Rais wa maaskofu tanzania Askofu Ngalalekumtwa akisalimiana na rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa- katika jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu na miaka 40 ya Upadre wa Ngalalekumtwa - sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Kanisa la jimbo la Kihesa Iringa.
Baadhi ya maaskofu.
waziri mkuu Mizengo Pinda akimsalimu askofu Tarcisius Ngalalekumtwa- katika jubilei yake ya Uaskofu na Upadrisho, mjini Iringa.
Waziri mkuu mstaafu- Edward Lowassa akisaliamiana na mmoja wa maaskofu katika jubilei ya askofu Ngalalekumtwa ambaye ni rais wa maaskofu Katoliki Tanzania.
Askofu Ngalalekumtwa ambaye pia ni askofu wa jimbo la Kanisa Katholiki Iringa, akipokea zawadi siku ya jubilei yake- iliyofanyika katika jimbo la kanisa katholiki Kihesa-Iringa.
Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba akimkabidhi Rais Kikwete Rasimu ya pili ya katiba mpya.
KATIKA ujumbe wetu wa
kichungaji wa Pasaka 2014, Sisi maaskofu Katoliki Tanzania, tuliwaandikia barua
watu wote wenye mapenzi mema kwa nchi yetu tukiwaalika kuchukulia maanani
mchakato wa kuandika Katiba mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati huu tena tunawaalika
Watanzania wote kwa pamoja, tuungane kuwakumbusha wale waliopewa dhamana
yakukamilisha rasimu ya pili ya katiba ya jamuhuri ya muungano kuwajibika
binafsi na katika maridhiano kutupatia Katiba Maridhawa.
Kwa moyo wa Sala na
tafakarimakini, tulifuatilia mlivyojadiliana katika BMK kuanzia mwezi Februari
hadi April 2014, katika siku sitini na saba (67)ninyi wateule wa Rais mpatao
mia sita (600).
Mlijadiliana pasipo umoja,
mkishambuliana kwa kauli kali kati yenu, mkikashfiana pasipo udhibiti wa
uongozi mliojichagulia wenyewe kwa kanuni na sheria mlizojitungia.
Mwenendo huu ulikuwa wa
kusikitisha na kuchukiza katika mahali pale panapoheshimiwa na wote, kwani
tulitegemea majadiliano katika kuheshimiana hoja za kizalendo na kiungwana
zitokanazo na mambo na masuala makuu yaliyopendekezwa katika Rasimu ya pili ya
Katiba.
Badala yake tulijionea
mabishano makali na mpasuko uliosababisha upotoshaji wa nia iliyokusudiwa,
hatimaye hila na hilba zikateka kabisa jukumu adili la BMK.
Tukumbuke Rais wa
jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa uthubutu na ujasiri wa kipekee, alianzisha machakato wa kuunda katiba mpya, na
kisha aliridhia kwa kuipokea rasmi kwa furaha Rasimu ya pili ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Ni lazima sasa
tujiulize, nini kimetokea hadi kugeuza kabisa mwelekeo mzima wa mchakato wa
katiba kwa kuikejeri na kushutumu vikali Rasimu hiyo katika wakati wa kipekee
kabisa wa kihistoria wa uzinduzi wa BMK? Hata kusahau gharama kubwa ambayo
ilibebwa na walipa kodi? Na sasa hii inaonyesha dhahiri jambo hili limeiingiza
nchi katika mgogolo mkubwa unaoashiria hatari mbeleni.
Kwa maoni yetu tatizo
hili kubwa ambalo limekuwa kikwazo kikubwa linaonyesha kukosekana utashi wa
kisiasa na wahusika kutokuwa wakweli juu ya suala la mchakato wa katiba.
Tunawaomba wajumbe wa
BMK kuwa wamoja na kufanya kazi yenu kwa mtazamo usioegemea siasa za vyama kuandika katiba ni kazi
iliyo ngazi ya juu zaidi ya siasa za vyama na hivyo utashi wa kisiasa wa kuunda
katiba mpya wa kuzingatia msingi huu.
Kwa kadri ya hali ya
nchi yetu ziko sababu za kutosha za kutaka katiba mpya Sababu hizi ni pamoja na
ufisadi, wananchi kujisikia kukosa usalama, nchi kutokuwa na dira, tunu, msingi
n.k.
Ni kwa hiyo tunawasihi
kwa mara nyingine tena ninyi wajumbe wa BMK kurejea katika sehemu ya pili ya
mjadala hapo mwezi August mkiwa na moyo na mtazamo mpya.
Tunaomba achaneni
kabisa na ubinafsi, uwe wa mtu mmoja mmoja au katika vikundi. Kwa kazi yenu
tusaidieni sisi watanzania tuweze kujivunia kuwa na Taifa adilifu tukifanyakazi
kwa pamoja kwa ajili ya manufaa na ustawi wa wote.
Kumbukeni BMK mnao
wajibu wa kimaadili kwa nchi yetu na vile kwa namna mnavyotekeleza wajibu wenu maandika
historia ya nchi yetu, kubeba dhamana ya kuandika katiba mpya ni wajibu wa
kimaadili kwenu.
Tambueni kwamba
Watanzania hawako tayari kurudi nyuma na kuendelea na maisha yanayoongozwa na
katiba ya mwaka 1977 kwa sababu licha ya mapungufu yake na ukiukwaji mkubwa
ambao umekuwa ukifanyika, kufanya hivyo (Kuendelea kuongozwa na katiba ya 1977)
kutaleta migogolo mikubwa yenye kuhatarisha vikali amani nchini.
Wajibu mliokabidhiwa
ikiwa mtautimiza kwa dhamira njema mtalijengea Taifa letu misingi imara iliosheheni
tunu za kimaadili ambazo ni heshima katika utu wa Mwanadamu, umoja, mshkamano
na kujali na manufaa na ustawi wa wote.
Ni lazima matunda ya
kazi yenu yawe ni kulipatia Taifa dira inayowapa watu msukumo wa kujenga pamoja
Taifa lenye watu wamoja na wanaojaliana kwa stahamala katika tofauti zao.
Wajibu wenu huo ni
mtakatifu na hivyo ni kosa kubwa mno kuusaliti kwa sababu ya ushindani katika
medani za kisiasa au kujitafutia sifa mbele ya watu.
Kwa matokeo yoyote
yatakayotokana na kazi yenu katika BMK Watanzania watawawajibisha, ikiwa
matokeo yatakuwa yenye kuleta mema na kuimarisha amani na utulivu nchini watu
wote watawashukuru na kuwasifu.
Lakini kama tunda la
kazi yenu litakuwa ni lenye kuiingiza nchi katika matatizo zaidi, kuwataabisha
wananchi na kukosa maelewano baina yao, basi watu watawahukumu na kuwawajibisha
kwa kukosa umakini katika jukumu hili muhimu mlilokabidhiwa.
Kwa sasa tunahitaji
Katiba itakayowezesha ushiriki kamili wa watu katika maamuzi ya vipaumbele vya
maendeleo yao ya Taifa. Ni katiba shirikishi katika matumizi ya madaraka ili
yatumike kwa ajili ya kuhudumia wote badala ya wachache.
Tunahitaji katia ambayo
inaruhusu utawala wa sheria, haki sawa kwa wote, manufaa na ustawi kwa wote na
kuheshimu Utu wa kila mmoja, Katiba iwezayo kuzuia matumizi mabaya ya madaraka
na Ufusadi, hicho ndicho wananchi wanachokitarajia kutoka kwenu.
Yeyote anayedharau
hitaji la katiba mpya ama anayejaribu kupuuza na kuweka kando Rasimu ya pili,
huyo siyo mwakirishi wa utashi wa watu, mwisho wake Historia itamuhukumu vikali
mtu huyo.
Wajumbe wa BMK
msiwaangushe watu wenu.
Sisi Maaskofu Katoliki
Tanzania tunawaahidi sala zetu ili mwenyezi Mungu awaangazie Nuru yake na
kuwajalia nguvu ya KiMungu muweze kukamilisha kazi kwa mafanikio kadiri ya matarajio
ya watu wake wa Tanzania.
Tunawaalika watu wote
wenye mapenzi mema kuwaombea wajumbe hao na bunge maalumu la katiba wajaliwe
neema za Mungu.
T. Ngalalekumtwa.
MWISHO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni