Baadhi ya wananchi wakiendelea na usafi katika mtaa wa Mlandege manispaa ya Iringa.
Hali ya takataka katika dampo la Mlandege, tuchafu ambao unadaiwa haujazolewa kwa zaidi ya miezi miwili.
Moja ya kontena lililowekwa jirani na manispaa ya Iringa likiwa limechakaa, na hili likiwa na unafuu kwa mengine yanayotumika.
Afisa afya mkuu wa Manispaa ya Iringa, akiwa ofisini kwake akizungumza na mmiliki wa mtandao huu ulipofika katika ofisi hiyo.
<<<HABARI>>>
WANANCHI wa Kata
ya Mlendege katika Manispaa ya Iringa wamefunga barabara ya Meya wa Manispaa ya
Iringa wakiishinikiza manispaa hiyo ya Iringa kuondoa takataka katika madampo ya
mjini Iringa, likiwemo la Mlandege ambalo wamesema limetelekezwa kwa zaidi ya
miezi mitatu.
Wakilalamikia hali
hiyo, wakazi hao wa Mlandege wamesema mlundikano wa takataka katika eneo lao na
maeneo mengine ya mji wa Iringa, ni hatari juu ya kuibuka kwa maradhi ya
mlipuko huku wakitilia shaka ugonjwa wa Dengue.
Chagu Michael Chali amesema takataka hizo ambazo zinatoka katika maeneo mbalimbali
hazijaondolewa kwa miezi mitatu na hivyo kuwepo kwa tishio hasa kwa wakazi
jirani na dampo hilo, na hivyo kuamua kufunga barabara inayoelekea nyumbani kwa
Meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi ili kuishinikiza Manispaa kupeleka
kifaa cha kuhifadhia takataka.
“Tumeamua
kufunga barabara hii anayopita Meya, maana kama kuongea tumeongea vya kutosha
lakini hakuna lolote tunalosaidiwa, wanatupiga kiswahili kila siku hawa Manispaa,
sasa ni bora tufunge barabara hii, hizi takataka ni hatari sana kwa magonjwa ya
mlipuko, na hasa huu ugonjwa wa Dengue unaoenezwa na Mbu anayeng’ata mchana,
ugonjwa huo unaweza ukazuka kupitia takataka hizi, maana hapa tumezungukwa na
vilabu 7 vya pombe za kienyeji, takataka na uchafu wenye maji maji unamwagwa
kwenye dampo hili, wanataka kutuua hawa Manispaa,” alisema Chagu.
Said Mohamed
amesema kukithiri kwa uchafu katika eneo hilo pia kumechangiwa na Manispaa
kuliondoa dampo kwa zaidi ya miezi mitatu, na hivyo wananchi kulazimika kutupa
takataka chini, jambo linalosababisha adha kwenye nyumba jirani na Dampo hilo,
kwa kuwa takataka zimekuwa zikipeperushwa na upepo na kuingia katika makazi ya
watu.
Enock Sanga
amesema mlundikano wa uchafu huo ni hatari zaidi kwa kundi la watoto ambao
wamekuwa wakicheza nje ya nyumba zilizo jirani na takataka hizo, na hivyo
kuitaka manispaa kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa kujituma bila
kushinikizwa.
Akijibu tuhuma
hizo, Meya Mwamwindi amekiri kuwepo kwa uchafu katika eneo hilo, na kuwa sababu
kubwa ni kuwa barabara inayoelekea katika Dampo hilo ilikuwa inatengenezwa kwa
kiwango cha Lami, na hivypo magari ya kuchukua takataka kushindwa kuingia kabla
ya Lami hiyo kukauka.
Aidha Mwamwindi amelaani
vitaka hatua iliyochukuliwa ya wananchi hao kufunga barabara ikiwa pamoja na
kufanya maandamano, na kuwa kulikuwa na njia mbadala ya mazungumzo baina ya
wananci hao na viongozi wao wa eneo husika.
“Hoja ya kwamba
dampo lipo kwenye makazi ya watu si sahihi, kwani Skip Baket zinatakiwa
kutengwa katika maeneo ya wazi, na mwenye kupanga dampo likae wapi ni kamati ya
maendeleo pamoja na mamlaka siyo mtu mwingine, lakini kilichojitokeza pale ni
kwamba barabara pale ilikuwa inatengenezwa, sasa nimeongea na watu wa barabara waone
kama magari yanaweza kuingia pale, tulikuwa tunafanya maendeleo kwani ujenzi wa
barabara ni meneleo na uondoaji wa takataka nayo ni shughuli ya kimaendeleo, kwa
hiyo niombe wawe na subira, lakini hatua waliyoichukua siyo sahihi, siyo ya
kiungwana na siyo ya kistaarabu, na mimi siikubari kabisa,” Alisema Mwamwindi.
Amesema tatizo
kubwa lililopo ni uhaba wa makontena ya kuhifadhia takataka, kwa kuwa yaliyokuwepo
awali kwa asilimia kubwa yameharibiwa kwa kuchomwa kwa moto, na hivyo maeneo
mengi kutokuwa na huduma hiyo.
Mwamwindi amesema
kontena moja linauzwa zaidi ya shilingi Milioni 8, na uhitaji wa Manispaa ya
Iringa ni kontena 100, na hiyo ni kutokana na mji wa Iringa kutanuka na
mahitaji yake kuongezeka kutokana na uzalishaji wa takataka kuongezeka.
Amesema Manispaa
inahitaji jumla ya Kontena 100 ambayo ni
sawa na shilingi Milioni 800 fedha
ambazo ni mapato ya ndani ya Manispaa, na walichokifanya ni kuyafanyia
ukarabati makontena 10 ili yaweze kupunguza tatizo hilo.
Afisa afya wa Manispaa
ya Iringa Mercy Kiwenekejo amesema suala la usafi wa mazingira linaiguza
Manispaa pamoja na jamii, ili kuhakikisha manispaa yao inakuwa safi, na
changamoto ni uhaba wa makontena.
Amesema Manispaa
ya Iringa ina magari mawili ambayo yanatuimiwa kubeba Kontena,
na kuwa sasa Kontena zimebaki 28 pekee
kutoka 56 zilizokuwepo mwaka 2000 kupitia mradi wa Sustainable Iringa Project (SIP).
Kewenekejo amesema
mahitaji ya sasa ni makubwa na upungufu wa
Kontena ya kuhifadhia takataka unatokana na Kontena mengi kuwa chakavu,
na hiyo ni kutokana na baadhi ya wananchi kutupa takataka zikiwa na majivu
yenye moto ambao umeyaunguza madampo
hayo.
Hata hivyo Kewenekejo
amesema juhudi za halmashauri zinaendelea na katika hatua ya awali Halmashauri
imekarabati Kontena (Skip Baket), na katika mwaka bajeti ya mwaka 2015- 2016 kupata
Skip Bajet 50 mpya kutoka mradi wa benki ya dunia (Word Bank) huku Manispaa
ikiwa na mkakati wa kununua gari jipya
la takataka.
MWISHO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni