Baadhi ya Wananchi wa Kata ya Ipogolo mjini Iringa wakisikiliza elimu kwa njia ya burudani, inayotolewa na mradi wa "Haki ya afya ya uzazi kwa vijana tuitetee" mradi uliopo chini ya shirika la AMREF na SIDA.
Wananchi wa Ipogolo mjini Iringa wakitazama burudani katika tamasha hilo la "Road Show".
HABARI
LICHA ya asas mbalimbali na serikali kutumia kila mbinu kuwahamasisha vijana kujitokeza kupima afya zao, hasa kujua hali ya maambukizo ya Virus vya Ukimwi (VVU) bado kundi la vijana limeonekana kukwepa huduma hiyo na hivyo kuangamia kwa ugonjwa wa Ukimwi.
Hayo yamezungumzwa afisa utetezi na sera ya afya ya uzazi kwa vijana Meshack Molel, wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Ipogolo mjini Iringa katika mafunzo ya huduma rafiki kwa vijana juu ya afya ya uzazi kupitia mfumo wa burudani za barabarani.
Molel amesema mradi wa haki ya afya kwa vijana ambao upo chini ya shirika la AMREF na SIDA umeamua kuwafikia vijana kwa kutumia burudani mbalimbali ili kuwahamasisha kupima VVU ikiwa pamoja na kuwapa elimu ya ushauri nasaha ingawa bado kundi la vijana halina mwamko mkubwa wa kujitokeza kupima VVU na kuishia kutazama burudani pekee zinazotolewa.
Aidha Molel amesema wameamua kutumia njia hiyo ya utoaji wa burudani barabarani (Road Show) ili kuwakusanya vijana wengi na hatimaye kuwafikishia ujumbe unaohusu afya ya uzazi ikiwa pamoja na kuwataka wapime VVU.
Filbet Temba mshauri nasaha wa kituo cha angaza kutoka jijini Dar es salaam amesema licha ya uwepo na idadi ndogo ya vijana kupima VVU lakini baada ya kufikiwa na elimu imewapa msukumo wa kujua afya zao tofauti na siku za nyuma.
Temba amesema asilimia kubwa ya vijana wanaojitokeza kupima afya wamekuwa wakipatiwa huduma ya ushauri nasaha ili kuwaepusha na tabia ya ngono zembe ambayo kwa kiwango kikubwa vijana wengi wamekuwa wakipata maambukizi hayo ya VVU kutokana na kutotumia kinga hasa Kondom.
Amesema elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ni muhimu kwani kundi hilo ndilo muhimili wa Taifa, na changamoto kubwa kwa kundi hilo wengi wao hawatumii kondomu huku baadhi yao wakiwa hawana kabisa elimu sahihi ya matumizi ya kondomu licha ya kuwa tayari wamejiingiza katika mahusiano ya kimapenzi.
Naye Christina Kiwanga mmoja wa vijana amesema mpango huo wa utoaji wa elimu ya afya ya uzazi kupitia maonyesho ya barabarani ni mzuri kwani baadhi ya vijana wamekuwa wakiogopa kufika katika vituo vya afya, kwa kuhofia wahudumu wasio na maadili ambao hutoa siri.
Hata hivyo Amani Gwendumi mmoja wa vijana amesema wao wamekuwa wakiogopa kupima kutokana na baadhi yao kushiriki ngono zembe na hivyop kuwa na hofu juu ya afya.
Gwendumi amesema mpango huo wa kuwafuata vijana katika maeneo mbalimbali itasaidia kwa kuwa wanashindwa kufika katika vituo vya upimaji na ushauri nasaha kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya muda wa kufika huko.
"Huduma hii itatusaidia sana sisi vijana kwani wengi wetu hatuna muda wa kwenda huko kwenye vituo vya upimaji, lakini wakitufuata kwenye maeneo yetu haya na kutupa elimu inatupa hamasa ya kusikiliza elimu wanayoitoa na pia tutaelimika na kujitokeza kupima, hii ni kweli kuwa vijana wengi tunashiriki ngono kama starehe lakini tukielimishwa tutaachana na tabia hiyo ambayo ni hatari kwa afya zetu," alisema Gwendumi.
Mkoa wa Iringa wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa asilimia 9.1 inasemekana asilimia 60 ya maambukizo hayo ni vijana ambao ndiyo tegemeo kuu na muhimili katika ujenzi wa Taifa, huku Mkoa huo ukiwa wa pili kwa maambukizo ya juu kitaifa ukifuatiwa na mkoa wa Njombe ambao awali ulikuwa ndani ya Mkoa wa Iringa.
MWISHO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni