu Azimio ukiwa umeonekana.
Mwili wa marehemu Azimio ukiwa umeopolewa majini.
Baadhi ya wananchi wakiwa wameuzunguka mwili.
Askari Polisi wakiondoka na mwili eneo la tukio kuelekea Hospitali kwa ajili ya uchunguzi.
<<<HABARI>>>
WANANCHI wa Kata
ya Ruaha katika eneo la Ipogolo, ndani ya Manispaa ya Iringa - nusura wazue tafrani
ya patashika na nguo kuchanika, baada kudai kuchoshwa na uzembe unaofanywa na
baadhi ya Polisi.
Wakilalamikia
hali hiyo kwa madai ya kutelekezewa ndani
ya maji mwili wa marehemu, anayedaiwa
kuuawa na kisha kutupwa katika mto mkuu Ruaha mkuu, mwili ambao umekaa katika
maji kwa muda wa siku tano.
Marehemu aliyefahamika
kwa jina la Azimio Mwanilwa ambaye kwa jina alilopewa na wazazi wake aliitwa “Augustino
Mwanila”, kifo kinadaiwa kilitokana na
kipigo, kutoka kwa majambazi, ambao walimvamia, alipokuwa njiani akielekea
vijijini kununua bidhaa ya biashara yake, tukio lililotokea katika barabara ya Ipogolo
– Kilolo Wilayani- katika eneo la Chuo cha maendeleo ya jamii Tagamenda Manispaa ya Iringa.
Wananchi hao walisema
idara ya Polisi inayojihusika na matukio ya majanga na vifo katika kituo cha Polisi
kati Iringa, pamoja na kikosi cha zimamoto, wamekuwa wazembe kutekeleza wajibu
wao kwa wakati, jambo linalosababisha hasira na hivyo kutokuwepo kwa
ushirikiano mzuri.
Akizungumzia
hali hiyo kandokando yam to Ruaha mkuu - Rehema Kidava amesema tangu litokee
tukio la kuzama majini kijana “Azimio”, hakuna ushirikiano wa aina yoyote
kutoka kwa idara hizo za jeshi la Polisi, jambo lililowalazimu wananchi kuhangaikia
shughuli za kuutafuta mwili huo majini.
Grace Mgimwa na Grolia Mbimbi nao wamekinyoshea kidole
Kikosi cha zimamoto Iringa, kwa madai ya kutokuwa bega kwa bega nao, katika
shughuli hiyo ya uokozi wa mwili wa marehemu, jambo ambalo limewalazimu wananchi kuacha
majukumu yao na kushinda katika eneo hilo la mto Ruaha wakihangaika uuopoaji wa
mwili.
Zenaide Nzeukia
amesema kumekuwa na tofauti juu ya matukio ya ukamataji na matukio ambayo
wananchi wanaomba msaada, hususani yanayohusisha vifo, huku akisema yale ya
kukamata wauzaji wa dawa za kulevya, wanywaji wa pombe za jadi “Kienyeji”, na
hata wachezaji wa michezo ya kamali – Polisi wamekuwa wakifika kwa muda
muafaka, tofauti na matukio yanayotoa usaidizi kwa wananchi.
Yakob Fyimagwa mwenyeviti
wa mtaa wa Buguruni – Ipogolo, miongoni mwa mitaa inayozungukwa na mto mkuu wa
Ruaha katika eneo la tukio, amesema kinachoudhi ni baadhi ya askari wa vikosi
hivyo vya Polisi - kupuuzia majukumu yao, kwa madai kuwa shughuli hiyo ya
uokoaji wa mwili uliopo ndani ya maji ni yao Polisi kitengo cha Zimamoto.
Fyimagwa amesema
endapo Polisi hao hawatabadili utendaji wao wa kazi, basi kuna hatihati ya
kuvunjika kwa ushirikiano baina ya wananchi na jeshi hilo.
“Tunashangazwa
kweli na hawa Polisi kuwa mpaka leo hii ni siku ya tano hawajafika katika tukio
hili licha ya kuwa taarifa zilitolewa mapema siku ile ile ya tukio, lakini yangekuwa
ni matukio yanayohusiana na ukamataji wa waharifu au hata wanywaji wa pombe za
jadi huko vilabuni, wangekuja kwa wakati tena wakiwa wengi utadhani wanakwenda
vitani, …kwani wanajua baada ya kuwakamata watuhumiwa wananufaika kwa kupewa
chochote, lakini hapa siku ya tano hawajafika kama unavyoona tunahangaika tu, na
msiba unakuwa mrefu kwa sababu tu ya uzembe wa baadhi ya watu wachache ambao
wanalipwa mishahara kwa kazi hii,” Walisema wananchi.
Kwa upande wa
wazamiaji binafsi wa majini waliokuwa wakiendelea na shughuli ya uogeleaji
kuutafuta mwili wa Marehemu Azimio, wao walidai kuwa kuna umuhimu kwa Jeshi la
Polisi kikosi cha Zimamoto na Maokozi - kuona umuhimu wa kuwawezesha vifaa, ili
kuifanya kazi hiyo kwa utaalamu na tahadhari.
Fredy Kibasa,
Paulo Kitamuka, Saimoni Magubike na Fredy Kilumbi ni miongoni mwa waogeleaji (Waokozi Binafsi) wa majini, wamesema
mto Ruaha una wanyama mbalimbali kama Viboko, Mamba na wengine ambao ni hatari
kwa usalama wao, lakini hulazimika kuifanya shughuli hiyo ndani ya maji
pasipokuwa na kifaa chochote jambo ambalo ni hatari kwao, na lengo likiwa ni kuopoa
miili ya watu isiharibike au kupotelea majini.
Naye Ismail
Mlenga ( Baba Mwadhani) mlezi wa kikundi hicho cha Uokozi majini, alisema
matukio ya majini hayana tofauti na maafa, na hivyo kuna umuhimu kwa taasisi
zinazohusika na shughuli hiyo, kwa maana ya Polisi na kikoisi cha zimamoto kufanya
kazi zao kwa weredi, kwa madai kuwa kutelekeza mwili wa mtu aliyetumbukia
majini ni kuwapa wakati mgumu ndugu wa marehemu na wananchi, kuomboleza kwa
muda mrefu wakati wakiendelea kutafuta maiti.
Baba Mwadhani
amesema Kikosi cha zimamoto kinapaswa kijitadhmini upya katika utekelezaji wake
wa majukumu, huku nao Polisi wakiacha tabia ya kufanyakazi kwa mazoea na sasa wanapaswa kutekeleza wajibu wao
ipasavyo, bila kusubiri kushinikizwa wala kusukumwa.
Kamanda wa
kikosi cha Zimamoto mkoa wa Iringa, Keneth Komba alipotafutwa kwa njia ya simu
- ili kujua nini kinawakwamisha kufanya kazi hiyo ya uokozi iliyopo ndani ya
idara yao, alisema yupo safarini kuelekea mkoani Ruvuma- ambako amepata taarifa
ya mzazi wake kuugua, huku akiahidi kulishughulikia jambo hilo, kwa kuiagiza
ofisi yake ifike katika eneo hilo.
Siku ya tano
mwili ukiwa ndani ya maji ya mto mkuu Ruaha- majira ya saa sita na dk 35 kikosi
binafsi cha wazamiaji majini, kilifanikiwa kuuona mwili huo wa kijana Azimio,
ambapo viongozi wa mitaa iliyopo eneo hilo la Ipogolo kwa njia ya Simu walitoa
taarifa kituo cha polisi juu ya kupatikana kwa mwili huo, kama ni moja ya
taratibu ya vifo vya aina hiyo.
lengo la
utaratibu huo ni kutambua sababu za kifo na kisha wananchi kupata ridhaa kutoka
kwa polisi, kuzika mwili na hiyo huwa ni mara baada ya Daktari kupima… – lakini
hali ilikuwa tofauti, baada ya polisi tena kudaiwa kuchelewa kufika katika tukio hilo,
kwa takribani saa tatu, huku mwili huo ukiwa juani ukieendelea kubadili
muonekano wake wa awali, jambo lililozua hasira kwa wananchi.
Mara baada ya askari
Polisi kuwasili eneo hilo, kilizuka kituo kingine, kwani wananchi waliwataka polisi
hao wafike eneo la tukio – jambo ambalo
baadhi ya askari walisema wanashindwa kulifikia eneo lililokuwa limewekwa mwili
huo, kwa kile walichodai kuwa kuna maji na tope na hivyo kuwawia vigumu kupita
katika mazingira hayo.
Tope hilo lililowakwamisha
baadhi ya askari ni lile linalotokana na mto Ruaha mkuu kuchepusha maji yake
mara baada ya mvua kunyesha, suala ambalo wananchi hawakukubaliana nalo na endapo
viongozi waliokuwepo wasingetumia busara kuwapoza ghadhabu wananchi hao basi ingetokea
Vurugu ya majini.
Mmoja wa askari Polisi
ambaye hakufahamika jina, aliyekuwa wa kwanza kuingia katika tope na maji ya
eneo hilo pasipo kujali – alizungumza na wananchi kwa upole akiwataka wavute
subira wakiwangoja wengine ambao walitumia muda mrefu tena kufika eneo hilo,
kwani iliwalazimu kutafuta eneo kavu la kupita.
Busara za askari
zilitawala!!,….Kwani hata wananchi walipotumia lugha za kuudhi askari walionekana kutojali, na lengo hapo lilikuwa
ni kupunguza ghadhabu za wananchi hao ambao walikuwa wakitamka maneno makali
kwa hasira za kutelekezewa majukumu hayo ya uokozi wa mwili wa mpendwa wao.
Msemaji wa kikosi cha polisi kilichotinga eneo la
tukio, aliwasihi wananchi, huku akiwaeleza sababu za wao kuchelewa ikiwa ni
pamoja na kumfuata daktari wa upimaji, na kuwaomba wananchi waache jazba na wafanye kazi kwa ushirikiano… jambo
ambalo ndugu wa marehemu na wananchi zaidi ya 200 waliokuwepo katika eneo hilo
walilidhia.
Idadi kubwa ya
wananchi waliofika katika eneo la tukio hilo, iliwawia vigumu askari polisi
kuwapanga katika utaratibu ambao ungefaa, ili
mwili huo ufanyiwe uchunguzi papo
hapo na daktari, na kuwawezesha wananchi kuendelea na taratibu za Mazishi.
Msongamano huo
wa watu ulikwamisha mwili huo kufanyiwa uchunguzi, kama ilivyotakikana awali, jambo
ambalo msemaji wa kikosi cha polisi aliwaeleza wananchi ugumu wa kufanya
uchunguzi eneo hilo, na kisha kuwaomba baadhi ya ndugu wa marehemu waambatane
pamoja kuelekea Hospitali ya Rufaa mkoa wa Iringa – ambako huko ndiko daktari angeweza
kuifanya kazi yake hiyo kwa ufasaha jambo lililopokewa kwa mikono miwili.
Kwa mujibu wa Noel
Mwanilwa- Pacha wa marehemu Azimio Mwanilwa – na David Charles Mwanilwa kaka
mkubwa wa marehemu- majira ya saa moja jioni mwili wa marehemu Azimio ulizikwa
katika eneo la Tagamenda, ambapo marehemu ameacha mke na watoto sita.
Marehemu Azimio
alikuwa ni mfanyabiashara wa Kuku katika Kituo kidogo cha mabasi cha Ipogolo,
na hata mauti yake kumfika, inasadikiwa kuwa alikuwa akielekea kununua Kuku
katika Wilaya ya Kilolo- Iringa, ambapo watu wasiofahamika walimvamia majira ya
saa kumi na moja alfajiri akiwa anakwenda kununua malighafi yake hiyo ya
biashara.
MWISHO.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni