Jengo la idara ya ujenzi wilaya ya kilolo, ambalo watumishi wake wametiliwa mashaka juu ya utendaji wao wa kazi.
Jengo la halmashauti ya Wilaya ya Kilolo- Mkoani Iringa
<<<<HABARI>>>>
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya
Wilaya ya Kilolo limemuagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo kufuatilia ofisi ya
mhandisi wa halmashauri hiyo na wakandarasi juu ya watumishi wanaopewa kazi.
Madiwani hao wameonesha hofu ya
kuwepo kwa rushwa katika idara hiyo ya ujenzi hasa kutokana na kandarasi nyingi kujengwa
chini ya kiwango, na hivyo kuigharimu serikali juu ya fedha ambazo ni kodi ya
wananchi.
Kikao hicho kilichofanyika Ijumaa
iliyopita mjini Kilolo kKatika kikao hicho, baadhi ya madiwani wake wamesema
kazi nyingi za barabara zimekuwa zikitengenezwa chini ya kiwango na kuwa huenda
wakandarasi wanaopewa kazi hizo ni wale wasio na sifa.
“Tuna hofu na hatuna sababu ya
kuficha hisia zetu, huenda wakandarasi wanaopewa kazi hizi kwasababu zile zile
zilizojificha wakawa ni wale wasio na sifa au wale wanaotumia leseni za watu
wengine ili kujipatia fedha,” alisema diwani wa kata ya Idete, Bruno Kauka.
Kauka alisema barabara nyingi
zinazotengenezwa wilayani humo huaribika baada ya muda mfupi na kuleta adha
kubwa kwa watumiaji wake vikiwemo vyombo vya usafirishaji.
Bila kumtaja jina, alitoa mfano wa
mkandarasi aliyepata tenda ya kujenga daraja linalounganisha kijiji cha
Kiwalamo na Idete Juni, 2013.
Pamoja na kupewa fedha, mkandarasi
huyo ameshindwa kuifanya kazi hiyo hali iliyosababisha mawasiliano ya barabara
kati ya vijiji hivyo vinavyotengenishwa na mto Lukosi kukatika.
Alisema zaidi ya wananchi 2,600
wameathiriwa na ukosefu wa huduma hiyo hali inayofanya shughuli zao za
kibinadamu zikiwemo za kwenda mashambani na kwenye vituo vya huduma za afya
ziendelee kuathirika.
Alisema ili wananchi wa kijiji cha
Kiwalamo waweze kufika kijiji cha Medege na kupata huduma mbalimbali zikiwemo
za afya wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 20 kwa kuzunguka kupitia kijiji
cha Kidabaga, badala ya tano kwa kupitia
darajani hapo.
Malalamiko ya diwani huyo yaliungwa
mkono na madiwani wengine akiwemo Anna Msolla wa kata ya Ilula, Israel Mwilafi
wa kata ya Ukwega, Fabiola Nzasule wa kata ya Mazombe, Mejusi Mlieveke wa kata
ya Kimara na Auzilio Mbilinyi wa kata ya Mtitu.
Madiwani hao walisema halmashauri
hiyo inaendelea kutoa tenda kwa wakandarasi wanaonesha kutokuwa na uwezo pamoja
na kulipwa fedha nyingi.
“Hatuelewi hizi barabara za vijiji
vya Idete, Kiwalamo, vijiji vya Winome, Mawambala, Ukumbi, Lulindi, Mkalanga,
Makungu, vijiji vya kata ya Udekwa na Mtandika kwanini hazitengenezwi kwa muda
mrefu huku kukiwepo na taarifa za wakandarasi waliopewa kazi hizo wamelipwa fedha...
Wananchi wanalia sana juu ya barabara hizo,” alisema diwani Mbilinyi wa mtitu.
Akijibu malalamiko ya madiwani hao,
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ubald Wampembe alisema kuwa wakandarasi
waliowengi wanapatiwa tenda hizo wakati wa mvua hali inayosababisha wengi
washindwe kuzitengeneza kwa hofu ya kuharibiwa na mvua hizo.
Wampembe amesema Halmashauri hiyo itachunguza
uwezo na uhalali wa wakandarasi hao kupewa kazi hizo wakati wakiendelea
kusubiri mvua zipungue ili ujenzi uendelee.
Kuhusu daraja la mto Lukosi, alisema
Halmashauri walishamwandikia barua mkandarasi huyo kwa kushindwa kutengeneza
daraja la muda wakati akiendelea kufanya harakati za kulitengeneza daraja hilo.
Idara hiyo pia iliwahi kutiliwa mashaka na Naibu Waziri wa TAMISEMI Agrey Mwanry, alipotembelea mkoa wa Iringa na kufanya ziara za kikazi kwa halmashauri zote za mkoa wa Iringa, na baada ya kukagua baadhi ya miradi ya barabara ya Wilaya ya Kilolo na kukuta kasoro, waziri huyo alilazimika kuomba cheti cha elimu ya darasa la saba cha mhandisi wa Wilaya hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni