Jumatano, 26 Februari 2014

CCM YAWATAKA WANANCHI KUHOJI MSHAHARA WA DR. SLAA


 Mgombea ubunge wa jimbo la kalenga kupitia chama cha mapinduzi CCM - Godfrey Mgimwa akisalimia na wazee wa jimbo hilo, katika moja ya mikutano yake ya kampeni.

 "Twende zetu" kampeni meneja wa CCM jimbo la Kalenga Bw. Meja Mbuta (wa kwanza kushoto) akiwa na mgombea ubunge jimbo hilo la Kalenga Godfrey Mgimwa pamoja na baadhi ya viongozi wa CCM wakielekea katika kampeni.

 Mgombea Godfreu Mgimwa akizungumza na wananchi katika moja ya mikutano yake ya Kampeni za kuwania ubunge wa jimbo la Kalenga.

<<<<<HABARI>>>>>
kwa hisani ya Frenk Leonard

KATIBU wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mufindi, Miraji Mtaturu amewataka wananchi wa Jimbo la Kalenga kujua kiasi cha fedha anazolipwa Dk Wilbroad Slaa kila mwezi ili waoanishe na harakati zake anazodai zinalenga kupinga ufisadi.

Dk Slaa ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema); yupo wilayani Iringa akiongoza kampeni za kumnadi Grace Tendega anayegombea ubunge katika jimbo hilo kupitia chama hicho.

Katika mikutano ya kumnadi mgombea wao Godfrey Mgimwa iliyofanyika katika vijiji vinne vya kata ya Kiwele jana, Mtaturu alisema Dk Slaa ndiye kiongozi wa chama cha siasa nchini anayelipwa fedha nyingi kuliko mwingine yoyote.

Alisema katika mazingira ambayo wanachama na baadhi ya viongozi watendaji wa Chadema wanatumia fedha zao za mifukoni kujenga chama hicho, Dk Slaa analipwa zaidi ya Sh Milioni 10.

“Muulizeni akija hapa ni kiasi gani analipwa kila mwezi; aliwekwa sharti la kulipwa kiwango kinachofanana na kile wanacholipwa wabunge kama sharti la kukubali kugombea urais badala ya ubunge katika Uchaguzi Mkuu uliopita,” alisema.

Alisema mtu anaweka masharti na kutanguliza maslai yake mbele katika kazi ya kuwatumikia wananchi hafai kuwa kiongozi na ni muhimu kuwa makini na kauli zake.

Katika mikutano iliyofanyika katika vijiji vya Mgera, Kiwele, Mfyome na Kitapilimwa, Mtaturu aliwaomba wananchi wa jimbo la Kalenga kutofanya makosa katika uchaguzi huo.

“Kazi anayokwenda kumalizia Godfrey Mgimwa ilikwishaanza kufanywa na marehemu Dk William Mgimwa; mpeni kura zenu zote ili akamalizie utekelezaji wa Ilani ya CCM,” alisema.

Akijinadi kwa wapiga kura wa kata hiyo, Mgimwa alisema “sijagombea nafasi hii ili niharibu kazi inayoendelea kufanywa na chama changu, sikugombea ili kupotosha ukweli wa yale yote yanayoendelea kufanywa, ninagombea kwasababu nataka kumalizia kazi,” alisema.

Alisema akiwa mbunge katika jimbo hilo atahakikisha kwa kushirikiana na wapiga kura wake anamalizia utekelezaji wa ahadi mbalimbali za maendeleo zilizotolewa na CCM kupitia Ilani yake ya 2010 na zile zilizoachwa na marehemu baba yake.

“Najua katika kata hii kuna changamoto zinazoendelea kupatiwa ufumbuzi; nipeni nafasi nikazishughulikie,” alisema na kuzitaja changamoto hizo zikihusisha sekta ya maji, afya, barabara, pembejeo, elimu na mawasiliano.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa, Delfina Mtavilalo alisema katika uchaguzi huo Chadema itashika nafasi ya pili kama inavyojidhihirisha kupitia salamu yao.

“Vidole viwili havina maana nyingine zaidi ya namba mbili na ndio maana kila wanapopita wanaonesha wao ni namba mbili kwa kuonesha ishara ya vidole hivyo,” alisema.

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga alisema wananchi wa Kalenga watakosea kama watampa ubunge mtu ambaye hawajui watampata wapi.

Alisema CCM inawajibika kwa wananchi na ndio maana ina mfumo wa uongozi kutoka ngazi ya tawi hadi taifa tofauti na Chadema.

Akiahidi kutoa zawadi ya fedha kwa wananchi wa kata ya Kiwele kama watamtajia safu ya viongozi wa chama hicho katika jimbo hilo, Mtenga alisema bado hakiaminiki na ndio maana kinakosa viongozi katika nafasi zake mbalimbali.

“Ulizeni kama chama hicho kina viongozi wa kuchaguliwa kwenye kata zake na kama kina uongozi wa wilaya uliokamilika,” alisema.

MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni